Home » » MASHABIKI WAITEGA KAGERA SUGAR

MASHABIKI WAITEGA KAGERA SUGAR


na Ruhazi Ruhazi, Kagera
VIONGOZI wa klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, wanakuna vichwa katika kutekeleza masharti waliyopewa na mashabiki wa soka mkoa wa Kagera.
Akizungumza kutoka kwenye mashamba ya miwa ya Muleba, ambako ndiko makao makuu ya klabu hiyo, meneja na msemaji wa timu hiyo, Mohammed Hussein, alisema kuwa timu hiyo imeanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Alisema kuwa mashabiki hao wamewataka kuhakikisha wanawapa nafasi vijana ambao ni wazaliwa wa mkoa huo, iwapo wanataka waendelee kuwaunga mkono, tofauti na hivi sasa ambapo wamekuwa hawapati sapoti ya kutosha kutoka kwa mashabiki hao.
Meneja huyo, alisema kuwa uongozi umekubaliana kuyafanyia kazi mapendekezo ya mashabiki wao kwa kuwapa nafasi ya kwanza wachezaji wazaliwa wa mkoa huo.
“Ndugu yangu tumeanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi na pia tunajipanga kukiimarisha kikosi chetu cha vijana kwa kuwa imekuwa ndio kilio cha mashabiki wengi wa soka mkoani Kagera,” alisema Hussein.
Alisema kuwa, wachezaji wao wamesharipoti na kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu chini ya Kocha wao Abdallah Kibaden ‘King Mputa’ na ambaye atasaidiwa na mchezaji wao wa zmaani na kocha msaidizi wa muda mrefu katika kikosi hicho Mrage Kabange.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa