BAADHI ya wananchi wa Kijiji cha Bihata, Kata ya Kyebitembe Wilaya
ya Muleba mkoani Kagera, wamedai kuporwa ardhi yao ipatayo hekari 3,700
na mwekezaji, Diolex Joseph.
Pia wananchi hao wanalalamikia vitendo vya mwekezaji huyo kuwapiga na kuwajeruhi wazee wa kijiji hicho.
Wakizungumza na gazeti hili jana, walidai kuwa wamekuwa wakiuza ardhi kwa kulazimishwa na mwekezaji huyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Samweli Kakura, alisema kuwa
wamekuwa wakipigwa viboko pamoja na kutishiwa maisha kwa madai kwamba
hawana sehemu ya kushitaki kwa sababu mwekezaji huyo anawahonga
viongozi.
Alisema kutoka na hali hiyo, mwekezaji huyo amekuwa akipora ardhi ya
kijiji pamoja na sehemu za wananchi kibabe pasipo kuguswa na uongozi.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mussa Abdallah, alisema tatizo hilo la
mwekezaji huyo kutumia ubabe kupora ardhi limekuwepo kwa kipindi kirefu
ambapo hununua hekari kama saba na baadaye hujiongezea nyingine pasipo
kumshirikisha kiongozi yeyote wa kijiji.
“Mwekezaji huyo alijimilikisha ardhi ya kijiji pamoja na baadhi ya
ardhi za wananchi na anaposhitakiwa katika uongozi wowote, amekuwa
akitoa rushwa na kesi kushindwa kusikilizwa.
“Anapita kila sehemu akijigamba na kusema kuwa hakuna mtu wa kumweza
kutokana kwamba ana fedha nyingi,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza:
“Baada ya kumiliki ardhi bila kufuata sheria, aliweka mabango ya
kuwazuia wananchi wasipite maeneo hayo. Kila anayepita hufanyiwa
vitendo vya kikatili ikiwemo kupigwa viboko.”
Mussa aliongeza kuwa pamoja na kujimilikisha ardhi hiyo, pia amevamia
hifadhi ya Burigi na kuharibu mazingira kwa kukata miti na kuchana
mbao na kukata mkaa kisha kutengeneza mitumbwi inayotumika katika uvuvi
haramu ndani ya Ziwa Burigi.
Alisema kuwa walishapeleka malalamiko hayo katika ofisi za kata,
lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake, badala yake
viongozi wanamsikiliza zaidi mtuhumiwa.
“Hata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Muleba alifikishiwa taarifa
hizo, alifika hapa kijijini na kumwagiza mwanasheria wa ardhi
kufuatilia suala hili, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema.
Alipotafutwa Joseph, alikana kupora ardhi hiyo akidai kuwa alinunua
kwa wananchi kwa kutumia uwezo wake wa kifedha, na kwamba anakiri
kuharibu mazingira ya Burigi, lakini yuko na watu wengine.
Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka ambaye pia ni Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema kuwa wananchi ndio wenye
ridhaa ya kutoa ardhi katika kijiji bila kuzidisha hekari 50 ili mradi
zifuatwe taratibu za kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment