Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Migango wilayani hapa amemchapa viboko mwalimu
mwenzake mbele ya wanafunzi akimtuhumu kwa wizi wa sahani tano pamoja na
nusu kilo ya sukari iliyotolewa kwa ajili ya mahafali ya wahitimu wa
darasa la saba.
Katika
taarifa yake ya kulaani kitendo hicho, kaimu katibu wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT) Wilaya ya Biharamulo, Joseph Lugumba alisema mwalimu
mkuu, Mateso Musaku alimpiga viboko mwalimu wake Hosea Masatu mbele ya
wanafunzi tukio ambalo linalaaniwa na wazazi, uongozi wa CWT na jamii ya
Kata ya Runazi wanakoishi walimu wa shule hiyo.
Lugumba
alisema baada ya kupata taarifa za mwalimu huyo kuchapwa viboko Ijumaa
iliyopita, uongozi wa CWT ulifika Runazi kujiridhisha ambako wanafunzi
na wazazi walithibitisha tukio hilo ikidaiwa kwamba mwalimu huyo
alifungwa kamba kwenye mti.
Alisema
mwalimu Masatu alidaiwa kuiba vitu hivyo siku moja baada ya kumalizika
mahafali ya darasa la saba na kwamba alipoulizwa alikiri.
Alisema
mbali ya kuonywa, alipelekwa na kufungwa kamba chini ya mti na kuchapwa
mbele ya wanafunzi kitendo alichokiita cha udhalilishaji na kinyume cha
haki za mtumishi na binadamu.
“Tunashauri
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kwa kutumia mamlaka zilizomteua
mwalimu mkuu huyo kuongoza shule hiyo amuwajibishe kwenye ngazi za
kinidhamu kwa maana amekiuka kanuni za uteuzi katika kuongoza walio
chini yake,” alisema Lugunda.
Imeelezwa
kuwa tukio hilo lilitokea Novemba Mosi baada ya mwalimu Masatu
kukamatwa saa nane mchana na mkuu wa shule na kufungwa katika mti uliopo
mbele ya shule hiyo na kuchapwa viboko saba huku wanafunzi
wakishuhudia.
Mwalimu
Musaku alithibitisha kumchapa mwenzake kwa madai kwamba alipata ridhaa
kutoka kwa mwalimu aliyetuhumiwa kwa wizi na hakufikiria kama suala hilo
lingeweza kuleta matokeo hasi katika jamii.
Alisema
kwamba katika madaraka aliyopewa hakuna kipengele kinachomruhusu kutoa
adhabu kama hiyo ya kipigo na kwamba ilitumika baada ya mwalimu huyo
kukiri kosa na kutaka apewe adhabu ya viboko saba.
Hata
hivyo, mwalimu Masatu alisema kitendo cha kupigwa na mkuu wake wa kazi
kwa tuhuma za wizi wa mali ya shule ni udhalilishaji.
Alisema
baada ya tukio la kupigwa alipelekwa kituo kidogo cha Polisi Runazi
ambako alikaa rumande kwa siku tatu kwa madai ya kulewa saa za kazi na
aliachiwa Novemba 3.
Hata hivyo, Polisi wilayani Biharamulo hawakutaka kuzungumzia suala hilo.
Kutokana
na tukio hilo, Mwalimu Masatu alisema hana amani katika kata ya Runazi
na Wilaya ya Biharamulo kutokana na taarifa za tukio hilo la
kudhalilishwa kwake kusambaa.
Alisema hana imani kama ataingia darasani na kufundisha ipasavyo kwani ameathirika kisaikolojia.
Aidha,
alikana madai ya kuiba sukari na sahani tano na kwamba ametuma
malalamiko kwa mratibu elimu kata na mwenyekiti wa kamati ya shule ili
wachukue hatua dhidi ya mkuu wake kumdhalilisha kiutumishi na kijamii.
Walimu
katika Shule ya Msingi Migango, Francisco Leonard na Faustine Mathias
walioshuhudia tukio hilo walisema kitendo alichofanyiwa mwenzao ni
udhalilishaji na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuanzia kamati ya shule
hiyo mpaka ofisi ya mkuu wa wilaya zifuatilie na kujiridhisha juu ya
ushahidi utakaotolewa ili kuhakikisha mwalimu aliyedhalilishwa
anatendewa haki kwani kila anakopita ananyooshewa vidole na kukosa amani
kuanzia kwenye familia yake.
Alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya
Biharamulo, Wende Ng’ahala alisema japokuwa hajapewa taarifa anajipanga
kulishughulikia.
0 comments:
Post a Comment