Home » » BAWACHA: WATUMISHI IBURUZENI SERIKALI MAHAKAMANI

BAWACHA: WATUMISHI IBURUZENI SERIKALI MAHAKAMANI

MWENYEKITI wa Taifa wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee
MWENYEKITI wa Taifa wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee, amewataka watumishi wa umma kuiburuza Serikali mahakamani endapo watakatwa mishahara yao kwa ajili ya ujenzi wa maabara bila wao kuridhia kwa maandishi kama sheria ya kazi inavyotaka.
Aidha, amesema kuwa kama Rais Jakaya Kikwete ana dhamira ya dhati ya kuzijenga maabara hizo, basi akate sehemu ya bajeti yake ya kusafiri nje ya nchi ambayo kwa mwaka huu ametengewa sh bilioni 50 azipeleke kwenye ujenzi huo.
Pia, ametaka Serikali kuacha kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni kubwa ambazo inakadiriwa kufikia kati sh trilioni 1.5 na 2 kwa mwaka, ili fedha hizo na kodi nyingine zinazokusanywa kwa wananchi zitumike kutekeleza mapango huo.
Mdee, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na umati mkubwa wa wananchi wa Bukoba kwenye uwanja wa mashujaa wa Mayunga, akiwa ameambatana na
Makamu wake, Hawa Mwaifunga, Katibu Grace Tendega na Naibu Katibu, Kunti Yusuph.

Alisema kuwa hawapingani na ujenzi wa maabara hizo ambazo zinasomesha watoto wengi wa wananchi maskini, ila wanachokataa ni utaratibu mbovu unaotumika kukusanya fedha kwa nguvu kwa kukamata mishahara ya watumishi wa umma.
Alisema kuwa taarifa ya msimamizi na mkaguzi mkuu wa serikali, (CAG), inaonyesha kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita, kumefanyika ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, ambako mishahara hewa ilikuwa trilioni 1.6, jambo alilohoji ni kwa nini serikali isizibe mianya hiyo ili fedha hizo zikatumika kujenga maabara hizo.
“Tusiwape mzigo walimu, tusiwape mzigo mapolisi, tusiwape mzigo manesi wala tusiwatese wananchi wetu kwa watendaji kuwakimbiza na fimbo wakiwadai michango ya ujenzi wa maabara, wakati fedha unazo wewe Rais (Kikwete), na serikali yako… zitoeni zitumike kufanya maendeleo ya nchi ….
“Mimi nilikuwa mtumishi wa Wizara ya Kazi na Ajira, sheria ya kazi namba 28 ya mwaka 2004 ya mahusiano makazini, inasema ni marufuku kwa mtu yeyote kumkata mtumishi wa umma mshahara wake mpaka pale mtumishi huyo atakaporidhia kwa maandishi… hivyo mapolisi, manesi, waalimu mkikatwa mishahara mnaweza kuishitaki serikali mahakamani,” alisema Mdee.
Tendega awataka wananchi kuwa majasiri
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa BAWACHA, Grace Tendega aliwataka wananchi hao kuwa majasiri kwa kuhakikisha wanafanya maamuzi sahihi ya kuwang’oa CCM madarakani kupitia sanduku la kura, zoezi wanalopaswa kulifanya kuanzia Desemba 14 mwaka huu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Alisema kuwa, njia rahisi ya kuwang’oa CCM ni kuanza kuwakataa kuanzia ngazi za chini ili iwe rahisi kuwatoa madarakani mwakani kwenye uchaguzi mkuu.
Tendega, aliwataka wagombea wa CHADEMA watakaosimama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi huo, wahakikishe ni wale wenye umri wa miaka zaidi ya 21 kama sheria inavyoeleza ili waepuke kuondolewa kwa kukosa sifa, hivyo kufanya mgombea wa CCM apite bila kupingwa.
Mwaifunga: Wanawake msikubali kuwa madaraja
Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Hawa Mwaifunga, aliwataka wanawake kukataa kutumika kama madaraja ya kuwaingiza madarakani viongozi wa CCM, ambao miaka yote wamekuwa wakiacha kuwatatulia matatizo yao.
Alisema kuwa, kila inapokaribia uchaguzi wanawake huonekana lulu kwa wawania uongozi wa CCM, ambao huwaendea na vijizawadi vidogo kama sukari, kanga na vilemba, ambavyo huwarubuni navyo ili wafikie malengo yao ya kuukwaa uongozi na baada ya hapo hawawakumbuki tena.
“Ifike mahali wanawake muwaambie CCM imetosha, wametufanya daraja kwa muda mrefu sana kuvuka, lakini hatuoni mafanikio wala mabadiliko yoyote, zaidi maisha yanazidi kuwa magumu huku kukiwa hakuna huduma muhimu za jamii, mahospitalini tunazalia chini, hivyo imetosha na msiwape kura chaguzi zote zinazokuja,” alisema Mwaifunga.
Kunti: Ni ajabu taifa tajiri wananchi wake maskini
Naye Naibu Katibu Mkuu wa BAWACHA Taifa, Kunti Yusuph, alisema kuwa hakuna Mtanzania maskini ambaye hajui maumivu ya kuiweka CCM madarakani, kwani wakati nchi ni tajiri kwa kuwa na rasilimali nyingi, lakini wananchi wake wengi ni maskini wa kutupwa wasioweza hata kumudu milo mitatu kwa siku.
Alisema kuwa ni aibu kwa Taifa hili tajiri kwa kuwa na gesi asili, uraniam, dhahabu, tanzanite na mbuga nzuri za wanyama viongozi wake kugeuka ombaomba kwa kuzunguka nchi mbalimbali wakiomba misaada, jambo alilodai kuwa linasababishwa na kuweka madarakani viongozi wabinafsi na wezi.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa