WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema
Tanzania ni changa katika sekta ya viwanda hivyo faini za mara kwa mara
kwa wawekezaji wa sekta hiyo wakidaiwa kuharibu mazingira zitawakatisha
tamaa.
Baraza la Taifa la Uhifadhi Mazingira (NEMC) imekuwa ikifanya ziara
mara kwa mara kukagua viwanda hasa vile ambavyo vinalalamikiwa kufanya
uchafuzi wa mazingira na kuvifungia kwa muda ili vifanye marekebisho,
kutoza faini au vyote viwili.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini jana, siku ambayo
huadhimishwa Siku ya Viwanda Afrika, Mwijage alisisitiza kuwa faini za
mara kwa mara kwa wawekezaji haiwajengi, bali kuwakatisha tamaa.
Mwijage alisema ni kazi ya wizara yake pamoja na taasisi nyingine
kuhakikisha wawekezaji wanaelimishwa badala ya kutozwa faini kwani nchi
bado ni changa katika sekta ya viwanda na pia faini hazifundishi.
“Hawa watu walikuwa na shughuli zao, lakini tumefanya kazi kubwa
kuwashawishi kuingia katika sekta ya viwanda, leo hii unataka wajue
elimu yote kwenye viwanda walisomea wapi?” alihoji Mwijage.
Alisema wizara yake mwaka huu inaanzisha Kitengo cha Mazingira kwa
lengo la ulezi na pia kuwafundisha wenye viwanda utunzaji wa mazingira
katika viwanda. Akizungumzia viwanda, Mwijage alisema nia ni kuwa na
viwanda vingi vyenye ushindani na kila mwananchi ashiriki katika uchumi
huo na kujenga viwanda ambavyo vinatumia malighafi za ndani.
“Asilimia 70 mpaka 80 ya Watanzania wanajihusisha katika kilimo sasa
tujenge viwanda ambavyo vinapokea haya mazao, pili tuzalishe ajira za
kutosha kwa vijana na kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa sana na watu,”
alisema na kuongeza kuwa nia ya serikali pia ni kuhakikisha viwanda
vyote vinafufuliwa ambapo alifafanua kuwa kuna viwanda 156 hapa nchini,
vinavyofanya vizuri ni 62 na 56 vilikua na matatizo.
Mwijage alisema kati ya hivyo, viwanda 56 vyenye matatizo sasa vimepata wawekezaji na vingine wenyewe wanavifufua
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment