UMOJA wa wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania kutoka mkoani Kagera
(Kausta), umewaomba wadau wa sekta mbalimbali kujitokeza kuwaunga mkono
ili waweze kwenda kujitolea katika shule za kata.
Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kausta Mkoa wa
Kagera, David Willbard, wakati alipokuwa akisoma taarifa katika kikao
kilichowahusisha viongozi wa kada mbalimbali kwenye Ukumbi wa Mkuu wa
Mkoa mjini Bukoba.
Willbard alisema kuwa wameamua kuwaita viongozi hao ili waweze
kujadili kwa pamoja ufundishaji na namna bora ya kuanzisha mfuko
shirikishi kusaidia wanafunzi wa umoja huo watakaokwenda kujitolea
katika shule hizo pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu juu ya suala la
taaluma katika Mkoa wa Kagera ambao unaonekana kuwa na changamoto kubwa
kwa kizazi hiki.
Alisema vyuo vikuu husaidiana baina ya wanafunzi wenyewe katika
kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakiwa vyuoni na
kuangalia namna bora ya kuinua maendeleo ya Mkoa wa Kagera katika nyanja
mbalimbali za kitamaduni, kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.
Hata hivyo, alisema kuwa wameamua kwenda kujitolea katika shule za
kata, kutokana na kuziona zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya
kidato cha nne, hivyo kutokana na utafiti uliofanywa na Kausta mwaka
2012, waliona kiwango cha elimu katika mkoa huo ni tofauti na miaka ya70
na 80.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabiani
Massawe, alisema kuwa uongozi wa mkoa umepokea suala hilo na watawaunga
mkono ili kuona kama ufaulu katika shule za kata utaongezeka.
Pia, amewataka wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu kuachana na tabia ya
kukaa nyumbani wakisubiri matokeo, badala yake wajitolee katika shule
kama hizo ili kujijengea uelewa zaidi.
Chanzo;Tanzania Daima
1 comments:
Ndibalema Twinomukama. ilo ni wazo zuri na la kuunga mkono ili liwe endelevu. wadogo zetu wanashindwa kufanya vizuri kimasomo kutokana na upungufu wa walimu. kwa njia yoyote ile nawa support KAUSTA na kwa mchango zaidi 0715 983089 mwenyekiti au kiongozi yoyote katika chama nitafuteni kwa namba iyo.
Post a Comment