WALIMU WAFUNDWA JUU YA MIKOPO


na Mbeki Mbeki, Karagwe
WALIMU wilayani Karagwe, Kagera wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchukua mikopo inayoendana na uwezo wao kiuchumi na mishahara yao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani hapa Velenan Vedasto, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazowakabili walimu.
Vedasto alisema walimu wanapaswa kuchukua mikopo inayoendana na uwezo wao wa mishahara, ili iweze kuleta tija katika familia zao.
Alisema utafiti uliofanywa na ofisi yake hivi karibuni ulibaini walimu 23 hawana mishahara kabisa na wengine 65 wanapokea mishahara chini ya sh 50,000 kwa mwezi.
“ Kwa kweli hii ni hatari kwa familia za walimu, mwisho wa mwezi hana mshahara…mwalimu wa aina hii hata akaingia darasani kufundisha hata mwanafunzi anamuelewa?” alihoji Vedasto.
Alisema baadhi ya walimu wamekuwa wanakopa mikopo mikubwa katika taasisi za fedha ambayo haiendani na vitega uchumi vyao, matokeo yake kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na wakati mwingine kuziathiri familia zao.
Chanzo: Tanzania Daima

MASHABIKI WAITEGA KAGERA SUGAR


na Ruhazi Ruhazi, Kagera
VIONGOZI wa klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, wanakuna vichwa katika kutekeleza masharti waliyopewa na mashabiki wa soka mkoa wa Kagera.
Akizungumza kutoka kwenye mashamba ya miwa ya Muleba, ambako ndiko makao makuu ya klabu hiyo, meneja na msemaji wa timu hiyo, Mohammed Hussein, alisema kuwa timu hiyo imeanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Alisema kuwa mashabiki hao wamewataka kuhakikisha wanawapa nafasi vijana ambao ni wazaliwa wa mkoa huo, iwapo wanataka waendelee kuwaunga mkono, tofauti na hivi sasa ambapo wamekuwa hawapati sapoti ya kutosha kutoka kwa mashabiki hao.
Meneja huyo, alisema kuwa uongozi umekubaliana kuyafanyia kazi mapendekezo ya mashabiki wao kwa kuwapa nafasi ya kwanza wachezaji wazaliwa wa mkoa huo.
“Ndugu yangu tumeanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi na pia tunajipanga kukiimarisha kikosi chetu cha vijana kwa kuwa imekuwa ndio kilio cha mashabiki wengi wa soka mkoani Kagera,” alisema Hussein.
Alisema kuwa, wachezaji wao wamesharipoti na kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu chini ya Kocha wao Abdallah Kibaden ‘King Mputa’ na ambaye atasaidiwa na mchezaji wao wa zmaani na kocha msaidizi wa muda mrefu katika kikosi hicho Mrage Kabange.
Chanzo: Tanzania Daima

DC AAMURU MWALIMU ACHUNGUZWE


na Ashura Jumapili, Bukoba
MKUU wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Ngara kufanya uchunguzi wa siku 14, ili kubaini tuhuma mbalimbali zinazomkabili Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabanga, Enock Ntakisigaye, ikiwemo kutumia majina hewa ya walimu kujipatia fedha pamoja na matumizi mabaya ya fedha na mali za shule.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mkuu huyo wa wilaya (DC), alisema ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa za kuwepo mgomo baridi wa kufanya kazi kutoka kwa walimu wa shule hiyo kutokana na tuhuma kadhaa ambazo walikuwa wamelalamika kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi.
Alisema kutokana na tuhuma hizo ameamua kumuagiza mkurugenzi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
Aliongeza katika kipindi hicho, mkuu wa shule, Enock Ntakisigaye, makamu wa shule, Daud Michael, na Mhasibu, Kalenzo Majanja, watakuwa nje ya ofisi kupisha uchunguzi.
Chanzo: Tanzania Daima
 DC AAMURU MWALIMU ACHUNGUZWE
na Ashura Jumapili, Bukoba
MKUU wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Ngara kufanya uchunguzi wa siku 14, ili kubaini tuhuma mbalimbali zinazomkabili Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabanga, Enock Ntakisigaye, ikiwemo kutumia majina hewa ya walimu kujipatia fedha pamoja na matumizi mabaya ya fedha na mali za shule.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mkuu huyo wa wilaya (DC), alisema ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa za kuwepo mgomo baridi wa kufanya kazi kutoka kwa walimu wa shule hiyo kutokana na tuhuma kadhaa ambazo walikuwa wamelalamika kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi.
Alisema kutokana na tuhuma hizo ameamua kumuagiza mkurugenzi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
Aliongeza katika kipindi hicho, mkuu wa shule, Enock Ntakisigaye, makamu wa shule, Daud Michael, na Mhasibu, Kalenzo Majanja, watakuwa nje ya ofisi kupisha uchunguzi.
Chanzo: Tanzania Daima

MKOA WA KAGERA WAJIANDAA NA SENSA KWA KUENDESHA MAFUNZO YA WAKUFUNZI




Na Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa, Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe afungua rasmi mafuzo ya wakufunzi wa sensa mkoani Kagera jana tarehe 17/07/2012 na kuwaasa wajumbe wa mafunzo hayo kuzingatia yote watakayofunzwa ili takwimu sahihi za sensa na makazi ziweze kupatikana kwa ajili ya maendweleo  ya mkoa wa Kagera.

Mratibu wa sensa mkoa wa Kagera akimkaribisha Mkuu wa Mkoa katika ufunguzin huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Linas Night Club, alisema dhumuni kubwa la mafunzo hayo  ni kuwafundisha wajumbe hao kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Kagera ili watakapoiva wawe wakufunzi  wa makarani wa sensa kuanzia ngazi ya Tarafa.

Mkuu wa Mkoa katika hotuba yake aliwasistiza sana wajumbe wote ambao walitoka katika kila wilaya kuzingatia sana mafunzo hayo kwa kuhakikisha kila kitu watakachofunzwa wanakizingatia kwa umakini mkubwa ili kuwa na uelewa mkubwa  wa kwenda kuwafundisha makarani  kule kwenye tarafa.

Pia Mkuu wa Mkoa aliwaonya wakufunzi hao kutojihusisha na vitendo vya kubuni au kukadilia takwimu pale watakapokuwa wanakusanya takwimu kwani ni muhimu sana kupata tawimu sahihi zitakazosaidia katika kupanga maendeleo ya taifa zima kwa miaka kumi ijayo. Vile vile alisistiza sana kuwa taarifa zote za sensa ni siri na hakutakuwa na mtu ambaye atatoa taarifa za kaya au za mtu binafsi zitakazoulizwa wakati wa sensa.

Wito; Mkuu wa Mkoa  pia alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kuhesabiwa siku ya kuamkia tarehe 26/07/2012 kwa kila sehemu ya mwananchi atayokuwa amelala. Pia alitoa wito kwa Taasisi za dini, na Taaasisi mbalimbali zote mkoani Kagera  kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kujitokeza na kuhesabiwa. Mhe. Massawe alitoa angalizo kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote atakaye jaribu kuvuruga zoezi la sensa, hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja.

Mafunzo hayo ya sensa Mkoani Kagera yanaendeshwa na wakufunzi kutoka ngazi ya Kitaifa, aidha mafunzo yanayotolewa ni juu ya kutambua maeneo ya sensa, namna ya kuuliza maswali, namna ya  kujaza madodoso pia mafunzo hayo yanafanyika kwa nadharia na vitendo na mwisho wa mafunzo hayo wakufunzi watafanya mtihani wa kujaribiwa kuona kama wameiva.

Fainali za Kumasaka Mrembo wa Kagera Kufanyika Jumamosi tarehe 14.07.2012



Shindano la kumsaka Miss Utalii mkoa wa Kagera 2012, litafanyika katika ukumbi wa Linas Club siku ya tarehe 14-7-2012 kuanzia saa, mbili usiku. Katika shindano hilo Warembo 15 watachuana kuwania taji la miss Utalii Tanzania 2012- Kagera, ambapo watapita jukwaani katika mavazi ya kitanzania ya Ubunifu,kitalii,kutokea na ya asili, huku wakitangaza Utalii, Utamaduni,urembo wa kitalii, ubunifu na vipaji vya kuimba na kucheza nyimbo na ngoma za asili za makabila ya mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla. Burudani mbalimbali za Ngoma za asili, bendi na wasanii wa muziki wa kizazi kipya watakuwepo, wakiwemo Diamond Musica Band, Agcox Burchaman toka Uganda,Maua na BK Sunday. Shindano hilo limedhaminiwa na Cargo Star, Vodacom Tanzania,Kroyera Tours,Vission Radio,Kasibante Radio, prins Hotel,Paradise Hotel,Linas Club ,Nice and Lovely Salon,misstourismorganisation.blogspot.com na Amazing Tanzania Tours(Tours and Safaris) .
Washindi wa shindano hilo watawakilisha mkoa wa Kagera katika fainali za miss Utalii Tanzania 2012- Kanda ya Magharibi, na baadae katika fainali za taifa za Miss Utalii Tanzania 2012 zitakazofanyika siku ya mkesha wa uhuru wa Tanzania 8-12-2012.
Miss Tourism Tanzania  Symbol Of National Heritage - Do Value Added Pageant
"Lets Visit & Promote Tanzania National Parks -Tourism is Life ,Culture is Lining"





Kizimbani kwa kula mishahara hewa


na Antidius Kalunde, Bukoba
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Kagera (TAKUKURU) imewafikisha mahakamani watumishi wawili wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera na watumishi sita wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kwa tuhuma ya kuchukua na kufuja fedha zinazopitishwa kwa njia ya mishahara hewa.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kagera Samson Bishati alisema watumishi hao wamejihusisha na suala la kupitisha fedha ambazo ni mishahara ya watumishi hewa na kujinufaisha wao wenyewe.
Aliwataja baadhi ya watumishi ambao wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bukoba kuwa ni wawili kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambao ni Shaban Kitimbisi na Sifa Musa ambao wote ni wa idara ya fedha.
Watumishi wengine ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni kutoka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Idara ya Afya ambao ni David Buhenyenge na Martin Muganyizi.
Alisema watumishi wanne waliobaki bado wanatafutwa na taasisi hiyo na hakuwa tayari kuwataja majina kwakuwa bado wanatafutwa ili kufikishwa mahakamani.
Watumishi ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani chini ya hakimu wa mahakama hiyo Willibard Mashauri wako nje kwa dhamana hadi kesi itakapotajwa tena ambayo inaendeshwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Fuja Siabo.
Katika hatua nyingine kaimu kamada huyo Bishati ametoa rai kwa umma kutojihusisha kwa namna yoyote katika vitendo vya rushwa kwani TAKUKURU ipo makini na ina uwezo wa kuibua na hatimaye kuwafikisha mahakamani watumishi wa umma ambao sio waadilifu
Chanzo: Tanzania Daima

Njaa yatishia Karagwe


na Mbeki Mbeki
VIJIJI 102 vya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera viko hatarini kukumbwa na njaa kufuatia ugonjwa wa mnyauko kuangamiza zao la ndizi.
Tahadhari hiyo imetolewa jana na mtaalamu wa kilimo wa Wilaya ya Bukoba, Mugenzi Byabachwezi, wakati akitoa mada ya uboreshaji wa hali ya chakula duniani, na kudai kuwa wilaya hiyo na ile mpya ya Kyerwa zitakumbwa na baa hilo.
Alisema kuwa zaidi ya migomba 30,000 tayari imeshambuliwa na migomba 26,000 imefyekwa katika harakati ya kudhibiti ugonjwa hao hatari.
Alisema kuwa ugonjwa huo umeenea kwa kasi zaidi katika vijiji vilivyo mpakani na nchi ya Uganda ambako ugonjwa huo ndiko ulikotokea, kutokana na wafanyabiashara wengi wanaotoka huko na kuingia wilayani humo kwa ajili ya kununua ndizi na mara nyingine mashina ya migomba.
Aliongeza kuwa mbali na kuenea kwa njia ya upepo, matumizi ya mapanga wanayotumia kukatia migomba, hivyo akataka kusitishwa kwa matumizi ya zana hizo kabla ya kuzipitisha kwenye moto.
Mtaalamu huyo alisema namna pekee ya kukabiliana na janga hilo ni kwa wananchi kulima mazao mengine ya chakula kuliko kutegemea misaada kutoka nje
Chanzo: Tanzania Daima


Wajasiriamali wakabidhiwa mkopo wa Sh14 milioni


Phinias Bashaya, Bukoba
MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Zipola Pangani, amekabidhi mkopo wa Sh14.5 milioni kwa vikundi vya wanawake, huku akiwataka kuwa wabunifu katika utafutaji masoko.

Akikabidhi mkopo huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Pangani alisema hakuna haja ya kuogopa kukopa, kwani hata matajiri hutumia fursa hiyo kama njia ya kujiongezea mitaji.

Pangani aliwataka wanawake na makundi mbalimbali kwenye wilaya hiyo, wasibweteke kusubiri msaada wa Serikali kwani wanaweza kujiwezesha kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali.

Hata hivyo, Pangani alisema mwanzoni vikundi vya wanawake havikuwa na matokeo ya kuridhisha baada ya kupewa mikopo kutokana na kutoandaliwa vizuri.

Pia, aliwataka wasing'ang'anie mradi wa aina moja na kuwa watafute masoko hata kwenye ushindani mkubwa, zikiwamo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambako Kagera inapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.

“Msiogope kuchukua mikopo, itumieni kuongeza mtaji wa biashara zenu, mnatakiwa kuwa wabunifu mvuke hata mipaka kuangalia mahitaji ya bidhaa zenu katika masoko mengine,” alisema Pangani.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Beatrice Dominick, alisema changamoto inayowakabili ni maombi mengi ya vikundi vinavyohitaji mikopo ikilinganishwa na uwezo mdogo wa halmashauri.

Dominick alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilitoa Sh8 milioni na zilizosalia zimeongezwa na halmashauri, zinatakiwa kurejeshwe ili baadaye wizara itoe mkopo maradufu.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo, Charles Kiberenge, alisema vikundi 12 vilivyopewa mikopo kwa viwango tofauti vinatoka kata  za Kemondo, Kaagya, Nyakato, Kanyangereko, Nyakato, Mikoni na Ibwera.

Alisema halmashauri inaendelea kujengea uwezo makundi mbalimbali na kwamba, kikundi cha Vijana cha Msifuni kinachojihusisha na ufugaji wa samaki kitapewa mkopo hivi karibuni.
Chanzo: Mwananchi

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa