Home »
» WAZIRI WA JK ATEMA CHECHE
WAZIRI WA JK ATEMA CHECHE
WAZIRI
katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ametaka viongozi wote
walionufaika na fedha za kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, washtakiwe,
wafungwe na kufilisiwa mali zao, kwani kuwafuta kazi au kujiuzulu
hakusaidii Watanzania.
“Kitendo cha kufukuzwa
kazi viongozi walionufaika na fedha za akaunti ya Escrow hakutoshi...
kuwafanya hivyo, ni sawa na kuwafanyia watu send off na kuwapeleka
fungate kwa pesa ya wananchi.”
Kauli hiyo ilitolewa na
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati alipofanya ziara katika
Hospitali ya Mwananyamala ili kuwajulia hali wajawazito na watoto ikiwa
ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Alisema endapo
watafilisiwa na kufungwa jela itakuwa ni kujenga Taifa lenye kuogopa
fedha za umma zinazohitajika kutumika sehemu nyingi kwa ajili ya manufaa
ya nchi yetu.
“Watu wanaokula pesa za
wananchi ni lazima wafukuzwe, kufungwa na hata kufilisiwa pesa hizo ni
kodi ya wananchi ambayo ingetumika sehemu nyingine kama
hospitali...kitendo cha wajawazito kulala watu wawili ni aibu kwa nchi
yetu, hivyo inatakiwa ukusanywaji wa kodi ufanywe kwa kina ili kuondoa
changamoto zilizopo hospitalini,”alisema Nchemba.
Aliongeza kuwa tayari watumishi saba wamesimamishwa kazi ni wale ambao walioiachia kodi katika sakata la escrow. “
Hivyo wanatakiwa
kuhojiwa na katika mahojiano hayo wakisema kuwa walikuwa hawajui kama
pesa hizo zilikuwa zinatakiwa kukatiwa kodi itajulikana kuwa walikuwa si
watumishi wa TRA au BoT na wakisema kuwa walikuwa wanajua ni lazima
hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Nchemba aliwashangaa
viongozi wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuacha kufanya majukumu
waliyonayo na kuanza kusimulia habari za uchukuaji wa fomu za urais.
“Hii inachekesha mno
badala ya sisi viongozi kufanya majukumu yetu tuliyoagizwa tunawaza
namna ya kuchukua fomu ya urais wakati muda bado haujafika, wana- CCM
wenzangu muda ukifika kila mtu atawajibika kuchukua fomu,”alisema
Nchemba.
Naye, Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Sophinias Ngonyani, alisema anashukuru
kwa msaada alioutoa Waziri katika hospitali hiyo kwa kuwa utawaletea
tija.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment