Home » » Operesheni Kimbunga yanasa wahamiaji haramu 1,851

Operesheni Kimbunga yanasa wahamiaji haramu 1,851


HATIMAYE operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu nchini, iliyopewa jina la Kimbunga, imeanza juzi huku watu 1,851 wakikamatwa. Hatua hiyo, imetokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka watu wanaomiliki silaha na kuishi nchini kinyume cha sheria, kuondoka wenyewe kwa hiari yao kabla vyombo vya dola havijaanza kazi ya kuwasaka.

Operesheni hiyo inayovishirikisha vyombo vyote vya dola, imeanza katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu, Fabian Massawe, alisema hadi jana wahamiaji haramu 1,851 wamekamatwa wakati 11,601 wameondoka kwa hiari yao.

Alisema operesheni hiyo haitamuacha mhamiaji haramu ndani ya mikoa hiyo.

Alisema licha ya wahamiaji 11,601 kuondoka wenyewe, Serikali imelenga wahamiaji 52,053 ambao bado wapo katika mikoa hiyo.

Alisema tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa agizo la wahamiaji haramu kuondoka kwa hiari, bunduki 65 zikiwamo Sub Machine Gun (SMG) tatu, ShortGun 10 na magobole 52 zilisalimishwa.

Naye, Mkuu wa Operesheni Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, alisema vyombo vyote vya dola vinaendelea na kazi ya kuwasaka wahamiaji.

Aliwatahadharisha wananchi mkoani Kagera kujihadhari na kuuziwa mali yoyote kutoka kwa mtu yeyote anayehamishwa bila maandishi kwa ajili ya kuepuka kukamatwa na kuhusishwa kushirikiana na wahamiaji hao.

Alisema walikamata ng’ombe 1,765, sare na vifaa mbalimbali vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). 


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa