MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe
amewataka wahudumu wa afya kuacha tabia ya kuwabagua wagonjwa wenye
kadi za bima ya afya, hususani wazee wakati wanapofika vituoni kupata
huduma.
Massawe alitoa onyo hilo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Siku ya
Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliofanyika mjini
Bukoba juzi.
Alisema kuwa yapo malalamiko ya wagonjwa ambao ni wanachama wenye
kadi za NHIF kwamba wanabaguliwa wanapokwenda kupata matibabu kwenye
hospitali na vituo vya afya vilivyotengwa kwa ajili hiyo, wakitakiwa
kutoa fedha taslimu.
“Ubaguzi wa aina yoyote hasa pale mtu anapohitaji kupata huduma ya
msingi ambayo ni haki yake hautakiwi, sisi kama watoa huduma
tunaposhindwa kutoa huduma kwa wananchi kikamilifu ni kuwakatisha tamaa
wanaochangia huduma, mfano mfuko huu,” alisema.
Massawe alisema kuwa wazee hao wanachama wa mfuko huo wanakatwa kiasi
kikubwa cha fedha katika mishahara yao kwa ajili ya kugharimia
matibabu kwa hiyo wapate huduma bora kama walivyo watu wengine.
Aliliomba Bunge kuweka kifungu kwenye katiba mpya ili kila mwananchi
ajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu bora ya
gharama nafuu.
Chanzo:Tanzania Daima