JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Awamu ya Pili ya Operesheni Kimbunga imeweza
kukamata majambazi ya kutumia silaha 67 na wahamiaji haramu 134 katika kipindi cha wiki moja tangu kuanza kwake Septemba 21hadi Septemba 27
mwaka huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Silaha zilizokamatwa ni pamoja na bunduki aina
ya SMG Moja, Pistol Moja na Magobole 17 pamoja na risasi 115 zikiwemo za bunduki
aina ya SMG 102 na Risasi za Pistol 13. Aidha, Magazine mbili zilikamatwa pamoja
na Sare za Jeshi la Burundi.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni
kutoka nchi za Burundi ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume
na sheria wakati raia wa Rwanda 20 walikamatwa katika kipindi hicho.
Aidha, watu Watatu walikamatwa kwa tuhuma za
kuhifadhi wahamiaji haramu nchini huku Lita 271 za gongo , ngozi ya Mbwea, Bangi
kilo Tatu na Makokoro 12 vilikamatwa wakati wa operesheni Kimbunga awamu ya
Pili ikiwa katika wiki yake ya kwanza.
Wakati huo huo, Wilaya
ya Karagwe mkoani Kagera imejipanga kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu
ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo linafikia mwisho wake na kuwapa nafasi
wananchi kufanya shughuli zao za kijamii na kimaendeleo bila ya hofu ya
kufanyiwa uhalifu na wahamiaji haramu.
Mkuu wa Wilaya ya
Karagwe Bi Dari Rwegasira amewaambia Maafisa
Tarafa na Watendaji wa Kata aliokutana nao katika Ukumbi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Karagwe, mwishoni mwa wiki iiliyopita kuwa kuanzia sasa kila
kiongozi, kuanzia ngazi ya Kiijiji/Mtaa, Kata, Tarafa na Wilaya, atawajibika kwa
jinsi anavyoshughulikia kumaliza tatizo la wahamiaji haramu katika eneo lake.
Wilaya ya Karagwe ni
moja ya wilaya zenye tatizo sugu la wahamiaji haramu ambao wanatuhumiwa
kuwanyanyasa wananchi katika baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo, kwa kuendesha
vitendo vya wizi wa mifugo, kuvamia maeneo ya kilimo, na pia kuchochea uhalifu
wa unyang’anyi wa kutumia silaha na kusababisha mauaji.
Wahamiaji hao haramu
wanashutumiwa kufanya baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Karagwe yasipitike kwa
urahisi, mojawapo ikiwa ni eneo la msitu wa Kimisi, ambapo eneo hili limekuwa
na matukio mengi ya ujambazi wa kutumia silaha na wananchi kuvamiwa na kuibiwa
mali zao na hata wengine wakipoteza maisha katika matukio hayo.
Maazimio kadhaa
yalitolewa katika kikao hicho kati ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe na Watendaji
Wakuu wa Wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa:
·
Viongozi kuanzia ngazi ya
Kijiji/Kitongoji, Kata hadi Tarafa kutia saini mkataba wa kushughulikia
wahamiaji haramu, majambazi wa kutumia silaha na wafadhili wao, mifugo haramu
inayoingia nchini kutoka nchi jirani pamoja na vitendo vyote vya uhalifu katika
maeneo wanayoyaongoza.
·
Kiongozi yoyote wa Kijiji,
Kata au Tarafa atakayeshindwa kushughulikia wahamiaji haramu walioko katika
eneo lake atawajibishwa.
·
Wahamiaji wote haramu ambao
bado wapo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo wasakwe na kurejeshwa kwao
mara moja.
·
Msako uanzishwe mara moja
kuwasaka wahamiaji haramu wote ambao wamejificha katika maeneo ya misitu na
ranchi za mifugo zilizoko katika wilaya hiyo kwa kuvishirikisha vyombo vyote
vya Utawala na vya Ulinzi na Usalama vilivyoko katika Wilaya hiyo.
·
Kila kijiji kiwe na takwimu
sahihi za wageni waliopo katika maeneo yao.
·
Wahamiaji haramu wote
wanaorejeshwa kwao wasipewe nafasi ya kurudi tena nchini na mwananchi yoyote
atakayebainika kuwapokea au kuwasaidia kurejea atolewe taarifa haraka ili hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yake.
·
Vibali vyote vya Ukazi
vilivyotolewa kwa wageni mbalimbali sasa vitakaguliwa upya ili kuhakiki uhalali
wake.
Imeandaliwa na:
Timu
ya Habari ya Operesheni Kimbunga
Septemba30,2013