Home » » WAGOMA KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO

WAGOMA KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO

 
Zaidi ya kaya 600 zenye watu takribani 4,000 kwenye kijiji cha Mpago, kata ya Kaniha, wilayani Biharamulo, wamegoma kuchangia miradi ya maendeleo kutokana na serikali kushindwa kutatua mgogoro wa ardhi kati ya kijiji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Nyantakara.
Uamuzi huo ulifikiwa na wananchi hao baada ya Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kuwataka kuondoka kwenye kijiji hicho kwa madai kwamba kimejengwa ndani ya hifadhi kinyume cha sheria za uhifadhi misitu na wanyama. 

Mbali na kuondolewa, pia wananchi hao wametakiwa kutoendeleza shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo hayo.

Akizungumzia mgogoro huo wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata yake kwenye kikao cha madiwani wa Biharamulo, Diwani wa kata hiyo (CCM), Mashauri Paschal, alisema licha ya mgogoro huo kufika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda. lakini bado haujatatuliwa na kuwafanya wananchi hao kuishi kama wakimbizi.

Alisema shughuli ya ujenzi wa sekondari kwenye kata yake umekuwa ukisuasua kutokana na wananchi wa kijiji cha Mpago kugoma kuchangia maendeleo.

Alisema mpaka sasa wananchi hao hawajui hatma ya maisha yao kutokana na mgogoro huo uliodumu takribani miaka mitatu wakizuiwa kuendelea na shughuli za kilimo na kwamba kuwaomba michango ni sawa na kuwakejeli.

Diwani wa kata ya Bisibo (Chadema), Josephat Kayamba, alisema hali ni tete kwenye kata yake kufuatia kaya 340 zenye watu takribani 2,040 kutakiwa kuondoka kwenye ardhi yao kwa kipindi kisichozidi siku saba kutokana na kudaiwa kuvamia eneo la Hifadhi ya Wanyama ya Burigi, wilayani humo.

Mbunge wa Jimbo la Biharamulo (Chadema), Antony Mbassa, amewataka wananchi kuepuka kununua ardhi yenye migogoro na kwamba wanapolipia ni vyema wakapewa stakabadhi za serikali ili kuepuka fedha zao kuliwa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Nassib Mmbagga, alisema serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na viongozi wa Hifadhi za Burigi, Nyantakara na Biharamulo, wakati wakiendelea kusubiri majibu ya Waziri Mkuu kuhusiana na migogoro hiyo.

Aidha aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuendelea na shughuli zao za kilimo lakini wajiepushe kuongeza maeneo ambayo awali walikuwa hawayatumii.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa