MSAKO WANASA BUNDUKI, VIROBA VYA KONYAGI

JESHI la Polisi mkoani Kagera limekamata bunduki moja ya kivita ikiwa imefukiwa ardhini pamoja na viroba bandia vya pombe aina ya konyagi katoni 20.
Hayo yalisemwa juzi na Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi.
Vitu hivyo vimekamatwa kufuatia msako mkali ulioanza kwa wiki moja kuanzia Agosti 18 mwaka huu katika maeneo ya nchi kavu na majini.
Kamanda Mwaibambe, alisema bunduki ya kivita iliyokamatwa ni aina ya Uzigan ambapo alibainisha kuwa ilipatikana baada ya raia wema kutoa taarifa. Alisema bunduki hiyo ilikutwa imefukiwa ardhini katika kisiwa cha Gozba wilayani Muleba.
Katika tukio la viroba bandia, Jeshi limemkamata Arbogastus Kamala (38) mfanyabiashara mkazi wa Kamizilente, Kata ya Hamgembe akiwa na katoni 20 za viroba bandia vya konyagi maeneo ya stendi kuu ya mabasi Bukoba.
Alisema katika hali ya kawaida, ni vigumu kwa mtu kutofautisha kiroba halali na bandia kwa sababu tofauti iliyopo ni ndogo sana huku akisema mhuri wa kiroba halali haufutiki na kwenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandikwa neno Konyagi na TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) wakati bandia hakina maneno hayo na mhuri wake unafutika hata kwa kusugua kwa kidole.
Chanzo;Habari Leo 

AMANI AGEUZIWA KIBAO BUKOBA

Anatory Amani BAADHI ya madiwani na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamelaani kitendo cha aliyekuwa Meya wa manispaa hiyo, Anatory Amani cha kuweka pingamizi mahakamani ili kuzuia kikao cha dharula cha madiwani.
Waakizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho juzi, baadhi ya madiwani hao akiwemo mbunge wa Viti Maaalum, Conchestaer Rwamulaza (CHADEMA), walisema inasikitisha kuona malumbano yaliyokuwepo wakati wa nyuma yakijitokeza tena kupitia kwa mtu mwenye maslahi binafsi.
Rwamlaza ambaye pia ni Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera, alisema kuwa hatua ya Amani kuweka pingamizi mahakamani ni kukwamisha maendeleo ya wananchi bila sababu.
“Sikufurahishwa na maamuzi haya aliyochukua Amani kwenda mahakamani kupinga vikao visiendelee. Tulikuwa na kesi baadhi ya madiwani wameondolewa nyadhifa zao wakituhumiwa kukwamisha maendeleo ya Bukoba lakini bado yeye kwa maslahi yake binafsi anaweka pingamizi tena,”alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Bakoba, Felician Bigambo (CCM), alisema kuwa japokuwa hawana mamlaka ya kuingilia uhuru wa mahakama lakini wamesikitishwa na hatua hiyo ya ubinafsi wa Amani ambaye pia ni diwani kata ya Kagondo.
“Tunaomba Serikali kuingilia kati hata kama mahakama haingiliwi, jamani angalia mtu mmoja anaamua kukwamisha na kuzuia vikao visiendelelee kwa maslahi yake.
Haingii akilini maana wenzetu walivuliwa nyadhifa wakidaiwa kukwamisha maendeleo, sasa wananchi wapime nani anawakwamisha,”alisema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza alisema kuwa Amani hapendi maendeleo ya Bukoba kwa sababu kila kinachofanyika yeye anaweka pingamizi mahakamani.
Wakili wa Amani, Alon Kabunga alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu kikao kilichoitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na Naibu meya, Alexander Ngalinda juzi hakikuwa halali kwani sheria, Amani bado inatambulika kuwa Meya Bukoba.
Chanzo;Tanzania Daima 

SERIKALI HAINA FEDHA ZA KULIPA FIDIA-MUHONGO

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali haina fedha za kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo Mradi wa Umeme Vijijini (REA) unatekelezwa mkoani Kagera.

Profesa Muhongo, alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa usambazaji umeme katika kijiji cha Katoke, wilayani Biharamulo, Kagera.

Alisema Serikali haina fedha za kuwalipa wananchi fidia katika maeneo ya mradi wa REA ingawa ni haki yao, kwa sababu hiyo italazimika kuhamisha mradi na kuupeleka ambako wananchi hawahitaji fidia bali nishati ya umeme.

Alisema kuwa, fidia ni utapeli na hakuna mahali ambapo fidia imetolewa (imelipwa ) kwa wananchi kesi zikaisha, hivyo wananchi waelezwe ukweli kuwa hakuna fedha za fidia. "Fidia ni haki yao, lakini hatuna fedha za kuwalipa.Sasa wafanye uamuzi, wanahitaji umeme au fidia.

"Kama ni fidia wasubiri baada ya miaka 20.Na kwa sababu hiyo tutahamisha mradi tuupeleke maeneo wasikohitaji kulipwa fidia," alisema Profesa Muhongo.

Alisema dhamira ya serikali ni kufuta umaskini na kuleta ajira mpya kwa kuwaunganishia wananchi umeme ambao utasaidia kukuza na kuboresha biashara zao, kilimo cha kisasa, kuboresha huduma za afya na elimu.

Aidha alisema tatizo ni wananchi kukataa kulipa fedha za kuunganishiwa umeme ambazo ni sh 27,000 tu,na kufafanua kuwa taasisi za umma (ofisi za watendaji, shule na zahanati) na taasisi za kidini (makanisa na misikiti) zitaunganishiwa bure nishati hiyo.

Profesa Muhongo, aliwataka Wahandisi nchini kuanzisha kampuni zao wafanye kazi za miradi mbalimbali ya ujenzi wa nishati ya umeme, badala ya kulalamika kuwa kazi nyingi wanapewa wageni badala ya wazawa.

Aidha Mratibu wa mradi huo mkoani Kagera, Mhandisi Julius Kateti wa kampuni ya Urban and Rural Engineering Service Ltd, alisema mradi huo utagharimu sh. 98 bilioni na utakamilika Januari mwakani.

Alisema zinahitajika nguzo 55,000 ili kukamilisha mradi huo na kampuni hiyo imeagiza nguzo nyingine kutoka nchini Uganda na Afrika Kusini

MTAMBO MPYA WA KUFUA UMEME WAFUNGWA KAGERA

 

WANANCHI mkoani Kagera wataondokana na tatizo la kukatika kwa umeme baada ya kufungwa mtambo mpya wa kufua Umeme (Transfoma) katika eneo la Kibeta kwa ajili ya kusambaza huduma ya umeme kwa wakazi wa mkoa huo.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco ) mkoani Kagera mhandisi Martine Madulu alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea eneo ilipofungwa transfoma hiyo.

Mhandisi Madulu alisema kuwa serikali imeamua kuleta transfoma hiyo mpya, iliyogharimu zaidi ya sh.Bilioni 1.3 kutokana na kuongezeka kwa wateja na kusababisha transfoma iliyokuwepo kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja.

“Transfoma hii ina uwezo wa kuzalisha megawati 12 za umeme tofauti na iliyokuwa ikitumika, ambayo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati nne… mahitaji ya wateja wote ambao ni zaidi ya 22,000 katika manispaa hiyo yaliishafikia megawati sita” alisema Meneja huyo.

Alisema kuwa transfoma hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja zaidi ya 22,000 tofauti na iliyokuwepo awali ambapo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia wateja 15,000.

Aidha Mhandisi Madulu aliwataka wananchi mkoani Kagera kuendelea kushirikiana na Tanesco katika kutoa taarifa kwa wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Wakati huo huo, alisema kuwa wameanza awamu ya pili ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA), ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwakani vijiji 400 mkoani Kagera vinatarajiwa kuwa vimenufaika kupitia mradi huo.

Kwa mujibu wa meneja huyo ifikapo mwakani wateja wanaohudumiwa na shirika hilo watakuwa wameongezeka kutoka idadi ya sasa hadi kufikia 36,000.

Kwa upande wake mhandisi wa Tanesco kutoka makao makuu,anayesimamia ufungaji wa transfoma hiyo, Amon Gamba alisema kuwa kufungwa kwa transfoma hiyo kutawezesha kuongezeka kwa idadi ya wateja na hivyo kuondoa malalamiko yaliyokuwepo ya umeme mdogo.

Chanzo;Majira

BAREGU:NAJUTA

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu, amejutia uamuzi wake wa kuendelea kuwa mjumbe wa Tume hiyo licha ya ushauri aliopewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kujitoa.
Prof. Baregu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amesema maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kubariki Bunge Maalum la Katiba liendelee kujadili Rasimu ya Katiba mpya bila kupatikana maridhiano kwanza, ni mbinu za chama tawala kutokuwa na nia ya kulipatia Taifa Katiba yenye maslahi ya wananchi.

Aprili 6, mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete aliteua watu 30 kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba akiwamo Prof. Baregu.

Tume hiyo pamoja na majukumu mengine, ndiyo iliyokwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mambo waliyotaka yawekwe kwenye Katiba mpya.

Awali kulikuwapo na taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa Chadema walimtaka Prof. Baregu kujitoa katika Tume hiyo ifikapo Aprili 30, mwaka 2012 kutokana na chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuelezea hofu yake kutokana na mchakato wa Katiba wakati ule ulivyokuwa unakwenda.

Hata hivyo, Prof. Baregu alisimamia msimamo wake, akisema kuwa ni haki yake na ataendelea kutekeleza jukumu la kulipatia Taifa Katiba bora kwa kuwa kwake Tanzania ni ya kwanza na mengine yanafuata.

Akizungumza na NIPASHE jana, Prof. Baregu, aliliomba radhi taifa yeye binafsi na kwa niaba ya wenzake 30 waliokuwa kwenye Tume hiyo, ambao kati yao hiyo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 Zanzibar.

Alisema hawanabudi kuomba radhi kwa kutekeleza mchakato wakiamini ni wenye lengo la kupatia Taifa Katiba mpya, kumbe walilaghaiwa wakatumika kuitumikia CCM kutafuta Katiba yake.

“Niligoma kujitoa kwenye Tume nilipotakiwa kufanya hivyo na chama changu (Chadema), nikiamini mchakato ulikuwa kwa maslahi ya taifa, kumbe tulilaghaiwa na sasa binafsi nimeamini Katiba inayotafutwa ni ya CCM na siyo ya Tanzania,” alisema Prof. Baregu.

Prof. Baregu alisema uamuzi wa CCM wa kubariki Bunge Maalum la Katiba liendelee siyo wa busara wala hekima bali umegubikwa na mihemko ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Kwa mujibu wa Prof. Baregu, kinachoelezwa na chama tawala kuwa kuna maendeleo mazuri  katika mchakato wa Katiba, ni kuondoa mambo yote yaliyo kwenye Rasimu ya pili, ambayo yalilenga kudhibiti nidhamu, uwajibikaji na utumishi bora kwa umma.

“Mgawanyo wa majimbo, ukomo wa mtu kugombea ubunge, miiko na maadili ya watumishi wa umma na mawaziri kutotokana na wabunge, vyote hivyo wanaviondoa kwenye rasimu wanataka kuunda utumishi au uongozi wa aina gani kama siyo unafiki?” alihoji Prof. Baregu na kuongeza:
“Hatunabudi kuomba radhi Watanzania tuliowaahidi kuwaletea Katiba Mpya.”

Alisema mpango huo una nia ya kufanikisha malengo ya muda mfupi na kuweka kando malengo ya taifa ya muda mrefu na kwamba unahatarisha usalama wa nchi kwani inaweza kuingia katika machafuko.

Kadhalika, alisema agizo la Kamati Kuu ya CCM kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, la kuendeleza usuluhishi kati ya makundi ya waliobaki bungeni na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni unafiki.

Alisisitiza kuwa hata kama Ukawa wangeamua kurejea bungeni, ingemaanisha ni kuridhia mambo ambayo hawakushiriki kuyaamua.

DK. SLAA ANENA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amesema kimsingi maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM hayana ushawishi wa kuwagawa Ukawa bali yanaviimarisha.

“Turuhusu hayo majadiliano yafike mwisho ambayo Kinana (Katibu Mkuu wa CCM) ameagizwa na Kamati Kuu chini ya Rais Kikwete kwamba akutane na vyama na wadau wengine ili kupata muafaka kwa sababu hata hivyo, ukilitazama tamko lao haliko committed (uwajibikaji) kwa upande wowote…

Naamini CCM haijafikia hali ya kukosa busara kiasi kwamba wakamwacha Samuel Sitta aendelee na Bunge lisilo na uhalali wa kisiasa,” alisema Dk. Slaa.

MHADHIRI WA RUCo
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha-Iringa, Rwezaura Kaijage, alisema uamuzi uliofanywa na CCM kubariki Bunge Maalum la Katiba kuendelea bila maridhiano, hauna tofauti na ubabe uliowahi kufanywa na baadhi ya viongozi wa Afrika wanaokumbukwa kwa ubabe wa kunyonga demokrasia.

“Huu ni ubabe ambao kimsingi hauna tofauti na wale viongozi wa Afrika wanaokumbukwa kwa kunyonga demokrasia, tusipoutazama kwa umakini zaidi uamuzi huo wa CCM hatutapata Katiba ya Watanzania ila tutapata Katiba ya CCM,” alisema Kaijage.

LHRC
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema pamoja na maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM, mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba unaashiria kuwa Katiba yenye maslahi ya taifa haitapatikana.

Alisema watu wengi walijua tangu mapema kuwa Bunge Maalum linaloendelea halitakuwa na jipya kutokana na wajumbe kuweka mbele maslahi yao badala ya maslahi ya wananchi.

Dk. Bisimba alisema Bunge Maalum la Katiba, linahitaji watu kuelewana ili kujadili na kukubaliana mambo ya msingi na kuunda Katiba yenye maslahi kwa Taifa.
 
CHANZO: NIPASHE

MWANALIBENEKE DOTTO KAHINDI NA ELIZABETH NGUMA WAMEREMETA‏

Baada ya kuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minane Dotto Paul Kahindi (Mandolin) na Elizabeth Riziki Morris Nguma, Agosti 9, 2014 Mungu amewajalia kufunga pingu za maisha kwenye kanisa la Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Assis, mjini Biharamulo, Kagera.

Dotto Paul Kahindi (Mandolin) na mkewe Elizabeth Morris Nguma katika pozi muda mfupi baada ya kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Asis, Biharamulo, Kagera.
Mr&Mrs Dotto na wapambe wao Mr&Mrs Frank katika pozi muda mfupi baada ya kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Asis, Biharamulo, Kagera.
Bibi Harusi akiwa na mpambe wake katika pozi muda mfupi baada ya kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Asis, Biharamulo, Kagera
Mr&Mrs Dotto, wapambe wao Mr&Mrs Frank, pamoja na wasimamizi wa ndoa hiyo Mr&Mrs Wema Rusasa katika pozi muda mfupi baada ya kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Asis, Biharamulo, Kagera
Bibi Harusi na Mameid

Mr&Mrs Dotto (Mandolin) na wapambe wao Mr&Mrs Frank katika picha ya pamoja na wazazi wa pande zote mbili
Maharusi wakiwa na wapambe wengine
Bwana harusi ni Baunsa sana tu
Mr&Mrs Dotto Paul (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya ndugu zao, kutoka kulia ni Mdogo wa bwana harusi Samweli, Kaka wa bibi harusi Deogratius, kaka wa bwana harusi Peter Kulwa na kaka wa bibi harusi Raygan
Bwana Harusi Dotto Paul na Bibi Harusi Elizabeth Riziki wakila kiapo wakati wa misa ya ndoa iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Francis wa Asis, Biharamulo, Kagera
Tumepokea vyeti

Mr&Mrs Dotto Paul wanameremeta
Mr&Mrs Dotto Paul katika picha ya pamoja na kamati ya harusi yao iliyofanyika kwenye ukumbi wa Rest mjini, Biharamulo, Kagera
Utambulisho
Wakati wa chakula
Mama wa bwana harusi Mary Charles Kahindi

Wakati wa zawadi

JUKATA YAWATETEA WALIOMEGUKA UKAWA

 VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kuacha kutoa kauli za kuwashughulikia wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaokiuka matakwa ama misimamo ya vyama vyao ili kusaidia mchakato wa katiba.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Deus Kibamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa wanachama wa Jukwaa la Katiba nchi nzima uliolenga kuwaelimisha juu ya namna ya kujadili rasimu ya katiba.

Kibamba alisema kuwa kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa siasa za kuwashughulikia wajumbe waliokiuka maazimio ya kundi moja juu ya mchakato wa katiba ndizo zinazaa mapigano miongoni mwao hivyo kuvuruga mchakato wa katiba.

"Kushughulikiwa kunazaa kupigana,watu wanapigwa sababu ya rasimu ya katiba na hata anayeonesha kutaka mchakato wa katiba usitishwe na yule anayesaliti msimamo wa UKAWA anaambiwa atashughulikiwa...sasa wanatakiwa kuacha kauli hizo na kushikana mikono ili kwa pamoja wajadili rasimu ya Katiba,' alisema Kibamba.

Aliongeza kuwa wananchi pamoja na wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wanapaswa kuvumiliana kwa hoja badala ya kujibizana kwa kuwa rasimu ya katiba ina mambo mengi ya kujadili ambayo hayahitaji majibizano.

"Sisi tunaongeza nguvu kwa Bunge Maalum kupitia mijadalatunayofanya na hawa wanachama wakirudi katika wilaya zao wataelimisha wengine namna ya kujadili rasimu pasipo kushikana mashati wala kushughulikiana," alisema Kibamba.

Kwa upande wake,Humphrey Polepole alisema kuwa ni vema Watanzania wakiwemo wanasiasa wakazuia tofauti za makundi na za vyama vya siasa ili kusaidia kusudio la Rais Kikwete la kupata Katiba Mpya.

"Tukisema tuzuie mchakato tutawapa nafasi watu wachache wasiotaka kupata Katiba Mpya,tushikamane pamoja kupigania mchakato huu kwani kila Mtanzania ana haki ya kushiriki kujadili katiba," alisema Polepole.

Chanzo:Majira

Wakulima Waneemeka na Elimu ya uzalishaji wa Mboga Mboga kutoka TAHA


Mh. Dr. Christine Ishengoma Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipokea taarifa kuhusu mfumo wa taarifa za masoko kutoka TAHA unavyofanya kazi zake kutoka kwa Cyrila Antony Afisa wa Masoko
Mkuu wa mkoa wa Iringa  Mh. Dr. Christine Ishengoma akisikiliza maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa kilimo wa TAHA Bw Ringo kuhusu uzalishaji wa zao la nyanya 
Elimu ikiendelea kutolewa
 Vitalu na green houses
 Aina Mbalimbali za matunda ambazo zimezalishwa na wakulima kutokana na elimu Bora waliyo ipata kutoka TAHA
 Mwananchi akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa TAHA
 Teknolojia ya umwagiliaji kwa mfumo wa kilimo cha matone ambao pia unaonesha utengenezaji bora wa matuta, nafasi na usafi
Hivi ni  Vitalu vya TAHA na Barton Tanzania
 Vitalu vya mboga na green house kama zinavyoonekana katika picha
 Watangazaji wa Radio Sweet FM ya Mbeya wakishangaa ubora wa karoti ambayo ni daraja la kwanza inapopelekwa sokoni
 Zao la chines
Zao la karoti lililopandwa kwenye vitalu vilivyopo ndani ya viwanja vya Nanenane Mbeya kwenye Banda la TAHA
 Mwananchi akifurahia maelezo kuhusu zao la karoti daraja la kwanza

********************
Wakulima na wananchi mkoani Mbeya wameendelea kuneemeka na elimu ya bure ya uzalishaji wa mazao ya mboga, viungo na matunda inayotolewa na Asasi ya wakulima, wafanyabiashara na watoa huduma ya mazao ya horticulture nchini Tanzania (TAHA).

Wakulima hao wameneemeka na elimu hiyo inayotolewa na maafisa wa ufundi wa kilimo kutoka TAHA kwa ushirikiano na wale wa Barton Tanzania ambao kwa pamoja wameweka kambi katika viwanja hivyo ili kuhakikisha jamii ya wakulima wa mboga kutoka ukanda wa Nyanda za Juu Kusini wanapata elimu ya msingi bora ya uzalishaji wa mboga wenye tija.

"Mpaka sasa tumetembelewa na wananchi na wakulima wasiopungua 460 ambao wamefika katika banda letu hapa Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale wakitaka kujifunza mbinu na misingi ya awali ya uzalishaji wa mazao ya horticulture, hiyo ni ishara njema kwani inaonesha ni kiasi gani wananchi  wanatafuta mbinu fasaha inayoweza kuwakwamua kutoka katika uzalishaji wa mboga wa kawaida mpaka uzalishaji wa tija unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa" Alisema Likati Thomas afisa Mawasiliano kutoka TAHA.
Akifafanua zaidi kuhusu elimu ya kilimo cha uzalishaji wa mboga kwenye banda la TAHA afisa mawasiliano huyo alisema kuwa wamepanda mazao tofauti katika ploti zilizopo kwenye eneo lao ambapo wakulima na wananchi wanaopata fursa ya kutembelea eneo hilo ujifunza teknolojia mbalimbali za uzalishaji kama vile uzalishaji unaozingatia Mbegu bora zenye tija.

Teknolojia nyingine ni pamoja na upandaji mazao unaozingatia nafasi kati ya miche na miche, umwagiliaji kwa njia ya matone(drip irrigation) unaozingatia uhifadhi wa maji na mazingira pamoja na ulimaji wa matuta yaliyoinuka ili kutoa nafasi kwa mizizi ya mimea kupenyeza kwenye udongo ili kujitafutia lishe.

Mbali na elimu hiyo ya uzalishaji wa mboga, wananchi wa Mbeya wanaotembelea banda hilo pia wanapata fursa ya kujifunza elimulishe kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya lishe wa TAHA Bi. Lawrencia …..ambaye amekuwa akiwafundisha wananchi juu ya umuhimu wa ulaji wa mboga na faida zake kwa afya ya miili yetu.



Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa