MWIJAGE: WAWEKEZAJI WASIKATISHWE TAMAA

Imeandikwa na Regina Mpogolo
Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema Tanzania ni changa katika sekta ya viwanda hivyo faini za mara kwa mara kwa wawekezaji wa sekta hiyo wakidaiwa kuharibu mazingira zitawakatisha tamaa.
Baraza la Taifa la Uhifadhi Mazingira (NEMC) imekuwa ikifanya ziara mara kwa mara kukagua viwanda hasa vile ambavyo vinalalamikiwa kufanya uchafuzi wa mazingira na kuvifungia kwa muda ili vifanye marekebisho, kutoza faini au vyote viwili.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini jana, siku ambayo huadhimishwa Siku ya Viwanda Afrika, Mwijage alisisitiza kuwa faini za mara kwa mara kwa wawekezaji haiwajengi, bali kuwakatisha tamaa.
Mwijage alisema ni kazi ya wizara yake pamoja na taasisi nyingine kuhakikisha wawekezaji wanaelimishwa badala ya kutozwa faini kwani nchi bado ni changa katika sekta ya viwanda na pia faini hazifundishi.
“Hawa watu walikuwa na shughuli zao, lakini tumefanya kazi kubwa kuwashawishi kuingia katika sekta ya viwanda, leo hii unataka wajue elimu yote kwenye viwanda walisomea wapi?” alihoji Mwijage.
Alisema wizara yake mwaka huu inaanzisha Kitengo cha Mazingira kwa lengo la ulezi na pia kuwafundisha wenye viwanda utunzaji wa mazingira katika viwanda. Akizungumzia viwanda, Mwijage alisema nia ni kuwa na viwanda vingi vyenye ushindani na kila mwananchi ashiriki katika uchumi huo na kujenga viwanda ambavyo vinatumia malighafi za ndani.
“Asilimia 70 mpaka 80 ya Watanzania wanajihusisha katika kilimo sasa tujenge viwanda ambavyo vinapokea haya mazao, pili tuzalishe ajira za kutosha kwa vijana na kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa sana na watu,” alisema na kuongeza kuwa nia ya serikali pia ni kuhakikisha viwanda vyote vinafufuliwa ambapo alifafanua kuwa kuna viwanda 156 hapa nchini, vinavyofanya vizuri ni 62 na 56 vilikua na matatizo.
Mwijage alisema kati ya hivyo, viwanda 56 vyenye matatizo sasa vimepata wawekezaji na vingine wenyewe wanavifufua
CHANZO HABARI LEO

TRA KUPAMBANA NA WAFANYABIASHARA ZA MAGENDO


 Kamishna wa Mamlaka ya mapato nchini(TRA)Charles Kichere(wa pili kutoka kushoto)akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi za mamlaka hiyo Mkoa wa Kagera(hawapo pichani)juu ya ziara yake ya kikazi katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera
Mkurugenzi wa huduma ya elimu kwa mlipa kodi Richard Kayombo(wa kwanza kushoto)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)

Na Editha karlo wa blog ya jamii,Kagera

MAMLAKA ya mapato(TRA)itaendelea kudhibiti na kupambana na wafanyabiashara wasio waaminifu wanaofanya biashara za magendo katika vituo mbalimbali na maeneo ya mipakani.

Kamishina mkuu wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) ,Charles Kichere ameyasema hayo kwenye ofisi za mamlaka hiyo Mkoani Kagera wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Wilaya zote za Mkoani humo.

Alisema TRA itazidi kupambana na kuwabana wafanyabiashara wote wanaopitisha mizigo yao kwa njia ambazo siyo za halali na kufanya serekali ikose mapato.Aliwataka wafanyabiashara wanaotumia mpaka wa mtukula kupitisha mizigo yao kuingia nchini Tanzania na kwenda nchi ya jirani ya Uganda kupitisha mizigo yao kwani huduma sasa hivi kituoni hapo zinapatika kwa haraka.

"Sasa hivi tutaziba mianya yote inayosababisha upotevu wa mapato hususani katika mipaka yetu,nina waomba wafanyabiashara wote watumie njia zilizo halali kupitisha mizigo yao watakapo kamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutaifishwa mizigo yao na kufikishwa katika vyombo vya dola"alisema.Alisema mamlaka haitavumilia vitendo vyovyote vya rushwa bali wataendelea kuwashughulikia mafisadi bila ya uogo wowote.Alisema tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera miaka ya hivi karibuni liliathiri ukusanyaji wa kodi za majengo kwani nyumba nyingi ziliathiriwa na tetemeko.

"Nimeona wakazi wa Kagera ni walipa kodi wazuri,maeneo niliyotembelea nimeona wanatumia mashine za kieletroniki za kodi(EFD's)wanapouuza au kutoa huduma"alisema Kamishna.Alisema mamlaka haitawavumilia wafanyabiashara wanaoikosesha mapato serekali kwa kuuza au kutoa huduma bila ya risti za EFD's kwa makusudi.Mkurugenzi wa huduma ya elimu kwa mlipa kodi Richard Kayombo amewataka wananchi kuwa mabalozi wa ukusanyaji wa mapato kwa kutimiza wajibu wao wa kudai risti wanaponunua bidhaa au kupatiwa huduma mbalimbali.

TATU MZUKA YAMPONGEZA BI. BUJINGINYA KUTOKA NGARA KWA KUSHINDA MILIONI 50.

Pichani kulia ni Judith Bujinginya mkazi wa wilaya ya Ngara Mkoani Kagera akizungumza jana jijini Dar mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),namna alivyoibuka mshindi wa jackpot ya Tatu Mzuka  ya shilingi milioni 50 katika droo ya 15 iliyofanyika mwishoni mwa wiki.Pichani kati ni
mwakilishi wa Tatu Mzuka, Kemi Mutahaba akiwa pamoja na
Joseph Kofia ambaye alishinda kimaajabu shilingi milioni 68 kupitia droo ya kila saa.
Pichani kati ni mwakilishi wa Tatu Mzuka, Kemi Mutahaba akiwatambulisha Washindi wa mchezo  huo,mbele ya Waandishi wa habari mapema jana jijini Dar.
Mwakilishi wa Tatu Mzuka, Kemi Mutahaba akimkabidhi mfano wa hundi Bi.
Judith Bujinginya mkazi wa wilaya ya Ngara Mkoani Kagera alieibuka  mshindi wa jackpot ya Tatu Mzuka  ya shilingi milioni 50 katika droo ya 15 iliyofanyika mwishoni mwa wiki

Mwakilishi wa Tatu Mzuka, Kemi Mutahaba akimkabidhi mfano wa hundi,
Joseph Kofia ambaye alishinda kimaajabu shilingi milioni 68 kupitia droo ya kila saa.

Judith Bujinginya mkazi wa wilaya ya Ngara Mkoani Kagera ameibuka mshindi wa jackpot ya Tatu Mzuka  ya shilingi milioni 50 katika droo ya 15 iliyofanyika jumapili.

Bi Bujinginya, mama wa watoto wawili ambaye anaungana na washindi milioni 130  wa Tatumzuka amesafirishwa kwa ndege kutoka Ngara kuja Dar es Salaam ili kuchukua pesa yake ya ushindi  katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Mikocheni.

 Baada ya kushinda mara chache katika droo ya kila saa, alipata msukumo wa kuendelea kucheza bila kukata tamaa. "Baada ya kuishi kwa kutafuta pesa ya mlo kila mwezi na miezi mingine bila pesa, Kiukweli sikujua itakavyokuwa ikifika Januari. Nimefurahi sana kwamba sasa naweza kutembea kwa kujiamini tena baada ya ushindi huu’ alikiri Bi Bujinginya.

Pia katika tukio la kukabidhi zawadi kwa mshindi alikuwepo Bwana Joseph Kofia ambaye alishinda kimaajabu shilingi milioni 68 kupitia droo ya kila saa.Dhamira ya Tatu Mzuka ya kubadilisha maisha ya watu haijabadilika ambapo zimebaki siku chache ili ichezeshwe droo kubwa ya Supa Mzuka jackpot ya milioni 150 jumapili ijayo. Tarehe 19 Novemba saa 3:30 usiku Mtanzania mmoja ataondoka na kitita cha milioni 150.

"Kila mtu ambaye umecheza tangu Tatumzuka izinduliwe na kutumia kuanzia shilingi 500 tu kupitia MPESA, TIGO PESA au AIRTEL MONEY, umeingia katika droo hii ambapo unaweza kujishindia milioni 150," alielezea mwakilishi wa Tatu Mzuka, Kemi Mutahaba.

Bi Mutahaba aliwahimiza watanzania kuendelea kucheza, akisisitiza kwamba bado washiriki hawajachelewa kujiwekea nafasi ya ushindi huo wa kihistoria.

PROFESA TIBAIJUKA ATANGAZA KUNG’ATUKA UBUNGE 2020


Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka, ametangaza kung’atuka nafasi ya ubunge kwa kutogombea tena kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Prof. Tibaijuka alitangaza msimamo huo jana mkoani Kagera, wakati wakizungumzia miaka miwili ya serikali ya Rais John Magufuli ambaye hivi sasa yuko mkoani humo kwa ziara za kikazi.

Jumatatu ya wiki iliyopita, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangaza kujiuzulu ubunge na pia kujivua uanachama wa CCM kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.

Baadaye Nyalandu alionekana akikaribishwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kisheria, kuhama chama humpotezea mbunge sifa ya kuendelea kuwa mwakilishi wa jimbo lake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huandaa uchaguzi mwingine mdogo kwa ajili ya kumpata mbunge mwingine kwenye jimbo husika.

Wakati akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kutogombea tena ubunge mwaka 2020, Tibaijuka aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, aliiambia Televisheni ya Taifa (TBC), kuwa ameamua kujing’atua ili kutoa nafasi kwa vijana.

“Sisi ni watu wazima… kizazi chetu tumeshamaliza kazi. Tumeshastaafu na mimi nikimaliza ubunge muhula huu nastaafu, nakwenda Muleba,” alisema Tibaijuka na kuongeza:

“Na kuaga nimeshaaga na wananchi wameniamini. Napenda tuwape nafasi vijana. Kuzeeka haimaanishi kwamba maarifa yangu yaondoke kwa sababu nimestaafu, tunawapa nafasi vijana washike nchi.

“Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tung’atuke… na mimi nang’atuka ili maarifa yetu yaweze kutumika kushauri, jamani tufanye hivi ili tuende mbele.”

Akizungumzia utendaji wa serikali ya Rais Magufuli katika kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, Tibaijuka alisema amefanya mengi mazuri na lazima Watanzania waendelee kumuamini.

“Hii nchi ilikuwa inasubiri kiongozi si Rais. Rais lazima awe pia kiongozi… sasa tujifunze kujua tofauti, mtu anaweza kukalia nafasi, lakini anaongoza? Anaonyesha njia? Ni jasiri? Kwa maana ujasiri unatokana na ukweli,” alisema.

Tibaijuka aliondolewa katika nafasi ya uwaziri kwenye serikali ya awamu ya nne ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete wakati baadhi ya wabunge walipomhusisha na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT).

JPM AIPONGEZA TANROADS KUOKOA BIL 4/- ZA MRADI

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Nishati, Medard Kalemani wakifungua pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Kyaka - Bugene kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 59.1 katika eneo la Kayanga wilayani Karagwe mkoa wa Kagera jana. (Picha na Ikulu).

RAIS John Magufuli amepongeza timu ya wataalamu wa Wakala wa Barabara (TANRODS) kwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 4 kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Kyaka-Bugene mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa 59.1.
Pongezi hizo amezitoa jana wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo iliyogharimu Sh bilioni 81.597, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania. Alisema hatua ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia timu ya wataalamu wa Tanroads kuusimamia mradi huo wao wenyewe kwa gharama ya Sh milioni 519.2 imeokoa zaidi ya Sh bilioni 4.5 ambazo angelipewa msimamizi kutoka nje.
“Napenda kuwapongeza sana Tanroads kwa kusimamia mradi huu ninyi wenyewe, zaidi ya shilingi bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu wetu kuusimamia mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha usimamizi wa miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000 wanaoweza kufanya kazi hizi, tuwatumie,” amesisitiza Rais Magufuli.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale amemweleza Rais Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene-Kasulo yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Barabara hiyo imejengwa na kampuni ya CHICO ya China. Kabla ya kufungua barabara hiyo, Rais Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth, walisafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika sherehe za ufunguzi.
Aidha, akiwa njiani kuelekea Karagwe, Rais Magufuli alisimamishwa na wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo.
Aidha aliwataka wawasaidie wananchi kuondoa migogoro ya ardhi, kusajili mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.
“Pale Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani kati yetu na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera mnachangamkia fursa hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao mengine ya kilimo, fugeni mifugo kisasa ili mnufaike,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo liliusimamisha msafara wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Rais Magufuli ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika mji huo na ametoa mwito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi walivyomuomba.
“Ndugu zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, mji huu hautakiwi uwe hivi ulivyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwashukuru kwa kazi kubwa wanayofanya waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha matangazo ya sherehe hizo na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia, ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka-Bugene zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla King, wabunge wa mkoa wa Kagera na viongozi wa dini na siasa. Leo Rais Magufuli ataendelea na ziara yake.
CHANZO HABARI LEO

RAIS DKT. MAGUFULI AKIFUNGUA UWANJA WA NDEGE WA BUKOBA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Andre Bald, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli wa pili kutoka (kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Serikali kuashiria ufunguzi rasmi wa Uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na viongozi hao mara baada ya ufunguzi wa rasmi wa Uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Andre Bald mara baada ya ufunguzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Andre Bald kuashiria ufunguzi wa wa rasmi wa Uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameshikana mikono na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Andre Bald, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli wanne kutoka kushoto waliokaa pamoja na viongozi wengine mara baada ya kukagua chumba cha abiria uwanjani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Mke wake Mama Janeth Magufuli watatu kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wabunge, viongozi wa Serikali pamoja na Viongozi wa Dini mara baada ya ufunguzi wa uwanja huo wa Ndege.
. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na kumshukuru Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Andre Bald mara baada ya shughuli za ufunguzi wa Uwanja wa ndege wa Bukoba.
Wananchi wakishangilia wakati wa Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kabla ya ufunguzi wa Uwanja wa ndege wa Bukoba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kabla ya ufunguzi huo wa uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera. PICHA NA IKULU

 

NEWS ALERT: RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA WAKURUGENZI WAWILI MKOANI KAGERA



RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AWASALIMIA WANANCHI WA MULEBA NA KEMONDO WAKATI AKIELEKEA BUKOBA MJINI MKOANI KAGERA



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Muleba wakati akiwa njiani kuelekea Bukoba mjini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasikiliza wananchi wa Muleba wakati walipokuwa wakiwasilisha kero zao mbalimbali.
 Baadhi ya wananchi wa Kemondo mkoani Kagera wakiwa juu ya miti kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihutubia wananchi wa eneo hilo.
 Wananchi wa Kemondo wakifurahia wakati  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akiwahutubia.
 Wananchi wa Muleba wakifurahia wakati  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akiwahutubia.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi wa Kemondo wakati akielekea Bukoba mjini. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwananchi Maarufu wa Muleba Hassan Milanga mara baada ya kuwasalimia wananchi wa Muleba.
 Baadhi ya mabango wa Wananchi wa Kemondo mkoani Kagera wakiyanyanyua wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akipita katika eneo hilo. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum  Kijuu mara baada ya kuwasili mkoani Kagera. PICHA NA IKULU


 

MWALIMU MKUU AMCHARAZA VIBOKO MWALIMU MWENZAKE


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Migango wilayani hapa amemchapa viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi akimtuhumu kwa wizi wa sahani tano pamoja na nusu kilo ya sukari iliyotolewa kwa ajili ya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba.

Katika taarifa yake ya kulaani kitendo hicho, kaimu katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Biharamulo, Joseph Lugumba alisema mwalimu mkuu, Mateso Musaku alimpiga viboko mwalimu wake Hosea Masatu mbele ya wanafunzi tukio ambalo linalaaniwa na wazazi, uongozi wa CWT na jamii ya Kata ya Runazi wanakoishi walimu wa shule hiyo.

Lugumba alisema baada ya kupata taarifa za mwalimu huyo kuchapwa viboko Ijumaa iliyopita, uongozi wa CWT ulifika Runazi kujiridhisha ambako wanafunzi na wazazi walithibitisha tukio hilo ikidaiwa kwamba mwalimu huyo alifungwa kamba kwenye mti.

Alisema mwalimu Masatu alidaiwa kuiba vitu hivyo siku moja baada ya kumalizika mahafali ya darasa la saba na kwamba alipoulizwa alikiri.


Alisema mbali ya kuonywa, alipelekwa na kufungwa kamba chini ya mti na kuchapwa mbele ya wanafunzi kitendo alichokiita cha udhalilishaji na kinyume cha haki za mtumishi na binadamu.

“Tunashauri mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kwa kutumia mamlaka zilizomteua mwalimu mkuu huyo kuongoza shule hiyo amuwajibishe kwenye ngazi za kinidhamu kwa maana amekiuka kanuni za uteuzi katika kuongoza walio chini yake,” alisema Lugunda.

Imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba Mosi baada ya mwalimu Masatu kukamatwa saa nane mchana na mkuu wa shule na kufungwa katika mti uliopo mbele ya shule hiyo na kuchapwa viboko saba huku wanafunzi wakishuhudia.

Mwalimu Musaku alithibitisha kumchapa mwenzake kwa madai kwamba alipata ridhaa kutoka kwa mwalimu aliyetuhumiwa kwa wizi na hakufikiria kama suala hilo lingeweza kuleta matokeo hasi katika jamii.

Alisema kwamba katika madaraka aliyopewa hakuna kipengele kinachomruhusu kutoa adhabu kama hiyo ya kipigo na kwamba ilitumika baada ya mwalimu huyo kukiri kosa na kutaka apewe adhabu ya viboko saba.

Hata hivyo, mwalimu Masatu alisema kitendo cha kupigwa na mkuu wake wa kazi kwa tuhuma za wizi wa mali ya shule ni udhalilishaji.

Alisema baada ya tukio la kupigwa alipelekwa kituo kidogo cha Polisi Runazi ambako alikaa rumande kwa siku tatu kwa madai ya kulewa saa za kazi na aliachiwa Novemba 3.

Hata hivyo, Polisi wilayani Biharamulo hawakutaka kuzungumzia suala hilo.

Kutokana na tukio hilo, Mwalimu Masatu alisema hana amani katika kata ya Runazi na Wilaya ya Biharamulo kutokana na taarifa za tukio hilo la kudhalilishwa kwake kusambaa.

Alisema hana imani kama ataingia darasani na kufundisha ipasavyo kwani ameathirika kisaikolojia. 

Aidha, alikana madai ya kuiba sukari na sahani tano na kwamba ametuma malalamiko kwa mratibu elimu kata na mwenyekiti wa kamati ya shule ili wachukue hatua dhidi ya mkuu wake kumdhalilisha kiutumishi na kijamii.

Walimu katika Shule ya Msingi Migango, Francisco Leonard na Faustine Mathias walioshuhudia tukio hilo walisema kitendo alichofanyiwa mwenzao ni udhalilishaji na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuanzia kamati ya shule hiyo mpaka ofisi ya mkuu wa wilaya zifuatilie na kujiridhisha juu ya ushahidi utakaotolewa ili kuhakikisha mwalimu aliyedhalilishwa anatendewa haki kwani kila anakopita ananyooshewa vidole na kukosa amani kuanzia kwenye familia yake.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Wende Ng’ahala alisema japokuwa hajapewa taarifa anajipanga kulishughulikia.

MPINA AHARAKISHA MNADA NG’OMBE WALIOTAIFISHWA

Imeandikwa na Mwandishi wetu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameiagiza Ofi si ya Mwanasheria Mkuu wa serikali wilayani Misenyi, kukamilisha taratibu za uhamiaji na mahakama, ili ng’ombe 6,648 waliokamatwa kwa kuingia nchini kinyemeleza waweze kupigwa mnada.
Ng’ombe hao walikamatwa hivi karibuni katika wilaya hiyo wakitokea Uganda na kukamatwa. Mpina alisema uvamizi wa kundi kubwa kama hilo la wanyama linaweza kusabisha madhara katika mazingira kama vile mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa vyanzo vya maji, kumaliza malisho ya mifugo iliyoko nchini, kusababisha migogoro ya mara kwa mara kwa wakulima na wafugaji na hata kuleta maambukizi ya magonjwa ya wanyama.
Mpina alisema suala hilo haliingiliani na ushirika wa Afrika Mashariki kwani ushirika huo upo kisheria, hivyo wavamizi wanaoingiza mifugo kinyemela nchini kutoka nchi jirani ni wahalifu kama wahalifu wengine. “Kwa hiyo naangiza ng’ombe hawa 6,648 waliokamatwa hatua ziendelee na ambao hawajakamatwa wakamatwe na wataifishwe na serikali.” alisisitiza. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Denis Mwila alisema utaratibu wa kutathmini ng’ombe katika wilaya yake bado unaendelea na taratibu za kisheria zinafuatwa.
CHANZO HABARI LEO

WAKULIMA WILAYA YA CHATO WAFURAHIA KUPATA MBEGU BORA KUTOKA COSTECH

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi (kushoto), kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), akimkabidhi mbegu ya viazi lishe kwa ajili ya shamba darasa la Kijiji cha Kibehe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari wakati wa uzinduzi wa shamba hilo wilayani Chato leo. 
 Wanakikundi cha Umoja cha Kijiji cha Kibehe kilichopo Kata ya Kigongo wakiandaa shamba lao la mbegu.
 Wanakikundi cha Umoja cha Kijiji cha Kibehe kilichopo Kata ya Kigongo wakiwa kwenye uzinduzi wa shamba darasa la viazi lishe na mihogo.
 Mtafiti wa Mazao ya Mizizi wa Wilaya ya Chato, Monica Mulongo akizungumzia vitamini A inayopatikana kwenye viazi lishe ambayo ni muhimu kwa watoto.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mbegu ya viazi lishe. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari.
 Mtafiti Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro akizungumzia ubora wa mbegu ya Wema pamoja na upandaji wake.


 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari , akionesha mbegu ya mahindi ya Wema baada ya kukabidhiwa.
 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akiwaonesha wakulima wa Kibehe jinsi ya kupanda mbegu ya mhogo.
 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho.
  Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula akitoa maelezo kwa wakulima wa vijiji vya Ipandikilo na Kitongoji cha Kaseni jinsi ya kupanda mbegu ya mhogo.
 Watafiti Bestina Daniel na Ismail kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga wakijadiliana jambo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi katika Kijiji cha Bukiliguru.
 Mshauri wa Jukwaa la ioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange akipanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa la Kijiji cha Itale.
 Wakulima wa Kijiji cha Bukiliguru wakishiriki kuapanda mbegu za mahindi katika shamba darasa.
 Mtafiti Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro akiwaelekeza wakulima jinsi ya kupanda mbegu bora ya mahindi ya Wema inayovumilia ukame.
Wakulima wa Kijiji cha Bukiliguru wakifuatilia uzinduzi wa shamba la mihogo.

Na Dotto Mwaibale, Chato

WAKULIMA Wilaya Chato mkoani Geita wamefurahia mbegu bora ya mihogo, mahindi na viazi lishe waliopewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuanzisha mashamba darasa ya mbegu hizo na kuzisambaza kwa wakulima wengine katika maeneo mengine.

Wakizungumza wilayani hapa leo kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu hizo katika vijiji vya Kibehe, Ipandikilo, Kitongoji cha Kaseni, Kijiji cha Itale na Bukiliguru kilichopo Kata ya Bwanga walisema mbegu hizo walizokabidhiwa na COSTECH kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwao.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Kachwamba,  Hamisi  Matesi alisema Costech kuwapelekea wakulima mbegu hizo itawasaidia sana kupata chakula wananchi wa kata hiyo ziada watauza.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho alisema wakulima walikuwa wakipata mavuno machache ya mahindi na mihogo kwa kuwa hawakuwa na mbegu bora hivyo baada ya kufunguliwa kwa shamba darasa la mbegu hizo katika maeneo yao wanategemea kupata mazao mengi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari aliwataka wananchi hao kutambua kuwa mpango huo wa serikali ya awamu ya tano unawategemea sana wakulima katika kilimo hivyo fursa hiyo walioipata ya kupelekewa mbegu hizo wasiipoteze.

“Hakikisheni  mbegu hizi bora za mihogo mnazopewa mnazitunza  ili kutoa nafasi kwa wananchi wengi zaidi kujifunza mbinu bora za kilimo hiki kupitia shamba darasa hili ili kila mkazi wa Chato aweze kulima na kuzalisha kwa tija” alisema Mhandisi Hari.

Hari ameishukuru COSTECH kwa kuamua kuipatia wilaya hiyo mashamba darasa katika vijiji hivyo kwani anaamini mbegu hizo zitasimamiwa vizuri na kisha kuwafikia wakulima wengi zaidi ili waweze kuachana na mbegu zao za zamani ambazo zinashambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi alisema kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa kama batobato katika mihogo.

Dk. Bakari aliwataka wakulima hao kuyatunza mashamba darasa hayo na kubwa baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa