Home » » ABIRIA WA MV VICTORIA WAFUNGA BARABARA

ABIRIA WA MV VICTORIA WAFUNGA BARABARA

ABIRIA walisafiri kwa meli ya Mv Victoria wanaotokea Mkoani Kagera kuelekea jijini Mwanza wamefunga barabara kuu za mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani za Rwanda na Burundi baada ya kukwama katika Bandari ya Kemondo.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa nyakati tofauti  baadhi ya abiria waliolala katika bandari hiyo walisema, waliondoka bandari ya Bukoba saa 3 usiku na kufika Kemondo saa 6 usiku jambo ambalo sio la kawaida.
Gervas Mugisha Alisema walilala bandari hapo bila kupewa maelekezo yoyote na kulipopambazuka wananchi waliokuwa safarini wakalazimika kufunga barabara kuu ya magari yaendayo mikoani na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
“Abiria wengine wameamua kuondoka kwa sababu hawana mizigo mimi ni mfanyabiasha na nina mizigo hivyo siwezi kuondoka na kuacha mizigo yangu nina subiria utaratibu,” alisema.
Alisema, wakati wanaondoka bandari ya Bukoba baada ya mwendo wa saa 1 walishuhudia meli hiyo ikipoteza mwelekeo muda mfupi baadaye na kuzima na baada ya muda mfupi ili ilianza safari tena.
Mugisha alisema, kuwa kabla ya kufika Kemondo meli hiyo ilizima mara tatu hali  ambayo ilisababisha hofu kwa abiria ambao waliaanza kukimbilia maboya na kunyang’anyana hadi kufikia hatua ya kuyachana na ghafla meli hiyo ilianza safari tena.
Alisema cha kusikitisha walipofika Kemondo abiria waliowakuta hawakuelezwa jambo lolote na waliendelea na shughuli ya kupakia  mizigo ndani ya meli hiyo.
Salum  Sambaa, ambaye ni jamaa  wa  marehemu  aliyekuwa, akisafirisha mwili wa  marehemu kutoka Bukoba kuelekea Mkoani Morogoro kwa mazishi alisema, watumishi wa meli hiyo wameshindwa kuwa na lugha nzuri kwa abiria.
Alisema  muda wote meli hiyo ilipozima hawakutoa taarifa yoyote kwa abiria kwa muda wa zaidi ya saa nne.
Naye nahodha wa meli hiyo, Bembere Samson alisema, meli hiyo ilipata hitilafu katika mfumo wa umeme na kusababisha kupoteza mwelekeo kwa muda wa dakika kumi baada ya hapo hali ilirudi kama kawaida.
Alisema baada ya muda tatizo hilo lilijirudia na walipochunguza walibaini kuwa yanahitajika matengenezo ya kubadilisha kifaa ambacho kinasubiriwa kutoka jijini Mwanza.
Alisema, kuchelewa kufika kwa meli kumetokana na ukubwa wa mzigo uliobebwa ndani ya meli hiyo na sio ubovu kama wanavyodai baadhi ya wananchi.
Afisa mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra ) Kapteni Alex Katama alisema, wamezungumza na uongozi wa kampuni hiyo juu ya tukio hilo.
Katama alisema, meli hiyo ipo salama tatizo lililotokea ni la kawaida ambalo limetokana na mfumo wa umeme ulioleta hitilafu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa