Home » » PINDA AVUNJA UKIMYA

PINDA AVUNJA UKIMYA

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, ameutaka uongozi wa Mkoa wa Kagera, kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba kwa manufaa ya wananchi.

Bw. Pinda alitoa wito huo juzi wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali mkoani humo baada ya kupokea taarifa ya Mkoa iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali mstaafu Fabian Massawe.

Katika kikao hicho, Bw. Pinda alimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jana mkoani humo.

“Naamini viongozi wa Mkoa huu, mtakaa kuzungumza ili muweze kukubaliana na kuondoa kesi iliyopo mahakamani, mkifanya hivyo kazi za kusaidia wananchi zitaendelea.

“Naumizwa na viongozi wa Mkoa huu, kukosa uchungu kwa kuwanyima wakazi wa Manispaa ya Bukoba, haki ya kupata maendeleo, kuna pesa zilizotolewa na Benki ya Dunia kiasi sh. bilioni 18 ambazo zinaweza kupotea kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache,” alisema.

Aliongeza kuwa, pesa za maendeleo zinapaswa kufanyiwa maamuzi katika vikao lakini watu wanashindwa kukutana kwa sababu ya mtu mmoja ambaye bila kujali maslahi mapana ya watu, anaenda mahakamani na kuzuia kila kitu kisifanyike hadi matakwa yake yatimizwe.

Akiwasilisha taarifa ya Mkoa huo, Kanali Massawe alisema tatizo la kisiasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba bado linaendelea ambapo hivi sasa kuna zuio la mahakama la kutofanyika vikao katika halmashauri hiyo ambalo limetolewa Agosti 25 mwaka huu hadi kesi namba 2/2014 itakapohitimishwa.

Alisema kesi hiyo ipo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba na nyingine mbili zinaendelea baada ya mahakamani kutoa hukumu ya kesi ya kutaka madiwani sita wavuliwe udiwani Juni 25 mwaka huu.

“Kuna kesi ya rufaa namba 11/2014 katika Mahakama Kuu ya Tanzania hapa Bukoba inayomuhusu Yusufu Ngaiza na wenzake watano dhidi ya Chifu Adronicius Kalumuna na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, wakipinga uamuzi wa kuvuliwa udiwani.

“Rufaa hiyo ilipokelewa Julai 18 mwaka huu na imepangwa kusikilizwa Oktoba 13 mwaka huu...kesi ya pili namba 02/2014 ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba ikimuhusu Anatory Amani ambaye anataka Mkurugenzi wa Manispaa amtambue yeye ni Meya wa Manispaa hiyo na kumpatia haki na stahiki zake,” alisema.

Aliongeza kuwa, kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 12 mwaka huu na imepangwa kuanza kusikilizwa Oktoba 6 mwaka huu ambapo Kanali Massawe alifafanua kuwa, kulikuwa na kesi nyingine namba 01/2014 katika Mahakama Kuu ya Anatory Amani dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mwanahseria Mkuu wa Serikali.

Alisema kesi hiyo ilifunguliwa Machi 7 mwaka huu ambapo mlalamikaji alitaka mambo kadhaa kuhusiana na taarifa ya ukaguzi maalumu ambayo ilitolewa Januari 17 mwaka huu yatenguliwe na mahakama.

“Aliiomba mahakama itengue taarifa hiyo akidai ni batili na isitambulike kisheria lakini mahakama imeiondoa kesi hiyo Septemba 25 mwaka huu kwa sababu ilipelekwa mahakamani hapo kwa kifungu kisicho sahihi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa