Home » » AUAWA KWA KUCHARANGWA MAPANGA

AUAWA KWA KUCHARANGWA MAPANGA

WATU wasiojulikana wamevamia Kanisa la Pentekoste Assemblies of God ( PAG ) usiku wa kuamkia leo Tawi la Kagemu, Kata ya Kitendaguro Manispaa ya Bukoba na kumuua mwalimu ambaye ni muumini wa kanisa hilo kwa kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali ya mwili.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo la tukio na kushuhudia sehemu ya madhabahu ikiwa imetapakaa damu, Mchungaji wa kanisa hilo, Faustine Joseph alisema, wamekuwa na kawaida ya kuomba hadi saa 4 usiku.
Alisema kuwa siku hiyo waliondoka saa 5 usiku na kumuacha marehemu aliyemtaja kwa jina la Dionis Ng’wangu na mwenzake wakiendelea na mkesha wa maombi.
Joseph alisema, alipata taarifa za tukio hilo majira ya saa 8 usiku baada ya kupigiwa simu na majirani wanaoishi karibu na kanisa hilo na kufika eneo hilo huku akikuta polisi nao wakiwa wamefika.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe alisema, kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa manane katika kata hiyo.
Kamanda Mwaibambe alisema mwili wa mwalimu huyo umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa huo huku muumini aliyetambuliwa kwa jina la Themistocles ambaye ni fundi ujenzi anaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo.
Alisema waumini hao walivamiwa na kundi la watu wanne hadi sasa mtuhumiwa mmoja amekamatwa kuhusiana na tukio hilo na jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa