Home » » TRAFIKI WATATU WAFUKUZWA KAZI

TRAFIKI WATATU WAFUKUZWA KAZI


JESHI la Polisi mkoani Kagera limewafukuza kazi askari wake watatu kwa kulifedhehesha jeshi hilo kutokana na kitendo cha kupiga picha inayowaonyesha wawili kati yao wakinyonyana ndimi wakiwa kazini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, alisema kitendo kilichofanywa na askari hao kimeshusha hadhi ya jeshi.
Aliwataja askari hao waliofukuzwa ni F.7788 PC Mpaji Mwasumbi, G 2122 PC Fadhili Linga na WP.8898 Veronica Mdeme ambao wote ni wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Misenyi.
Alisema PC Mpaji na WP Veronica walipiga picha inayokwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Polisi wakiwa kazini, huku PC Fadhili akiingia matatani kwa kuwapiga picha hiyo chafu askari wenzake na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Kamanda Mwaibambe alisema picha hiyo ilianza kuonekana katika mitandao mbalimbali ya kijamii mapema wiki hii.
Alisema askari PC Fadhili alipiga picha hiyo mwaka 2012 kwa kutumia simu yake ya kiganjani na kuitunza, lakini wiki hii aliamua kuisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kitendo ambacho ni kinyume na kazi yake.
“Napenda kuthibitisha kuwa picha hii iliyoonekana kwenye mitandao ya kijamii ni picha halisi ambayo haijachakachuliwa kabisa.
“Maadili ya kijeshi yapo kisheria na askari wetu wanafundishwa namna ya kuishi katika maisha ya utumishi wa jeshi na si vinginevyo.
“Jeshi halikubaliani na vitendo hivi, ikitokea askari kwenda kinyume lazima achukuliwe hatua kali,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Taarifa zaidi kutoka mkoani Kagera, zinaeleza baada ya kusambazwa kwa picha hiyo na kuonekana katika mitandao ya kijamii, WP Veronica alianguka ghafla na kupoteza fahamu kwa mshtuko wa tukio hilo.
Kutokana na hali hiyo, majirani waliokuwa karibu na nyumbani kwake walilazimika kumpatia msaada na kumkimbiza hospitali kwa matibabu, ambako aliruhusiwa juzi jioni kabla ya kutiwa mbaroni.
Chanzo:Mtanznia

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa