Home » » RC: FAINI ZA MAKOSA BARABARANI ZIONGEZWE

RC: FAINI ZA MAKOSA BARABARANI ZIONGEZWE

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe ametaka sheria za usalama barabarani, ziangaliwe upya kwa lengo la kuongeza adhabu na faini kwa wanaosababisha ajali.
Akihutubia jana katika ufunguzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mkoani Kagera, alisema sheria ya sasa imepitwa na wakati kutokana na kutoa adhabu ndogo jambo alilosema linawapa jeuri watu wanaosababisha ajali barabarani.
“Maana mtu akifanya kosa la kusababisha ajali, tena ameua mtu eti faini Shilingi elfu 20. Hii inawapa jeuri ya kuendelea kutenda makosa hayo,” alisema.
Alisema madereva hawajali kwa kuwa huchukulia kwamba watalipa faini hiyo ambayo ni ndogo. Alitoa mfano wa Australia, kwamba mtu akitenda kosa kama hilo katika nchi hiyo, hunyang’anywa leseni na haruhusiwi kuendesha gari milele.
Alisema haitoshi kwa polisi kila wakati kuorodhesha ajali zinazoendelea kutokea, ambazo sababu zake ziko ndani ya uwezo wao.
Alihimiza polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, kufuata kanuni na maadili ya kazi yao. Alisema jambo la muhimu ni kutekeleza kwa vitendo majukumu yao na mikakati madhubuti, waliojiwekea kukabili ajali zinazogharimu uhai wa watu.
Katika risala yake, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabara Mkoa wa Kagera, Peter Magayane , alisema ajali nyingi zinatokana na makosa ya kibinadamu, ambayo ni mwendo mkali, ulevi, uchovu na usingizi.
Alisema makosa mengine ni ya kimazingira, kama vile mteremko mkali uliopo eneo la K 9 wilayani Ngara mkoani Kagera
Chanzo;Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa