Home » » NGARA KATIKA KASHFA YA UBADHIRIFU WA FEDHA

NGARA KATIKA KASHFA YA UBADHIRIFU WA FEDHA

 
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ngara inadaiwa kukumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa fedha za umma katika miradi mitatu kwenye maeneo tofauti hali ambayo Kamati ya Utekelezaji ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera imeamuru irudiwe na kukamilishwa.
Ubadhirifu huo uligundulika baada ya kamati hiyo kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo juzi kwa lengo la kutathmini na kujiridhisha utekelezaji wa Ilani ya chama ya mwaka 2010.
Pia ililenga kujiridhisha kama fedha inayotolewa na serikali ya chama hicho inafanya shughuli zilizokusudiwa na kwa viwango.
Ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera Costansia Buhiye, ilibaini nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Ngoma iliyoko Kata ya Kasulo iliyojengwa kwa gharama ya Sh milioni 45 kuwa chini ya kiwango.
Kamati hiyo iliagiza ndani ya siku saba Halmashauri imtafute mkandarasi aliyejenga nyumba hiyo, aondoe milango, vigae na nyavu za madirisha na kuweka vingine kutokana na vilivyowekwa kuwa chini ya kiwango ikilinganishwa na fedha zilizotumika. Ubadhirifu mwingine umebainika katika Mradi wa Maji katika Kijiji cha Nterungwe Kata ya Nyamihaga.
Ilibainika mradi huo uliojengwa tangu mwaka 2004, maji hayajawahi kutoka licha ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kutenga zaidi ya Sh milioni moja kila mwaka kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mradi huo ‘hewa’.
Kamati ilimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha mradi huo unakamilika haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero kwa wananchi wa eneo hilo ambao hutembea umbali wa kilometa 10 kufuata maji.
Mradi mwingine ni wa upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji Ngara mjini ambao Sh milioni 150 zilitolewa na Rais Jakaya Kikwete. Pia ilibainika katika fedha hizo, zaidi ya Sh milioni 32 zimetumika tofauti na utaratibu.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya kugundua ubadhirifu huo, Meneja wa Mamlaka ya Maji Ngara Edward Magai (60) amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Chanzo;Habari Leo 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa