Home »
» MTAMBO MPYA WA KUFUA UMEME WAFUNGWA KAGERA
MTAMBO MPYA WA KUFUA UMEME WAFUNGWA KAGERA
WANANCHI mkoani Kagera
wataondokana na tatizo la kukatika kwa umeme baada ya kufungwa mtambo
mpya wa kufua Umeme (Transfoma) katika eneo la Kibeta kwa ajili ya
kusambaza huduma ya umeme kwa wakazi wa mkoa huo.
Meneja wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco ) mkoani Kagera mhandisi Martine Madulu alisema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea eneo
ilipofungwa transfoma hiyo.
Mhandisi Madulu alisema
kuwa serikali imeamua kuleta transfoma hiyo mpya, iliyogharimu zaidi ya
sh.Bilioni 1.3 kutokana na kuongezeka kwa wateja na kusababisha
transfoma iliyokuwepo kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja.
“Transfoma hii ina
uwezo wa kuzalisha megawati 12 za umeme tofauti na iliyokuwa ikitumika,
ambayo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati nne… mahitaji ya wateja
wote ambao ni zaidi ya 22,000 katika manispaa hiyo yaliishafikia
megawati sita” alisema Meneja huyo.
Alisema kuwa transfoma
hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja zaidi ya 22,000 tofauti na
iliyokuwepo awali ambapo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia wateja 15,000.
Aidha Mhandisi Madulu
aliwataka wananchi mkoani Kagera kuendelea kushirikiana na Tanesco
katika kutoa taarifa kwa wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo ili
hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Wakati huo huo, alisema
kuwa wameanza awamu ya pili ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA), ambapo
hadi kufikia mwezi Juni mwakani vijiji 400 mkoani Kagera vinatarajiwa
kuwa vimenufaika kupitia mradi huo.
Kwa mujibu wa meneja
huyo ifikapo mwakani wateja wanaohudumiwa na shirika hilo watakuwa
wameongezeka kutoka idadi ya sasa hadi kufikia 36,000.
Kwa upande wake
mhandisi wa Tanesco kutoka makao makuu,anayesimamia ufungaji wa
transfoma hiyo, Amon Gamba alisema kuwa kufungwa kwa transfoma hiyo
kutawezesha kuongezeka kwa idadi ya wateja na hivyo kuondoa malalamiko
yaliyokuwepo ya umeme mdogo.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment