Home » » MKURUGENZI MULEBA AJIKAANGA

MKURUGENZI MULEBA AJIKAANGA

KITENDO cha Mkurugunzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Joseph Mkude cha kuwafukuza waandishi wa habari na wananchi katika vikao vya Baraza la Madiwani, kimelaaniwa na Mkuu wa wilaya hiyo na madiwani.
Mkurugenzi huyo anadaiwa kukiuka kanuni ya kudumu namba 12 kifungu (1) na cha (2) inayowaruhusu wananchi kuhudhuria vikao hivyo vya wazi.
Mdiwani hao ambao walitishia kususia na kuhairishwa kwa kikao cha baraza cha Oktoba 31 mwaka huu, walimtaka mkurugenzi huyo, kurejea matangazo yake aliyoyabandika katika mbao za matangazo za halmashauri hiyo.
Tangazo hilo lilisomeka hivi; “Tangazo la mkutano wa Baraza la Madiwani. Napenda kuwatangazia wananchi wote  wa Wilaya ya Muleba kuwa mkutano wa Baraza la Madiwani utafanyika tarehe 30/10/ hadi 31/10/2014, kuanzia asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri”.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lenye kumb. namba KGR/HW/ML/.A.33/Vol.X/19, wananchi walikaribishwa kusikiliza kinachojadiliwa katika baraza hilo.
Hata hivyo, pamoja na tangazo lake hilo, Mkude aliingia ukumbini Okoba 30 mwaka huu, na kuwakuta wananchi pamoja na waandishi wa habari waliokuwa wamehudhuria kikao hicho, watoke nje, jambo lilipingwa vikali na madiwani.
Amri hiyo ya mkurugenzi, iliwafikisha waandishi kwa mkuu wa wilaya hiyo, Lembris Kipuyo na kumweleza yaliyojiri ambapo aliwataka kuwa wavumilivu wakati akiendelea kulishughulikia.
“Hata mimi sijapendezwa na kitendo hicho, kikao cha Baraza dogo ndio chenye habari nyingi na nzuri zinazohusu wananchi, unajua mimi huwa nawaambia viongozi wenzangu na watendaji wetu kuwa Muleba hii ina watu zaidi ya laki tano, sasa leo tukitaka wananchi wajue serikali yao imefanya mambo fulani lazima tutumie vyombo vya habari.
“Hata Rais Kikwete wakati tuko Dodoma katika semina elekezi mwaka 2006, alitueleza kuwa tukitaka mafanikio lazima tufanye kazi kwa karibu na vyombo vya habari, leo mkurugenzi amejisahau, nitamuita nimweleze,”alisema Kipuyo.
Alisema kuwa Muleba ikiharibikiwa pia naye ataharibikiwa kwa sababu kikao hicho kiko wazi, hivyo hakuna haja ya kuwafukuza waandishi kwani niwajibu wao kuchukua habari.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa