BAADHI
ya madiwani na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Bukoba
mkoani Kagera, wamelaani kitendo cha aliyekuwa Meya wa manispaa hiyo,
Anatory Amani cha kuweka pingamizi mahakamani ili kuzuia kikao cha
dharula cha madiwani.
Waakizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho juzi, baadhi ya
madiwani hao akiwemo mbunge wa Viti Maaalum, Conchestaer Rwamulaza
(CHADEMA), walisema inasikitisha kuona malumbano yaliyokuwepo wakati wa
nyuma yakijitokeza tena kupitia kwa mtu mwenye maslahi binafsi.
Rwamlaza ambaye pia ni Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera, alisema kuwa
hatua ya Amani kuweka pingamizi mahakamani ni kukwamisha maendeleo ya
wananchi bila sababu.
“Sikufurahishwa na maamuzi haya aliyochukua Amani kwenda mahakamani
kupinga vikao visiendelee. Tulikuwa na kesi baadhi ya madiwani
wameondolewa nyadhifa zao wakituhumiwa kukwamisha maendeleo ya Bukoba
lakini bado yeye kwa maslahi yake binafsi anaweka pingamizi
tena,”alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Bakoba, Felician Bigambo (CCM), alisema kuwa
japokuwa hawana mamlaka ya kuingilia uhuru wa mahakama lakini
wamesikitishwa na hatua hiyo ya ubinafsi wa Amani ambaye pia ni diwani
kata ya Kagondo.
“Tunaomba Serikali kuingilia kati hata kama mahakama haingiliwi,
jamani angalia mtu mmoja anaamua kukwamisha na kuzuia vikao
visiendelelee kwa maslahi yake.
Haingii akilini maana wenzetu walivuliwa nyadhifa wakidaiwa
kukwamisha maendeleo, sasa wananchi wapime nani anawakwamisha,”alisema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza alisema kuwa Amani
hapendi maendeleo ya Bukoba kwa sababu kila kinachofanyika yeye anaweka
pingamizi mahakamani.
Wakili wa Amani, Alon Kabunga alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu
kikao kilichoitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na Naibu
meya, Alexander Ngalinda juzi hakikuwa halali kwani sheria, Amani bado
inatambulika kuwa Meya Bukoba.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment