Home »
» SERIKALI HAINA FEDHA ZA KULIPA FIDIA-MUHONGO
SERIKALI HAINA FEDHA ZA KULIPA FIDIA-MUHONGO
WAZIRI wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali haina fedha za kulipa
fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo Mradi wa Umeme Vijijini (REA)
unatekelezwa mkoani Kagera.
Profesa Muhongo, alitoa
kauli hiyo wiki iliyopita, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa
usambazaji umeme katika kijiji cha Katoke, wilayani Biharamulo, Kagera.
Alisema Serikali haina
fedha za kuwalipa wananchi fidia katika maeneo ya mradi wa REA ingawa ni
haki yao, kwa sababu hiyo italazimika kuhamisha mradi na kuupeleka
ambako wananchi hawahitaji fidia bali nishati ya umeme.
Alisema kuwa, fidia ni
utapeli na hakuna mahali ambapo fidia imetolewa (imelipwa ) kwa wananchi
kesi zikaisha, hivyo wananchi waelezwe ukweli kuwa hakuna fedha za
fidia. "Fidia ni haki yao, lakini hatuna fedha za kuwalipa.Sasa wafanye
uamuzi, wanahitaji umeme au fidia.
"Kama ni fidia wasubiri
baada ya miaka 20.Na kwa sababu hiyo tutahamisha mradi tuupeleke maeneo
wasikohitaji kulipwa fidia," alisema Profesa Muhongo.
Alisema dhamira ya
serikali ni kufuta umaskini na kuleta ajira mpya kwa kuwaunganishia
wananchi umeme ambao utasaidia kukuza na kuboresha biashara zao, kilimo
cha kisasa, kuboresha huduma za afya na elimu.
Aidha alisema tatizo ni
wananchi kukataa kulipa fedha za kuunganishiwa umeme ambazo ni sh
27,000 tu,na kufafanua kuwa taasisi za umma (ofisi za watendaji, shule
na zahanati) na taasisi za kidini (makanisa na misikiti) zitaunganishiwa
bure nishati hiyo.
Profesa Muhongo,
aliwataka Wahandisi nchini kuanzisha kampuni zao wafanye kazi za miradi
mbalimbali ya ujenzi wa nishati ya umeme, badala ya kulalamika kuwa kazi
nyingi wanapewa wageni badala ya wazawa.
Aidha Mratibu wa mradi
huo mkoani Kagera, Mhandisi Julius Kateti wa kampuni ya Urban and Rural
Engineering Service Ltd, alisema mradi huo utagharimu sh. 98 bilioni na
utakamilika Januari mwakani.
Alisema zinahitajika
nguzo 55,000 ili kukamilisha mradi huo na kampuni hiyo imeagiza nguzo
nyingine kutoka nchini Uganda na Afrika Kusini
0 comments:
Post a Comment