Home » » WANAFUNZI SHULE YA RWEIKIZA WANG’AA

WANAFUNZI SHULE YA RWEIKIZA WANG’AA

WANAFUNZI  wote waliohitimu elimu ya msingi mwa huu katika shule ya msingi Rweikiza, iliyopo Kata ya Maruku, Wilaya ya Bukoba  mkoani Kagera, wamepata kiwango cha alama ‘A’.
Huu ni mwaka wa tatu kwa shule hiyo kushka nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 145 katika ngazi ya wilaya na ya pili katika mkoa wenye wanafunzi 909 huku ikiwa ya 13 katika ngazi ya taifa yenye wanafunzi 15,867.
Katika ufaulu huo, wanafunzi wote waliofanya mtihani na matokeo kutangazwa  na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) wiki iliyopita, wamepata alama ‘A’kwa wastani wa asilimia 88.56.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu juzi, Mkuu wa shule hiyo, Baraka Mwambinga, alisema siri ya mafanikio hayo ni ufundishaji, motisha pamoja na mazingira tulivu kwa walimu na wanafunzi.
Alisema pamoja na masomo ya kawaida, wanafunzi wa shule hiyo pia hupatiwa masomo ya ziada (tuition) huku wale wanaofanya vizuri katika mitihani ya majaribio ya kila wiki pamoja na ile ya mock hupewa motisha ya kutembelea maeneo mbalimbali nje ya mkoa huo wakiwa na walimu wao.
“Siri nyingine inayochangia sisi kufanya vizuri ni mazingira mazuri, tulivu na bora kwa walimu pamoja na wanafunzi kwa ujumla, tuna umeme, chakula kizuri, maji safi na salama, usafiri kwa walimu na wanafunzi wanaoishi nje ya shule, kimsingi vitu hivi vimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yetu”alisema.
Alitoa wito kwa serikali kugeukia shule zinazomilikiwa na watu binafsi kwa kuzipatia vitabu kama inavyofanya kwa shule zake kwa sababu matunda ya shule hizo ni manufaa ya taifa.
“Ninaiomba serikali itukumbuke kutupatia vitabu kama inavyofanya kwa shule zake kwa kuwa wote tunatoa elimu kwa watoto wa taifa hili,” alisema.
 Katika matokeo ya mwaka jana, shule hiyo ilikuwa ya kwanza kwa ngazi ya wilaya, ya tatu mkoa na 11 kitaifa.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa