Home » » MWALIMU ADAIWA KUMUUA MWALIMU MWENZAKE KAGERA

MWALIMU ADAIWA KUMUUA MWALIMU MWENZAKE KAGERA

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kaiho, Kijiji cha Rwigembe, mkoani Kagera, Tumaini Samson (42) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mwalimu mwenzake, Samson Mwenda (26) kutokana na kumchoma kwa kisu kifuani na mgongoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe alisema jana kwamba mtuhumiwa anashikiliwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwigembe, Fidel Kamugisha alisema marehemu ambaye ni mwenyeji wa Singida aliuawa baada ya kutokea mzozo na mwenzake walipofika nyumbani wakitokea kwenye moja ya baa kijiji hapo.
“Walimu hawa walikuwa marafiki jinsi walivyoishi na hakuna aliyedhani kama wangezozana,” alisema Kamugisha.
Alisema baada ya kutokea tukio hilo, mwalimu Samson alijisalimisha kwa majirani kutaka kuomba msaada ili kumfikisha mwenzake Hospitali ya Ndolage lakini alifariki wakati juhudi za kuokoa maisha yake zikiendelea.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kaiho, Costantine Augustine alisema wakati wa uhai wake, Mwalimu Mwenda alikuwa akitimiza wajibu wake na kwamba, hakuwa na ugomvi na mtu hivyo tukio hilo limewashangaza.
Kuhusu uhusiano wa walimu hao, Augustine alisema licha ya kuishi nyumba moja na kutembelea mazingira ya kijiji, walikuwa wakizozana baada ya kulewa na hatimaye kusameheana.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa