Baadhi ya wakimbizi wakiwa katika boti tayari kurejea kwao
Na Mwandishi Wetu - MAELEZO
Kufuatia
wito wa Rais John Pombe Magufuli alioutoa hivi karibuni, hadi kufikia
jana tarehe 01 Agosti, 2017 jumla ya wakimbizi 6,700 raia wa Burundi
wameshajiorodhesha kurejea nchini mwao kwa hiari.
Kufuatia
hatua hiyo, Mkutano wa pande tatu utakaojumuisha Serikali za Tanzania,
Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unatarajiwa kufanyika
mwishoni wa mwezi huu kujadili namna ya kuwarejesha nchini mwao
wakimbizi hao kwa kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi.
Katika mahojiano na mwandishi wetu ofisi kwake jana, Mkurugenzi Idara ya Huduma za Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana Harrison Mseke alieleza kuwa tangu kutolewa kwa wito huo, Wizara imekuwa ikiwamahasisha wakimbizi hao wa kujiorodhesha kwa hiari ili waweze kurejea nyumbani.
Akiwa
katika ziara yake kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Magufuli alitoa
wito kuwataka wakimbizi raia wa Burundi kurejea nyumbani kwa hiari kwa
kuwa hali ya usalama nchini mwao ni nzuri ambapo wakati akitoa wito huo
tarehe 20 Julai, 2017 huko Ngara aliambatana na Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunzinza ambaye nae aliwahakikishia wakimbizi hao kuwa hali ni shwari
nchini Burundi.
Kwa
mujibu wa Bwana Mseke, hivi sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 276,692
kati ya wakimbizi 348,019 walioko nchini. Wengine ni wakimbizi kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 70,840, Wasomali 150, na wengine
(mchanganyiko) 337.
Alifafanua
kuwa kati ya idadi hiyo ya wakimbizi raia wa Burundi 242,340 waliingia
nchini baada ya mwezi Aprili, 2015 kufuatia machafuko ya kisiasa nchini
humo.
Akizungumzia mwendo wa uingiaji wakimbizi kutoka Burundi, alieleza kuwa kwa sasa kasi imepungua kutoka wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kati ya mwezi Agosti hadi Disemba, 2016 hadi wastani wa wakimbizi kumi kwa siku katika miezi ya hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment