Phinias Bashaya, Bukoba
MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Zipola Pangani, amekabidhi mkopo wa Sh14.5 milioni kwa vikundi vya wanawake, huku akiwataka kuwa wabunifu katika utafutaji masoko.
Akikabidhi mkopo huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Pangani alisema hakuna haja ya kuogopa kukopa, kwani hata matajiri hutumia fursa hiyo kama njia ya kujiongezea mitaji.
Pangani aliwataka wanawake na makundi mbalimbali kwenye wilaya hiyo, wasibweteke kusubiri msaada wa Serikali kwani wanaweza kujiwezesha kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali.
Hata hivyo, Pangani alisema mwanzoni vikundi vya wanawake havikuwa na matokeo ya kuridhisha baada ya kupewa mikopo kutokana na kutoandaliwa vizuri.
Pia, aliwataka wasing'ang'anie mradi wa aina moja na kuwa watafute masoko hata kwenye ushindani mkubwa, zikiwamo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambako Kagera inapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.
“Msiogope kuchukua mikopo, itumieni kuongeza mtaji wa biashara zenu, mnatakiwa kuwa wabunifu mvuke hata mipaka kuangalia mahitaji ya bidhaa zenu katika masoko mengine,” alisema Pangani.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Beatrice Dominick, alisema changamoto inayowakabili ni maombi mengi ya vikundi vinavyohitaji mikopo ikilinganishwa na uwezo mdogo wa halmashauri.
Dominick alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilitoa Sh8 milioni na zilizosalia zimeongezwa na halmashauri, zinatakiwa kurejeshwe ili baadaye wizara itoe mkopo maradufu.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo, Charles Kiberenge, alisema vikundi 12 vilivyopewa mikopo kwa viwango tofauti vinatoka kata za Kemondo, Kaagya, Nyakato, Kanyangereko, Nyakato, Mikoni na Ibwera.
Alisema halmashauri inaendelea kujengea uwezo makundi mbalimbali na kwamba, kikundi cha Vijana cha Msifuni kinachojihusisha na ufugaji wa samaki kitapewa mkopo hivi karibuni.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment