na Antidius Kalunde, Bukoba
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Kagera (TAKUKURU) imewafikisha mahakamani watumishi wawili wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera na watumishi sita wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kwa tuhuma ya kuchukua na kufuja fedha zinazopitishwa kwa njia ya mishahara hewa.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kagera Samson Bishati alisema watumishi hao wamejihusisha na suala la kupitisha fedha ambazo ni mishahara ya watumishi hewa na kujinufaisha wao wenyewe.
Aliwataja baadhi ya watumishi ambao wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bukoba kuwa ni wawili kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambao ni Shaban Kitimbisi na Sifa Musa ambao wote ni wa idara ya fedha.
Watumishi wengine ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni kutoka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Idara ya Afya ambao ni David Buhenyenge na Martin Muganyizi.
Alisema watumishi wanne waliobaki bado wanatafutwa na taasisi hiyo na hakuwa tayari kuwataja majina kwakuwa bado wanatafutwa ili kufikishwa mahakamani.
Watumishi ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani chini ya hakimu wa mahakama hiyo Willibard Mashauri wako nje kwa dhamana hadi kesi itakapotajwa tena ambayo inaendeshwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Fuja Siabo.
Katika hatua nyingine kaimu kamada huyo Bishati ametoa rai kwa umma kutojihusisha kwa namna yoyote katika vitendo vya rushwa kwani TAKUKURU ipo makini na ina uwezo wa kuibua na hatimaye kuwafikisha mahakamani watumishi wa umma ambao sio waadilifu
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment