RAIS John Magufuli amepongeza timu ya wataalamu wa Wakala wa Barabara
(TANRODS) kwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 4 kwenye mradi wa ujenzi wa
barabara ya lami ya Kyaka-Bugene mkoani Kagera yenye urefu wa kilometa
59.1.
Pongezi hizo amezitoa jana wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo
iliyogharimu Sh bilioni 81.597, fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali
ya Tanzania. Alisema hatua ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kutumia timu ya wataalamu wa Tanroads kuusimamia mradi huo wao wenyewe
kwa gharama ya Sh milioni 519.2 imeokoa zaidi ya Sh bilioni 4.5 ambazo
angelipewa msimamizi kutoka nje.
“Napenda kuwapongeza sana Tanroads kwa kusimamia mradi huu ninyi
wenyewe, zaidi ya shilingi bilioni 4 mlizookoa kwa kuwatumia wataalamu
wetu kuusimamia mradi huu ni fedha nyingi sana, nataka kitengo hiki cha
usimamizi wa miradi tukiimarishe, hivi sasa tunao wahandisi 15,000
wanaoweza kufanya kazi hizi, tuwatumie,” amesisitiza Rais Magufuli.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale amemweleza Rais
Magufuli kuwa barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene-Kasulo
yenye urefu wa kilometa 183.1 ambayo inaiunganisha Tanzania na nchi
jirani za Rwanda na Burundi.
Barabara hiyo imejengwa na kampuni ya CHICO ya China. Kabla ya
kufungua barabara hiyo, Rais Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth,
walisafiri kwa barabara hiyo kutoka Kyaka hadi Karagwe zilipofanyika
sherehe za ufunguzi.
Aidha, akiwa njiani kuelekea Karagwe, Rais Magufuli alisimamishwa na
wananchi wa Kyaka na kusikiliza kero zao ambapo amewaagiza viongozi wa
Mkoa wa Kagera kutowabughudhi wananchi wanaojihusisha na shughuli za
kilimo.
Aidha aliwataka wawasaidie wananchi kuondoa migogoro ya ardhi,
kusajili mifugo yao na kuinua uzalishaji wa mazao ili Mkoa wa Kagera uwe
na malighafi za kutosha kuanzisha viwanda.
“Pale Mtukula tumejenga kituo cha pamoja cha huduma mpakani kati yetu
na Uganda, lengo letu ni kurahisisha biashara kati ya Tanzania na
Uganda, kwa hiyo nataka kuona wananchi wa Kagera mnachangamkia fursa
hii, anzisheni viwanda kama vya nyama na mazao mengine ya kilimo, fugeni
mifugo kisasa ili mnufaike,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa Bukoba Mjini kundi kubwa la wananchi wa mji huo liliusimamisha
msafara wake ambapo baada ya kupokea kero mbalimbali, Rais Magufuli
ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kutatua tatizo la uhaba wa maji katika
mji huo na ametoa mwito kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba kuwasilisha
serikalini andiko la kuomba kujengewa kituo cha mabasi kama wananchi
walivyomuomba.
“Ndugu zangu mimi nipo pamoja na nyinyi, kero zenu nazijua na
tutazishughulikia, ninachowaomba punguzeni kubishana, mnapoteza muda
mwingi kubishana badala ya maendeleo, mnajichelewesha, mji huu hautakiwi
uwe hivi ulivyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwashukuru kwa kazi kubwa
wanayofanya waandishi wa habari waliokuwa wakirekodi na kurusha
matangazo ya sherehe hizo na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea
kushirikiana nao, na ipo tayari kuwasaidia, ikiwa ni pamoja na kuwezesha
mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
Sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kyaka-Bugene zimehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani, Wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiongozwa na Prof. Norman Sigalla
King, wabunge wa mkoa wa Kagera na viongozi wa dini na siasa. Leo Rais
Magufuli ataendelea na ziara yake.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment