WAFUGAJI wawili wameuawa kinyama kwa kukatwa
mapanga na kuchomwa mikuki na wananchi, huku ng'ombe wapatao 12 nao wakiuawa
katika Kijiji cha Kasulo wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera.
Chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa ni uhasama wa
muda mrefu kati ya wananchi na wafugaji hao wanaodaiwa kuingiza mifugo kijijini
humo bila ridhaa ya serikali ya kijiji.
Tukio hilo lilitokea Septemba 19 mwaka huu, saa
11:00 jioni na kwamba ng'ombe waliouawa kwa kuchomwa mikuki na kukatwa mapanga,
nyama zake zilichukuliwa na wanawake kwa ajili ya kitoweo.
Akithibitisha tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Ngoma 'B' yalipotokea mauaji hayo, Simeon Nzakaya alilaani kitendo cha
wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuwataja waliouawa kuwa ni Ngabo
Godfrey (24) na mwingine ambaye bado hajatambulika jina lake.
Alisema kuwa miili ya marehemu hao
ilipatikana Septemba 20, na watu wanane wanashikiliwa na vyombo vya
usalama kwa mahojiano zaidi kuhusiana na mauaji hayo.
Hata hivyo, taarifa zinadai kwamba baadhi ya
mamlaka zinazolalamikiwa ni pamoja ni Idara ya Uhamiaji Wilaya, Mifugo na Halmashauri
ya Wilaya kupitia kitengo cha sheria kwa kushindwa kuchukua hatua mara baada ya
kuombwa kuingilia kati mambo ya uvamizi wa wafugaji.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasulo, Yusufu Katula
alithibitisha kuwepo kwa mauaji hayo pamoja na kulaani kitendo hicho.
"Mgogoro huo unafukuta kutokana na idara
husika kutochukua hatua mapema. Hii inachangia kutokea mauaji kama haya, na
hatua za haraka zisipochukuliwa yanaweza kutokea mapigano makali kati ya
wanakijiji na wafugaji wanaoingia kinyemela,"alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alionya
kuwa matukio kama hayo hayaruhusiwi kutokea katika jamii, na aliahidi ofisi
yake kuyafanyia kazi malalamiko yote yanayotolewa kwa baadhi ya mamlaka.
"Ni kweli baadhi ya mamlaka za serikali
zinalalamikiwa sana na wananchi. Na sasa nitakachokifanya ni kuchukua hatua za
haraka kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena," alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment