Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka.
Migogoro ya ardhi nchini haitamalizika iwapo viongozi wa serikali wataendelea kuwalinda watu wanaotumia fedha zao ‘kununua’ haki pasipo haki.
Akizungumza na NIPASHE, Mbunge wa Biharamulo (Chadema), Dk. Anthony Mbassa, alisema migogoro hiyo haitakuisha iwapo vitendo vya kulindana kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wenye fedha havitaondolewa.
Alisema kulindana huko kunasababisha baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mikononi baada ya kushindwa kuridhika na maamuzi yanayotolewa na vyombo vya serikali hususani mahakama.
"Iwapo vitendo vya kulindana miongoni mwa watumishi wa umma na kuwakumbatia watu wenye fedha hususani wafugaji wenye makundi makubwa ya mifugo havitaondolewa, italeta hatari kubwa ya kuendelea kutokea uvunjifu wa amani," alisema.
Alisema baadhi ya wenyeviti wa vijiji wamekuwa wakiuza ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kinyume cha sheria za ardhi kutokana na maslahi yao binafsi hali inayochangia ongezeko kubwa la migogoro hiyo.
Aidha, mbunge huyo alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutengeneza kikosi kazi kitakachoweza kuratibu kwa haraka migogoro yote inayojitokeza wilayani humo badala ya kuendelea kuwafumbia macho viongozi wasiowaaminifu.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum kata ya Nyakahura (CCM), Ziyuni Hussein, aliwatupia lawama baadhi ya viongozi wa chama na serikali kuwa chanzo cha migogoro hiyo kutokana na kuwakumbatia watumishi wabovu, hatua inayosababisha madiwani hao kushindwa kuchukua hatua za kuwawajibisha kisheria.
Zayuni alisema kila wanapofuatilia kujua wahamiaji wamepata wapi ardhi, huambiwa wamepewa baraka zote kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji na uongozi wa CCM wilayani humo.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Nassib Mmbaga, licha ya kukiri uwapo wa migogoro ya ardhi alisema atafuatilia kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kabla ya kutokea uvunjifu wa amani.
Hata hivyo, alisema halmashauri yake inatarajiwa kumpeleka mwanasheria wa halmashauri hiyo kwenda vijijini kutoa elimu kwa mabaraza ya ardhi ya kata ikiwa ni mkakati wa kuwajengea uwezo wa kutatua migogoro hiyo kabla ya kufikia hatua mbaya.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment