Home » » BOKSI 568 ZAVIPODOZI ZAKAMATWA

BOKSI 568 ZAVIPODOZI ZAKAMATWA

BOKSI 568 za vipodozi vya aina mbalimbali vikiwemo vilivyopigwa marufuku na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na dawa za binadamu, vimekamatwa mkoani Kagera wakati vikiingizwa nchini kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa vipondozi hivyo vilikamatwa katika mwalo wa Igabiro, Tarafa ya Bugabo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

Alisema vipodozi hivyo vilikuwa vinaingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Uganda kwa njia za magendo kupitia ziwa Victoria ambavyo hadi sasa thamani yake haijafahamika.

Kamanda Mwaibambe alisema, vipodozi hivyo vilikuwa vimepakiwa kwenye mtumbwi wenye namba za usajili TMZ 010078 ambavyo baadhi yake vilipigwa marufuku na Serikali kupitia TFDA.

Alivitaja baadhi ya vipodozi hivyo kuwa ni Esapharm, Lemon, Extra Clair, Top Lemon Cream and Lotion, Caro light pamoja na dawa za binadamu aina ya Cadiphen.

Alisema watu wanne wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kuhusika na uingizwaji vipodozi hivyo kinyume cha sheria ambapo uchunguzi wa awali umebaini vilikuwa vikisafirishwa kwenda Mwanza.

Kamanda Mwaibambe aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kasongo Otianga (34), Yusuph Juma (46), Sendi Wambura (32) na Eleven Sylivester (43), wote wakazi wa Jiji la Mwanza.

Aliongeza kuwa, polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na TFDA, wanaendelea kufanya upelelezi kabla watuhumiwa hao kuwajafikishwa mahakamani

Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa