Home » » JUKATA YAWATETEA WALIOMEGUKA UKAWA

JUKATA YAWATETEA WALIOMEGUKA UKAWA

 VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kuacha kutoa kauli za kuwashughulikia wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaokiuka matakwa ama misimamo ya vyama vyao ili kusaidia mchakato wa katiba.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Deus Kibamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa wanachama wa Jukwaa la Katiba nchi nzima uliolenga kuwaelimisha juu ya namna ya kujadili rasimu ya katiba.

Kibamba alisema kuwa kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa siasa za kuwashughulikia wajumbe waliokiuka maazimio ya kundi moja juu ya mchakato wa katiba ndizo zinazaa mapigano miongoni mwao hivyo kuvuruga mchakato wa katiba.

"Kushughulikiwa kunazaa kupigana,watu wanapigwa sababu ya rasimu ya katiba na hata anayeonesha kutaka mchakato wa katiba usitishwe na yule anayesaliti msimamo wa UKAWA anaambiwa atashughulikiwa...sasa wanatakiwa kuacha kauli hizo na kushikana mikono ili kwa pamoja wajadili rasimu ya Katiba,' alisema Kibamba.

Aliongeza kuwa wananchi pamoja na wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wanapaswa kuvumiliana kwa hoja badala ya kujibizana kwa kuwa rasimu ya katiba ina mambo mengi ya kujadili ambayo hayahitaji majibizano.

"Sisi tunaongeza nguvu kwa Bunge Maalum kupitia mijadalatunayofanya na hawa wanachama wakirudi katika wilaya zao wataelimisha wengine namna ya kujadili rasimu pasipo kushikana mashati wala kushughulikiana," alisema Kibamba.

Kwa upande wake,Humphrey Polepole alisema kuwa ni vema Watanzania wakiwemo wanasiasa wakazuia tofauti za makundi na za vyama vya siasa ili kusaidia kusudio la Rais Kikwete la kupata Katiba Mpya.

"Tukisema tuzuie mchakato tutawapa nafasi watu wachache wasiotaka kupata Katiba Mpya,tushikamane pamoja kupigania mchakato huu kwani kila Mtanzania ana haki ya kushiriki kujadili katiba," alisema Polepole.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa