Home » » TATIZO LA MICHE YA KAHAWA KUMALIZIKA

TATIZO LA MICHE YA KAHAWA KUMALIZIKA

WAKULIMA wa kahawa nchini, wanatarajia kuondokana na kero ya upatikanaji wa miche ya zao hilo, ifikapo Aprili mwaka 2015,baada ya kituo cha uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa (Tissue Culture) kuanza kuzalisha miche ya kahawa.

Kituo hicho kijulikanacho kwa jila la Crop Boiscience Solution kilichopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambacho kinafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na taasisi ya utafiti wa kahawa nchini TaCRI, kina uwezo wa kuzalisha miche ya kahawa zaidi ya milioni 10 kwa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Bw. Wilfred Mushoboz, alisema uzalishaji huo wa miche ni moja ya njia ambazo zinaweza kuzalisha miche mingi ya kahawa na kuondoa kiu ya Watanzania ya uhitaji wa miche.

"Upungufu wa miche ni moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wakulima wa kahawa nchini,lakini kwa sasa changamoto hiyo itaondoka, kwani kituo hiki kuna uwezo wa kuzalisha miche mingi hata zaidi ya milioni 10 kwa mwaka,kulingana na uhitaji wa wakulima;na sasa mchakato wa uzalishaji miche hiyo unaendelea na ifikapo Aprili mwaka 2015,tutaanza kusambaza miche hii," alisema Mushoboz.

Aidha, Mushoboz alisema uzalishaji wa miche hiyo ambao wamekuwa wakiufanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Kilimo, wamekuwa wakifuata utaalamu waliopewa na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI), na kwamba miche wanayozalisha ni bora ambayo imefanyiwa utafiti na ina ukinzani wa magonjwa.

"Miche ya kahawa tunayoizalisha hapa kwa njia ya matawi au vishina, ni ya aina zote yaani Arabica na Rubusta; na ni miche bora ambayo imefanyiwa utafiti na TaCRI; na miche hii ina ukinzani na magonjwa kama chulebuni, kutu ya majani na mnyaoko funzari; na inazaa sana, kwa kweli ifikapo mwezi Aprili mwakani, kilio cha wananchi kuhusu miche ya kahawa ndo itakuwa mwisho," alisema.

Akizungumza mtafiti wa usambazaji teknolojia na mafunzo kutoka TaCRI, Bw. Jeremiah Magesa, alisema kazi yao kubwa ni kuhakikisha teknolojia zote zinazopatikana katika taasisi ya utafiti wa kahawa Tanzania,zinawafikia wakulima.

"Sisi tumekuwa tukizalisha miche bora ya kahawa, lakini kutokana na mahitaji kuwa makubwa tumekuwa tukishirikiana na wadau mbalimbali, kikiwemo kituo cha uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa na tumeingia nao mkataba na kama alivyowaambia uzalishaji wake ni mkubwa, tatizo la upungufu wa miche litapungua kama si kwisha kabisa," alisema Magesa.

Wakizungumza baadhi ya wakulima wa kahawa mkoani Arusha walisema TaCRI, imekuwa ikiwapa utaalamu na kuwawezesha kuzalisha miche bora ya kahawa yenye ukinzani, kwa kuwapa vifaa na mbinu za uzalishaji wa miche bora

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa