DHURUBA YALAZA NJE KAYA 122 KAMACHUMU

KAYA 122 katika Kijiji cha Bulembo, Kata ya Ibuga, Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera zimekumbwa na maafa kutokana na mvua na upepo mkali ulioezua nyumba zao na kuangusha migomba na mazao mengine kwenye mashamba yao.
Maafa hayo yameathiri wakazi zaidi ya 600 ambao hadi jana hawakuwa na makazi wala uhakika wa chakula.
Baadhi yao walisema kuwa hadi jana serikali ngazi ya wilaya na mkoa ilikuwa haijatoa msaada wowote kwao, ingawa Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alisambaza taarifa kwenye mtandao wa Friends of Bukoba (FoB) kuwa alikuwa ametoa taarifa kwa uongozi wa wilaya na mkoa.
Hata hivyo, taarifa zinasema wataalamu kutoka wilayani walikuwa kijijini hapo wakiendelea na ‘upimaji’ katika maeneo ya nyumba zilizoezuliwa wakiambatana na Mwenyekiti wa Kijiji, Trasias Kyabona.
Haikujulikana baada ya upimaji huo serikali itatoa msaada gani kwa wananchi hao.
Diwani wa Kata ya Ibuga, Joseph Rweyongeza Rwazo (75), anasema hajawahi kuona upepo mkali wa namna hiyo.
Dhoruba hiyo imeezua pia madarasa yote katika Shule ya Msingi Rugongo iliyo kijijini hapo.
Kijiji hicho kina vitongoji vinne – Bulembo, Bungezi, Butorogo na Katoma. Vyote vimeathirika kwa dhoruba hiyo.
Viongozi wa vitongoji na kijiji walizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Bulembo jana na kuthibitisha kuwa juzi na jana waliendelea kukutana na wanakijiji  ili kutafuta ufumbuzi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bungezi, Jason Mutema, alisema kwamba kwenye kitongoji chake pekee nyumba 82 zimeezuliwa na upepo.
Nyumba nyingine zilizoezuliwa katika vitongoji vingine ni kama ifuatavyo: Bulembo (27), Katoma (7) na Butorogo (5).
Kutokana na maafa hayo, viongozi hao na wanakijiji wengine wanaendelea na jitihada za kusaidia familia hizo, ambazo hadi jana zilikuwa zinaishi kwa taabu.
Wengine wamelazimika kuishi kwa majirani, wakati wakitafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Mvua za masika bado zinaendelea kunyesha na kuleta hofu kwa wananchi. Kuanguka na kung’oka kwa migomba kumeongeza misukosuko kwa wananchi hao, kwani migomba hiyo ambayo ndilo zao kuu la chakula mkoani Kagera, imeshambuliwa na ugonjwa wa ‘mnyauko’ ambao kwa muda sasa umekuwa unatishia usalama wa chakula mkoani humo.
Viongozi wa kijiji wanaendelea kuwasiliana na ndugu, wadau na serikali ili kunusuru familia zilizoathiriwa na maafa hayo.
Maeneo mengine yaliyoathirika na mvua za masika ni kata za Ngenge na Rutoro, ambako mafuriko yanahatarisha ustawi wa wananchi wa maeneo hayo.
Juzi Ijumaa, Mto Kasharunga ulifurika na kuzuia wananchi kwa siku nzima. Mafuriko hayo yalivuruga pia soko la wazi la kila wiki (Omujajaro) katika eneo la Omumpike, ambalo hutumika kuuza na kununua bidhaa kwa wakazi wa Rutoro, Ngenge na maeneo jirani.
Baadhi ya wananchi walinusurika kusombwa na maji. Kwa mujibu wa mwananchi mmoja, Robert Rwegasira, ambaye alikuwa anasafiri kutoka Kamachumu kwenda Rutoro na wenzake watatu, wananchi kadhaa, akiwamo mwenzake, Justin Kingi, waliokuwa wamepanda pikipiki, walikuwa wamesombwa na mkondo wa maji, lakini wananchi walifanikiwa kuwanusuru.
Tofauti na kata nyingine za Jimbo la Muleba Kaskazini, Kata ya Rutoro ni moja ya maeneo yasiyo na miundombinu ya kutosha.
Hakuna barabara. Hakuna mito ya kudumu. Hakuna visima vya maji.
Gazeti hili linahamasisha wananchi wa Muleba waishio popote ndani na nje ya nchi watakaopata ujumbe huu, wanaopenda kutoa mchango wa kusaidia wananchi hawa wawasiliane moja kwa moja na mratibu kwa simu namba 0758000225.
Chanzo:Tanzania Daima

WARAKA wa CCM juu ya Rasimu ya Katiba Mpya na Hatma ya Muungano

 SIKILIZA TONE RADIO BOFYA HAPA: http://www.toneradiotz.com/listenlive.php


‘Wazazi pelekeni watoto vyuo vya ufundi’

WAZAZI na walezi wametakiwa kuwapeleka watoto wao waliohitimu kidato cha nne katika vyuo mbalimbali vikiwemo  vya ufundi na utalii, ili kuwaongezea utaalamu zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Diwani  wa Viti Maalumu, Joyce Mirembe Aenda, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kayanga.
“Kushindwa kuendelea na kidato cha tano si kwamba mwanao hana akili au uwezo wa kujiendeleza, ondoa fikra  hizo, pelekeni watoto shule,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima

RC MASSAWE AIPIGANIA BUWASA

MKUU wa Mkoa wa Kagera (RC), Kanali mstaafu Fabian Massawe, amezicharukia taasisi, makampuni na watu binafsi wanaoshindwa kulipa bili za maji katika Mamlaka ya Majisafi na Majitaka ya Manispaa ya Bukoba mkoani hapa (BUWASA).
Aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kwenye  uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Maji, yaliyofanyika katika uwanja wa ofisi ya Kata ya Kibeta, Manispaa ya Bukoba.
Massawe aliitaka mamlaka hiyo kusitisha huduma ya maji pindi mteja wake anaposhindwa kulipa bili za maji ili kuokoa hasara inayoweza kuikumba mamlaka hiyo
Chanzo:Tanzania daima

Rweikiza Cup kutimua vumbi Machi 25

KITIMUTIMU cha kumtafuta bingwa wa Kombe la Rweikiza kinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Machi 25, mwaka huu na kushirikisha vijiji 92 vya Jimbo la Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
Kombe hilo litaanza kwa mchujo kuanzia ngazi za vijiji na hatimaye kata na kumpata mshindi wa kwanza, ambako zawadi kwa washindi zinatarajiwa kutajwa hivi karibuni na waandaaji wa mashindano hayo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Kishogo juzi, Katibu wa Michezo wa Jimbo hilo, Cajethanus Charles, alisema tayari mchakato umekamilika na kwamba, Machi 25 michuano itaanza katika vijiji mbalimbali na hatimaye kumpata mshindi wa kombe hilo maarufu kwa jina la Rweikiza Cup.
Hata hivyo, aliwataka viongozi walioteuliwa katika maandalizi hayo kuanza kuwaandaa vijana vema ili michuano iwe na mvuto zaidi kwa kupata pia mashabiki wengi wa kuiangalia.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ndiye muandaaji wa mashindano hayo, Jasson Rweikiza, alisema tayari amenunua mipira zaidi ya 1,000 na jezi za kugawa kwa timu zote katika vijiji husika, sambamba na mabasi mawili ambayo yatatumika kubeba wachezaji pamoja na dawa mbalimbali, hivyo wachezaji wanatakiwa kukaa mkao wa kula tayari kwa mashindano hayo.
Alibainisha kuwa amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara lengo likiwa ni kujenga umoja baina ya vijana waliopo kijijini humo na hata kuwafanya wawe katika hali ya kuwaza michezo na si kuwaza kujiingiza katika mambo mabaya ambayo katika jamii hayana nafasi.
Pia alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa sasa lipo katika mchakato wa kusaka vipaji katika wilaya mbalimbali, hivyo ingekuwa vema wakafika katika ligi hiyo ambayo anaamini vijana wake wana vipaji ili waweze kutangazika.

Chanzo;Tanzania Daima

Mchungaji atuhumiwa kuchochea uhalifu Muleba

Muleba. Watu watatu akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Chochea Moto, Elmes Fabian, wanashikiliwa na polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kufanya uhalifu, kufyeka mashamba ya migomba na kuvunja nyumba tatu za wakazi wa Kijiji cha Kishulo wilayani Muleba wakiwatuhumu kwa uchawi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kudai kuwa mchungaji wa kanisa hilo, wakiwamo watu watatu wanashikiliwa kwa kosa la kuchochea vurugu, kuidhuru miili na kuharibu mali kinyume cha sheria.
Kamanda Mayunga aliwataja walionusurika kuuawa kuwa ni Fabian Albert na mkewe Gaudensia Fabian, Methodia Leonard na Georgina Kayonga wote wakazi wa Kijiji cha Kashulo wilayani humo mkoani Kagera.
Alisema uchunguzi wa jeshi hilo umebaini baadhi ya wananchi wakiwamo watoto wa watuhumiwa wa ushirikina walifanya ukatili huo wakishirikiana na baadhi ya wananchi waliokuwa na lengo la kuwaua wazee wa familia hizo.
Tukio hilo limesababisha wananchi zaidi ya 12 wakiwamo watoto na wanafunzi wa shule za msingi kukosa makazi, huku wazazi wao wakilazimika kukimbilia kwenye Taasisi ya Kusaidia Wazee na Yatima ya “Kwa Wazee” iliyopo Kata ya Nshamba wilayani Muleba ili kupata hifadhi ya muda.
Aidha, alisema mchungaji wa kanisa hilo anadaiwa kuwahubiri waumini wake kuwa ana uwezo mkubwa wa kuwabaini wachawi ambao wamekuwa wakisumbua kijijini humo kabla ya kuanza kuwataja kwa majina.
Hatua hiyo, ilionekana kupokewa kwa hisia kali na waumini wake wakiwamo watoto wa watuhumiwa, hivyo kuungana na wananchi wengine kwenda kuharibu mali na kuwadhuru wazee hao kwa mapanga.
Kwa upande wake, Mratibu wa “Kwa Wazee”, Lydiah Lugazia alisema kutokana na ukatili huo kwa wazee hao wamelazimika kuwachukua na kuwahifadhi kwa muda, ili kunusuru maisha yao kutokana na wananchi kutaka kuwaua kwa imani potofu za kishirikina.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lambris Kipuyo akiongea na gazeti hili alitoa onyo kwa wananchi wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba wanapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama iwapo kuna mtu mwenye tuhuma mbaya katika jamii husika.
Alisema vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ni kuvunja sheria za nchi na kuondoa uhai wa mtu ni kuvunja sheria za mungu, hivyo wazingatie maadili ya kiimani na kufuata sheria.
Chanzo;Mwananchi 

NDEGE WA AJABU WAVAMIA MAKAZI KAGERA

Ndege wa ajabu wakiwa juu ya miti katika Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Ndege hao wamezua hofu kwa wakazi kutokana na kinyesii chao kudhuru mifugo na ndege.

Ndege wa ajabu wanaosadikiwa kutoa kinyesi chenye sumu kali, wamevamia Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao, huku ukali wa sumu hiyo ukisababisha kutoboka mabati ya nyumba zilizopo kisiwani humo.
Ndege hao wanaoaminika kuvamia kisiwa hicho mwezi mmoja uliopita tayari wameshasababisha vifo vya kuku 516 na mbuzi 12 wanaodaiwa kugusa au kula kinyesi chao. Hata hivyo, bado haijafahamika ndege hao wanatokea nchi gani.
Akithibitisha habari hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Massawe alisema Serikali ilipata taarifa hizo kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadaye kuundwa timu ya kutafuta taarifa za awali za tatizo hilo.
Massawe alisema ndege hao, pamoja na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao pia baadhi ya miti katika kisiwa hicho imekauka na mabati kutoboka inapotokea kinyesi chao kitaangukia kwenye paa za nyumba zao.
Pia Massawe alisema kuwa, taarifa ya kuwapo kwa ndege hao katika Kisiwa cha Musira, ilifikishwa kwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kebwe Stephene Kebwe aliyekuwa mkoani humo wiki iliyopita na kuwa suala la kuwapo kwa ndege hao siyo la ghafla kwa kuwa walikuwapo hapo awali.
Dk. Kebwe alisema wizara imetuma wataalamu kuchunguza tatizo hilo na kuwa wizara hiyo itaangalia ukubwa wa tatizo hilo linavyoweza kuwaathiri wananchi.
Hata hivyo, alisema suala hilo pia linahitaji ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Dk. Munda Elias alikwishawasili kwa ajili ya uchunguzi na kuthibitisha kuwa tayari kinyesi cha ndege hao kimepelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi na Mkoa unasubiri matokeo ya utafiti huo.
Naye Ofisa Tarafa wa Rwamishenye, Abdon Kahwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Ziporah Pangani alisema tayari Serikali imechukua hatua za kupiga marufuku kupeleka au kusafirisha mifugo kutoka kisiwani humo kwenda maeneo mengine kwa hofu ya kusambaa kwa sumu hiyo.
Pia alisema ndege hao wameleta hofu kwa wakazi wa kisiwa hicho, kwani kinyesi chao kinapodondoka kwenye bati hupata kutu na kutoboka, huku kukiwa na hofu nyingine kwamba huenda mifugo nayo imeathiriwa.
Chanzo:Mwananchi

Diwani ataka serikali iongeze walimu

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Kagera, limeiomba serikali kujizatiti zaidi kuzalisha walimu wengi hapa nchini ili kukuza sekta hiyo muhimu.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo, walipokuwa wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Walisema upo umuhimu kwa serikali kuweka mkazo zaidi wa kuzalisha walimu wengi wakiwemo wa masomo ya sayansi na hisabati, na kuleta walimu wa kujitolea kutoka nje ya nchi.
Chanzo;Tanzania Daima

Walimu Karagwe waomba mafunzo JKT

WALIMU wa shule za msingi na sekondari wilayani Karagwe, wameitaka serikali kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, ili kuwajengea ukakamavu katika maeneo yao ya kazi.
Wakizungumza katika mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) jana, uliowajumuisha walimu wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa, walisema walimu waliopitia mafunzo ya JKT na ambao hawajapitia wanaonekana wako tofauti kiukakamavu na katika utendaji kazi wao.
“Serikali itupeleke jeshini tukapate ukakamavu. Tuliwaona walimu waliopita jeshini walikuja na vitu vingi vya kuiga, nyimbo za hamasa za mchakamchaka, gwaride, michezo mbalimbali,” alisema.
Chanzo;Tanzania daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa