Home » » WAINGIZAJI SUKARI YA MAGENDO KUSAKWA

WAINGIZAJI SUKARI YA MAGENDO KUSAKWA

SERIKALI imetangaza msako mkali kuwanasa waingizaji na wauzaji wa sukari ya magendo iliyoingizwa nchini na kuzagaa kwenye masoko.
Waingizaji sukari ya magendo kusakwa
Pia, maofisa wote wa Mamlaka ya Mapato na ushuru mwingine kwenye bandari kuu ya Dar es Salaam na watahojiwa.
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, (Sera), Mwigulu Nchemba, aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya siku moja kwenye kiwanda cha kuzalisha sukari cha Kagera, (KSL), mwishoni mwa wiki, kutokana na taarifa ya kiwanda kwamba, sukari inayoingizwa nchini kimagendo na hailipiwi ushuru, imekuwa tishio kwa ustawi wa kiwanda hicho.
Akijibu kilio cha kiwanda hicho kilichoko wilayani Misenyi mkoani Kagera, Nchemba alisema; “Tutawasaka waingizaji, maofisa wetu wa TRA walioshughulika kupitisha sukari hiyo bandarini na wote wanaouza sukari hiyo.”
Nchemba, aliongeza kuwa msako huo utakuwa endelevu na wote watakaokamatwa watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Kiwanda hiki cha Kagera Sugar, ni mfano mzuri wa viwanda vilivyobinafsishwa na ambavyo vinafanya vizuri, kutokana na uwekezaji wake na uzalishaji, hatuwezi kukubali kiwanda hiki kife wakati kinachangia pakubwa katika jitihada za serikali kuwapatia watanzania zaidi ya 4,000 ajira na kodi,” alifafanua.
Awali, akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Meneja Mkuu, Ashwin Rana, alisema sukari inayoingizwa kwa njia zisizo halali imetapakaa sokoni hapa nchini na matokeo yake, bei ya sukari imeshuka kwa kiwango kikubwa na hivyo kukifanya kiwanda hicho kuuza kwa bei isiyoendana na gharama za uzalishaji.
Waziri Nchemba, ambaye alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji ya kiwanda hicho pamoja na huduma za kijamii kama vile hospitali inayohudumia wafanyakazi na wanakijiji wanaozunguka kiwanda hicho, aliupongeza uongozi wa kwa mafanikio hayo makubwa ya uzalishaji sukari kwa njia ya kisasa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KSL, Seif Ali Seif, alisema kiwanda chake hakiogopi ushindani ulio sawa, wanacholalamikia ni njama za kuua juhudi za kiwanda kuzalisha sukari ya kutosha na yenye kiwango cha juu kukidhi soko la humu nchini na je ya nchi.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa