na Ashura Jumapili, Kagera
WANANCHI wa Kijiji cha Nyakabango, Tarafa ya Kimwani, wilaya Muleba, mkoani Kagera wamechoma nyumba ya mtendaji na mwenyekiti wa kijiji hicho na kuharibu mali zenye thamani ya zaidi ya sh milioni baada ya viongozi hao kudaiwa ‘kuchakachua’ mahindi ya misaada yaliyotolewa kwa wananchi hao.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Philip Kalangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Juni 20 mwaka huu kati ya saa 2:00 hadi saa 6:00 usiku.
Alisema kabla ya mali hizo kuharibiwa kulikuwa na vurugu za wananchi dhidi ya viongozi wa Kijiji cha Nyakabango ambao ni Ofisa mtendaji wa Kata Nyakabango Ansbert Sabinian(52) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakabango Ladislaus Manana (41).
Alieleza chanzo cha ugomvi huo ni msaada wa mahindi tani 61.5 uliopelekwa kwa viongozi hao wa kijiji Mei 28 mwaka huu uliotoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba lengo likiwa ni kugawa kwa wananchi na zoezi hilo lilifanyika.
Alieleza kwamba Juni 19 viongozi waligawa mahindi hayo katika Kitongoji vya Rwenkara na kesho yake waligawa vitongoji vya Nyamagojo na Nyakabango kisha kuwatangazia wananchi kuwa mahindi yamekwisha.
Alieleza kwamba ilipofika majira ya saa 1:00 usiku kulikuwa na minong'ono kuwa mahindi yamechakachulia na viongozi na kuwa ugawaji wa mahindi hayo haukufuata taratibu ndipo walipofanya msako na kukuta mahindi lukuki yakiwa kwa viongozi hao.
Miongoni mwa sehemu walizokuta mahindi hayo ni nyumbani kwa Sabinian (Ofisa Mtendaji wa Kata) ambako walikuta gunia moja na nusu na kwa Tilusubia (magunia mawili), ambapo waliyatoa nje na kuchoma nyumba moto.
Walikuta pia magunia 12 ya mahindi nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Ladslaus Manana.
Kwa mujibu wa Kamanda Kalangi, uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na wanawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni mtendaji na mwenyekiti.
Chanzo: Tanzania Daima