MAGAZETI YA LEO JUMATATU TAR 23.06.2014

MAGAZETI YA LEO IJUMAA , KURASA ZA MBELE NA NYUMA

KAGERA WAHIMIZWA KUJIUNGA NSSF

WANANCHI mkoani Kagera, wametakiwa kujiunga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili waweze kupata mafao bora ikiwemo bima ya afya bure kwa familia.
Wito huo ulitolewa mjini hapa jana na Meneja wa Mafao ya Matibabu wa NSSF, Dk. Ally Mtulia, alipokuwa akisoma taarifa ya utakelezaji mkoani hapa katika siku ya zoezi la upimaji wa afya bure kwa Kanda ya Ziwa.
Dk. Mtula alisema shirika hilo litaendelea kuwahimiza wananchi kujiunga nalo, kwani kuna mafao mengi wanaweza kunufaika nayo na pia wanaweza kujipatia mikopo hasa wajasiriamali wadogo, ushirika wa bodaboda, wakulima kupitia vyama vya akiba na mikopo.
Alisema  mbali na kujiunga na NSSF, amewaomba wananchi  hao kujijengea tabia ya kupima afya zao, ili kujiwekea mfumo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kuepuka magonjwa sugu.
Zoezi la kila mwananchi kupima afya lilianzia mkoani Mara, Shinyanga, Geita ambako watu wengi walijitokeza kupima afya zao.
Chanzo:Tanzania Daima

WAVUVI WALALAMIKIA POLISI

WAVUVI wa Kisiwani Mazinga, Kata ya Mazinga wilayani Muleba, Kagera, wamelilamikia Jeshi la Polisi kwa kutoweka ulinzi wa kutosha katika Ziwa Victoria hali inayosababisha wavuvi hao kufanyiwa vitendo vya uhalifu na kuuawa.
Walisema hayo jana walipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuona jeshi hilo halichukui hatua kuhusu taarifa za kunyang’anywa zana zao za uvuvi, zikiwemo injini za boti katika tukio la hivi karibuni.
Mvuvi Misana Ramadhani mkazi wa mwalo wa Kimoyomoyo, Kijiji cha Mazinga, alisema hivi sasa wamechoshwa na vitendo vya uhalifu wanavyofanyiwa kila mara.
Thomas Josia ambaye ni mmiiki wa mitumbwi, alisema serikali wakati wa kutoza kodi mbalimbali inakuwa ya kwanza kufika visiwani na wavuvi wanakuwa mstari wa mbele kulipa kodi, lakini suala la usalama wao haijali.
“Rais Kikwete wakati wa ahadi zake alisema atapambana na uhalifu katika sekta ya uvuvi, lakini tunashangaa hakuna kinachoendelea hadi sasa badala yake tunazidi kuporwa mali zetu… tutaishije wakati ulinzi unapelekwa nchi nyingine wazawa tunateseka?” alihoji Josiah.
Diwani wa Mazinga, Alex Bakenjela, alisema baada ya Jeshi la Polisi kuona kilio cha wavuvi hao, limekubali na kushauri kuwepo kwa polisi jamii watakaobaini chanzo cha tatizo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, George Mayunga, alisema hajapata taarifa hiyo kutoka wilayani, huku akiahidi kufuatilia suala hilo.
Chanzo;Tanzania Daima 

'PAMBANENI NA UVUVI HARMU'

WANANCHI wa Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, wametakiwa kutumia elimu wanayopewa na maofisa uvuvi kupambana na kutokomeza uvuvi haramu, ili kuokoa kuangamia kwa Ziwa Victoria.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Ofisa Uvuvi Wilaya ya Muleba, Siymphorian Ngaiza, alipozungumza na Tanzania Daima ofisini kwake, kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uvuvi haramu katika ziwa hilo.
“Jamii ina wajibu mkubwa wa kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu kwa vile wao ndio wanaoishi na wavuvi wenye tabia kama hizo,” alisema.
Alisema kuwa aina ya uvuvi haramu ulioshamiri katika Wilaya hiyo ni ule wa kutumia nyavu zisizoruhusiwa ambazo ziko chini ya kiwango na zinazonasa samaki wadogo.
Aliwataka wavuvi kuzingatia sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kulipia ushuru wa usafirishaji wa samaki ili kuepuka usumbufu unaojitokeza wa kukamatwa.
Pia aliwashauri wakazi wa visiwani humo kuanzisha ulinzi shirikishi, ili kuwabaini wageni wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa injini na zana nyingine za uvuvi na kuwafikisha katika kituo cha polisi.
Chanzo:Tanzania Daima 

WATAHADHARISHWA KUEPUKA MAGONJWA

WAKAZI wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa malaria ili kupunguza idadi ya vifo vya watoto na wajawazito.
Kauli hiyo imetolewa  jana na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya,  Leontine Rwamulaza wakati  akihojiwa na Tanzania Daima  ofisini kwake kuhusiana na mlipuko wa magonjwa wilayani kwake.
Rwamulaza alisema wilaya hiyo inaongoza kwa ugonjwa huo katika Mkoa wa Kagera, na hivyo akawataka wananchi kuzingatia sheria na masharti ambayo wanakuwa wanapewa na wataalamu wanazunguka  katika vijiji.
Alisema wamechukua hatua za kupambana na ugonjwa huo kwa kuanzisha utaratibu wa kutembelea vijiji kupima kila mtu na ambae anabainika kuwa na ugonjwa huo hupewa dawa  ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuweka mazingira safi ili kuondoa mazalia ya mbu.
“Wilaya yetu ni kati ya wilaya tisa hapa nchini zinazoongoza kwa ugonjwa huu, na hii inatokana na kuwa na mito inayoaminika kuwa na mbu wengi na ambayo pia wananchi wanaishi karibu nayo,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima

CUF YAHIMIZA WANACHAMA KUWANIA UONGOZI

CHAMA cha Wananchi (CUF) Wilaya Bukoba Mjini, mkoani Kagera, kimewataka wanachama na wakereketwa wa chama hicho kuhamasishana kukipa nguvu chama pamoja na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa  baadaye mwaka huu.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la CUF, Saverina Mwijage, alipokuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya uliofanyika katika Manispaa ya Bukoba.
Mwijage ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, aliwataka wananchi wilayani Bukoba kutokata tamaa na badala yake wakitetee chama mbele ya Watanzania.
“Kwa kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unakaribia, nawaomba wapenzi, wakereketwa na wananchi wote kwa ujumla kuanza kujiandaa kwa kuwabaini wanachama ambao wanaweza kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, kwani msingi wa chama cha siasa kuwa na nguvu ni kuanzia kuchukua madaraka katika serikali za mitaa,” alisema.
Alisema kwa kipindi ambacho amekuwa nje ya Bunge, kuna mambo mengi amejifunza yanayohusu maendeleo ya wananchi wa Bukoba na yanayomshawishi kuanza kuhamasisha wananchi wa Bukoba kupigania chama, ili kiweze kuwainua kiuchumi wananchi.
“Bukoba imegubikwa na migogoro kila siku, wananchi hawapati kile kilichotarajiwa. Migogoro haimsaidii mwananchi, mimi nimeazimia kusaidiana na chama changu kutatua kero hizo,” alisisitiza Mwijage.
Katibu wa CUF Wilaya ya Bukoba Mjini, Ramadhan Bahati, aliwataka vijana, wanawake na wapenzi wa CUF wilayani humo kuanza kurudisha nguvu ya chama hicho kuanzia ngazi za kata.
Alisema dhamira ya chama hicho ni kurudisha nguvu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Chanzo:Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa