SERIKALI kupitia Idara ya Uvuvi mkoani Kagera,
imekamata na kuteketeza kwa moto zana haramu 9,809 zilizokuwa zikitumika kwenye
uvuvi ndani ya Ziwa Victoria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba,
Ofisa Mfawidhi wa Uvuvi na Doria Mkoani Kagera, Apolinary Kyojo alisema zana
hizo zilikamatwa kutokana na msako maalumu wa kushitukizwa ndani ya Ziwa
Victoria.
Alisema msako huo wenye lengo la kupambana na uvuvi
haramu ndani ya ziwa hilo ulifanyika kati ya Juni na Agosti mwaka huu.
"Serikali inaendelea kupambana na watu
wanaoshiriki uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria. Kati ya Juni na Agosti mwaka
huu, tulikamata zana haramu 9,809. kwenye msako wa kushtukiza,” alisema.
Alizitaja zana zilizokamatwa kuwa ni nyavu zenye
matundu madogo zipatazo 7,000, nyavu aina ya timba 2,700, makokoro yenye urefu
wa zaidi ya mita 110,000, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh 750,000.
Kwa mujibu wa Kyojo katika kutekeleza misako ya
namna hiyo, idara yake inakabiliwa na changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka
kwa baadhi ya viongozi wa vijiji, kata na hata wasimamizi wa rasiliamali za
Ziwa Victoria (BMU).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment