Mwalimu wa Shule ya Msingi Kaiho, Kijiji cha Rwigembe, mkoani
Kagera, Tumaini Samson (42) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua
mwalimu mwenzake, Samson Mwenda (26) kutokana na kumchoma kwa kisu
kifuani na mgongoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe alisema jana kwamba mtuhumiwa anashikiliwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwigembe, Fidel Kamugisha
alisema marehemu ambaye ni mwenyeji wa Singida aliuawa baada ya kutokea
mzozo na mwenzake walipofika nyumbani wakitokea kwenye moja ya baa
kijiji hapo.
“Walimu hawa walikuwa marafiki jinsi walivyoishi na hakuna aliyedhani kama wangezozana,” alisema Kamugisha.
Alisema baada ya kutokea tukio hilo, mwalimu
Samson alijisalimisha kwa majirani kutaka kuomba msaada ili kumfikisha
mwenzake Hospitali ya Ndolage lakini alifariki wakati juhudi za kuokoa
maisha yake zikiendelea.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kaiho, Costantine
Augustine alisema wakati wa uhai wake, Mwalimu Mwenda alikuwa akitimiza
wajibu wake na kwamba, hakuwa na ugomvi na mtu hivyo tukio hilo
limewashangaza.
Kuhusu uhusiano wa walimu hao, Augustine alisema
licha ya kuishi nyumba moja na kutembelea mazingira ya kijiji, walikuwa
wakizozana baada ya kulewa na hatimaye kusameheana.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment