Picha Ya Nyumba Za Asili Za Wahaya, Nyegera Waitu Bukoba


Ujenzi wa nyumba za asili za wahaya nyumba maarufu kama 'Omushonge' (msonge) Picha kwa hisani ya J. Kempanju ambae ni mdau nambari moja wa MjengwaBlog kwenye kijiji cha Itahwa- Bukoba.
Picha  zote na Mjengwa Blog

Mwenyekiti Wa Bavicha Taifa John Heche, Aendelea Na Mikutano Mkoa Wa Kagera


Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, akihutubia Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nsisha, Kagoma, Wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera.
Picha na Mjenngwa blog

AJABU LAKINI KWELI: BINTI AJIFUNGUA AKIFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA, NI HUKO MULEBA

Binti ajifungua akifanya mtihani wa Darasa la Saba.. alipata uchungu akiwa katika mtihani wa Hisabati, Aliomba ruhusa atoke nje lakini msimamizi akatia ngumu.. Mtoto apewa jina la OMR ....soma zaidi

‘VIJANA JISHUGHULISHENI’

na Antidius Kalunde, Bukoba
VIJANA mkoani Kagera wameshauriwa kujishugulisha na kazi mbalimbali za kuwaletea maendeleo na kutakiwa kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwasaidia kutatua matatizo ambayo yanawakabili kimaisha na kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa shirika la Maejor Alliance Education Center (MAEC) la mkoani Kagera linalojishugulisha na kupambana na dawa za kulevya hasa kwa vijana, Godfrey Innocent, alitoa ushauri huo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwemo utawala bora wa asasi na usimamizi wa fedha kwa wanachama wa shirika hilo.
Alisema kuwa kwa hivi sasa nguvu kazi nyingi ya vijana imepotea kutokana na kujihusisha na madawa ya kulevya ikiwemo uvutaji wa bangi unywaji wa pombe uliokithiri jambo ambalo limesababisha vijana kukumbwa na wimbi la umaskini.
Innocent aliongeza kuwa shirika hili la MAEC linajitahidi kwa kasi kubwa kuhakikisha linawashawishi vijana kutambua athari za utumiaji wa madawa ya kulevya na kuwataka wapinge utumiaji huo na kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Edwin Sebastian alisema jumla ya wanachama 45 wamenufaika na kupata mafunzo ambayo yamefadhiliwa na shirika la the Foundation for Civil Society ambao wao ndio watakuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine mkoani Kagera na kuongeza kuwa mbali na kutoa elimu watapata uongozi bora usimamizi wa fedha na uandishi bora wa miradi.
Aliongeza kuwa shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2007 mkoani Kagera limewanufaisha jumla ya vijana 1250 kwa kuwapa elimu bora na kuwanusuru na utumiaji wa dawa za kulevya na wao kuendelea kuwashauri vijana wengine.
Chanzo: Tanzania Daima

MBUNGE AWAPELEKA WAKULIMA 120 KUJIFUNZA UGANDA

Mwandishi wetu, Kagera Yetu
Wakulima 120 kutoka Wilaya ya Bukoba Mkoa Kagera wamepata fursa ya kwenda kujifunza jinsi ya kupambana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba huko Mbarara nchini Uganda.

Akizungumza na waandishi wa habari mjinji Bukoba Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba vijijini Bw. Ahmed Kyobya amesema kila kijiji kimewakilishwa na mkulima mmoja ambao idadi yao ni 92 baada ya kurudi watakuwa walimu wa wakulima kwenye vijiji vyao.

Bw. Kyobya amesema katika msafara huo wamo Madiwani kumi kutoka Halmashauri ya wilaya Bukoba, Maafisa Kilimo wanne,Maafisa wawili kutoka chuo cha utafiti wa kilimo Maruku na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mh,Jasson Rweikiza.

Katibu wa Mbunge huyo amesema ziara hiyo ya siku tatu itaanza Jumanne (Septemba, 18 mwaka huu) kuelekea Mbarara Uganda ambako watapata fursa ya kuwatembelea wakulima mbalimbali na kuwaonyesha jinsi wanavyopambana na ugonjwa huo wa mnyauko.

Aidha safari hiyo imedhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Mh.Jasson Rweikiza baada ya kuona ugonjwa huo unazidi kuongezeka Mkoani Kagera.
Blogzamikoa

USAFIRI KUTOKA KAGERA KWENDA KIGOMA WAREJEA

Na Renatha Kipaka, Bukoba
WAKAZI wa Kagera wanaotegemea huduma ya usafiri kati ya Miji ya Bukoba na Kigoma wamepewa uhakika wa kuwapo na huduma hiyo, baada ya kumalizika kwa mgogoro baina ya Kampuni za Bukoba Express na Vislam, uliodumu kwa mwezi mmoja.

Akizungumza mjini hapa jana, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) mkoani Kagera, Japhet ole Simaye, alisema huduma hiyo imerejeshwa na itakuwa ya uhakika kwa kila wiki.

Alisema tatizo la upatikanaji wa huduma ya usafiri wa kila siku kati ya Mji wa Bukoba na Kigoma lilisababisha abiria wa sehemu hizo kukosa huduma ya usafiri.

Alisema mgogoro uliokuwapo kati ya watoa huduma hiyo ni wa kupinga kuingiliwa katika ratiba zake za kusafirisha abiria ambazo ni Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ambao ulipingwa na Kampuni ya Bukoba Express.

Kutokana na mgogoro huo, ushauri uliopata muafaka ni kuishauri Kampuni ya Bukoba Express kusafirisha abiria Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, utaratibu uliotolewa hapo awali na kampuni hiyo kuupinga.

Julai, mwaka huu, SUMATRA walichukua hatua kwa kuwanyang’anya leseni ya usafirishaji wa abiria na kuwarudishia Agosti, baada ya kuomba msamaha na kukubali masharti ya kulipa faini ya Sh 250,000.

Aidha, amewataka wasafiri mkoani Kagera kuondoa shaka juu ya huduma za usafiri, kwa kuwa ofisi hiyo iko tayari kusimamia sheria.
Chanzo: Mtanzania

WANANCHI WAVAMIA MAHABUSU, WAUA MTUHUMIWA

na Ashura Jumapili, Bukoba
WANANCHI wamevamia mahabusu ya Mahakama ya Mwanzo ya Muhutwe, wilayani Muleba na kuvunja milango na kumtoa mtuhumiwa, Faustine Rweyemamu (60), mkazi wa Ndolange-Kamachumu na kisha kumpiga hadi kumuua baada ya kufanya jaribio la kutaka kumwiba mtoto kwa kumpeleka maeneo ya msituni.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mtendaji wa Kijiji cha Bisore, Dominic Damasenyi, alisema mahabusu huyo ameuawa na wananchi kwa kutuhumiwa kuiba mtoto mwenye umri wa miaka 15, aitwaye Zakhia  Hashimu.
Damasenyi alisema wananchi walimuona mwanaume huyo akiondoka na mtoto huyo wakiwa wamefuatana kwa karibu kutokea maeneo ya Muhutwe stendi kuelekea Muleba mjini.
Alisema baada ya wananchi kuona hivyo, walishituka na kuanza kumfuatilia na walipomkamata, askari walimpeleka katika mahabusu hiyo.
“Hali hiyo ilisababisha wananchi wenye hasira kuvamia selo hiyo na kisha kumtoa mtuhumiwa huyo na kuanza kumpiga kwa kutumia mawe hadi kufa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, alithibitsha kutokea kwa tukio hilo.
Chanzo: Tanzania Daima

MWANAFUNZI UAWA, ACHUNWA NGOZI

na Ashura Jumapili, Bukoba
MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyarigamba iliyoko Kata ya Muhutwe wilayani Muleba, mkoani Kagera, Beatha James (12), ameuawa kikatili na kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili na kung’olewa meno.
Mwili wa marehemu ambao ulipatikana baada ya siku nane maeneo ya kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya, ulikutwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama mkubwa wa marehemu, Eyudosia  Salvatory, aliyekuwa akiishi naye katika Kitongoji cha Bitende, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani Agosti 29 mwaka huu majira ya saa 3.30 asubuhi akielekea kwa mama yake mdogo mwingine aitwaye Mariagoleti Ishengoma.
Eyudosia alisema baada ya kufika huko alitumwa akafuate maziwa kwa jirani yao aitwaye Erasmo Sostenes, lakini akatumia muda mrefu bila kurejea ndipo walipopiga simu sehemu wanayochukua maziwa  wakaambiwa kuwa hajafika na maziwa bado hayajachukuliwa.
Alisema ilipofika saa saba za mchana walianza kumtafuta ndipo alijitokeza mama mmoja aliyemtaja kwa jina la mama Anneth, akawaeleza kuwa  wakati akiwa shambani majira ya saa nne asubuhi alimuona Beatha akiwa amefuatana na mwanaume mmoja aliyekuwa amebeba mfuko wa ‘safulet’ akamuuliza anakwenda wapi, akamjibu kuwa anamwelekeza mwanaume huyo njia ya kwenda Maziba ziwani maeneo ya Bubabo.
Aliongeza kuwa wananchi waliamua kufuatilia njia hiyo wakishirikiana na wanafamilia kumtafuta mtoto huyo na walipofika Maziba walielezwa kuwa walimuona akiwa amefuatana na mwanaume, lakini hawakujua walikoelekea.
Kwamba wakati  wakielezea  wasifu wa  mwanaume  anayedaiwa  kumchukua mtoto huyo, walielezwa kuwa watu  hao wanatunzwa  kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo waliyemtaja kwa jina la Jacob na wakati wakielekea huko walikutana na mtoto wake ambaye alikimbilia kwa baba yake.
Eyudosia alifafanua kuwa walipofika kwa Jacob walimhoji ataje walipo watu anaoishi nao, lakini akadai hajui walipo kwani walifika hapo kutafuta kazi na kwamba mmoja wao alimueleza kuwa ana dili la fedha la kwenda kuiba mabati maeneo ya Igurubiri.
Wananchi hao walimchukua Jacob hadi eneo la Muhutwe akiambatana na mtoto wake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, na kwamba walipombana alikiri kuwa mwanaume huyo anayetafutwa alifika kwao akiwa na binti, wakalala lakini waliondoka usiku akiwa ameshikwa na vijana.
Eyudosia alisema kuwa baada ya maelezo hayo, walipiga simu polisi ambao walifika na kumpeleka Jacob kituo cha Muleba kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa mtoto.
Alisema Septemba 7 mwaka huu, ndipo walipopata taarifa za kupatikana maiti ya mtoto huyo katika maeneo ya Kaboya karibu na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwamba taarifa za mwili huo zilitolewa na wawindaji wanaowinda wanyama waharibifu na kuwa walipofika walikuta mwili wa Beatha ukiwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyofolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Alisema sura ilikuwa imeharibika hivyo waliweza kumtambua kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa kabla ya kukutwa na mauti.
Mtendaji wa kijiji hicho, Dominic Damasenyi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba taarifa zilitolewa kwake na wanafamilia.
Damasenyi alisema madaktari walifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili huo kisha wakaruhusu shughuli za mazishi kuendelea.
Chanzo: Tanzania Daima

WANASIASA WANAOKATAZA WANANCHI KUTOA MAONI YA KATIBA MPYA WAONYWA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu

Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoani Kigoma wameonywa kuacha kuwakataza wananchi wasiende kwenye mikutano ya kutoa maoni yao juu ya mchakato wa katiba mpya.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma Khamis Bitese  alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari Mkoani hapo, ambapo alisema kutokana na mchakato wa utoaji wa maoni wanasiasa wengi wamekuwa wapotoshaji wa jamii, kwa kuwapotosha wanajamii wasiweze kutumia fursa hiyo ili hali wao wanaenda kwenye mikutano mbalimbali ambayo hutolewa na baadhi ya asasi zilizopo.

Bitese aliwataka wananchi kutambua haki zao pasipo kufuata utashi wa vyama vya siasa kwani kwa kufanya hivyo ni kujidhulumu haki zao wenyewe.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Miriam Mbaga alisema wamejipanga vyema kuhamasisha jamii kutoa maoni yao na tayari wameshatoa katiba 18 kwa baadhi ya madiwani ikiwa na chachu ya kuwaelimisha wakazi wa kata zao.

Pia alizitaka asasi zisizo za kiserikali kutumia nafasi zao kuelimisha wakazi wa Mkoa huo. Tume ya kukusanya maoni itaanza kazi zake Mkoani Kigoma kuanzia Septemba 13-28 mwaka huu.

Blogzamikoa

WAJAWAZITO 60% HUFARIKI KWA KUJIFUNGULIA NYUMBANI

na Mbeki Mbeki, Karagwe
DAKTARI Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Nyakahanga, Andrew Cesari, amesema vifo vya wajawazito na watoto wadogo ni asilimia 60 katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera kutokana na wanawake kujifungulia nyumbani.
Dk. Cesari alibainisha hayo alipokuwa akisoma risala katika maadhimisho ya miaka 100 ya hospitali hiyo yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Nyakahanga wilayani humo.
Alisema hali hiyo inatokana na wajawazito hao kukosa elimu ya afya ya uzazi, hivyo kutoona umuhimu wa kujifungulia hospitali.
Dk. Cesari alisema hospitali hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, wamejipanga kuboresha huduma ya afya kwa kutoa elimu katika makundi yote.
Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upungufu wa dawa, waganga, madaktari na watumishi wengine.
Dk. Cesari alisema katika maadhimisho hayo watu zaidi ya 3,000 wamepewa huduma ya matibabu bure, pamoja na kupatiwa vipimo mbalimbali wakiwemo wanawake 108 wa saratini ya matiti na uzazi wa mpango 73.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema serikali inatambua mchango wa kanisa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiroho na kwamba haitasita kuwaunga mkono.
Alisema serikali imedhamiria kuboresha huduma ya afya kwa kushirikiana na madhehebu ya dini.
Chanzo: Tanzania Daima

MGODI WA TULAWAKA SASA KUFUNGWA



Na Audax Mutiganzi, Bukoba
KAMPUNI ya kuchimba dhahabu ya African Barrick Gold (ABG), inatarajia kufunga eneo la Mgodi wa Tulawaka ulioko wilayani Biharamulo mkoani Kagera, katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja kuanzia sasa.

Kauli hiyo ilisemwa na Mwanasheria wa ABG, Godson Killiza, wakati wa kikao cha pamoja cha na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya mkoa huo.

Alisema Barrick ikishafunga sehemu ya mgodi huo, wataukabidhi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Misitu na Nyuki wautumie kama msitu wa hifadhi.

Alisema kampuni hiyo imeanza hatua za awali za kufunga eneo la mgodi, ambazo ni pamoja na kuotesha miti katika maeneo ya Kijiji cha Mavota kinachozunguka mgodi huo, kusawazisha ardhi na kuotesha mimea na nyasi za asili.

Alisema kampuni hiyo ina mkakati mkubwa wa kuyashirikisha makundi mbalimbali kabla ya kuufunga mgodi kwa njia ya vikao.

Alisema kampuni hiyo tayari imeshafanya vikao na ujumbe wa Wizara ya Maji, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wizara ya Nishati na Madini, Baraza la Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Misitu na Nyuki.

Alisema kampuni hiyo inaendelea na kuandaa vikao zaidi vya kujadili mikakati ya kuufunga mgodi huo.

Aidha, alisema watakutana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Wizara ya Fedha na Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), waandishi wa habari na wananchi wanaozunguka mgodi wa Tulawaka.

Alisema baada ya kufungwa eneo la mgodi huo, miundombinu na mali nyingine, ukiwamo uwanja wa ndege, mashine saba za kuzalisha umeme, eneo la makazi, karakana kubwa mbili, makontena na majengo ya utawala vyote vitakabidhiwa kwa Serikali.

Alisema Barrick inataka kuliacha eneo la mgodi likiwa na uasili wake.

Alisema mashimo yote yaliyokuwa yamechimbwa katika eneo la mgodi yatafunikwa.

Aidha, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, kuwa kabla ya kufunika mashimo hayo kampuni itahakikisha inafanya ukaguzi ndani ya mashimo hayo kwa ajili ya wavamizi wa machimbo wasifunikwe.

Chanzo: Mtanzania

MAZISHI YA RUGAMBWA KUGHARIMU MIL. 200/-



na Mwandishi wetu
MAZISHI ya kihistoria ya masalia ya mwili wa Kardinali wa kwanza barani Afrika, Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa, yatagharimu sh milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema masalia ya mwili wa Kardinali Rugambwa yatahamishwa kutoka Kanisa Katoliki la Kashozi yalikohifadhiwa kwa miaka 15 iliyopita na kuzikwa rasmi katika Kanisa Kuu la Bukoba, ambalo ukarabati wake umekamilika.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitatumika katika shughuli za mazishi pamoja na uzinduzi wa mfuko wa elimu wa Kardinali Rugambwa.
Alisema shughuli ya kuhamisha masalia ya mwili wake uliozikwa Desemba 17 mwaka 1997 itafanyika Oktoba 6, mwaka huu na kufuatiwa na maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwake, Oktoba 7, mwaka huu.
“Lengo ni kupata sh milioni 200 ambazo zingine zitakuwa kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa elimu wa Rugambwa. Fedha hizi tunaziomba kutoka kwa Watanzania wote watakaopenda kuchangia na tayari tuna kamati jijini Dar es Salaam na Kagera zinazopokea na kuratibu michango na safari ya kuja Bukoba kwa shughuli hiyo,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema mfuko huo wa elimu utaanzishwa kwa lengo la kumuenzi, kwani enzi za uhai wake, Kardinali Rugambwa alihamasisha elimu na kujenga shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Sekondari ya Rugambwa, ujenzi wa seminari kuu ya Ntungamo, Segerea na shule nyingine nyingi nchini ambazo hadi leo zinafanya vizuri.
Askofu Kilaini alisema wanatarajia kupata wageni wengi wa ndani na nje ya nchi ambapo Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, marais wastaafu, mawaziri, mabalozi wa nchi mbalimbali ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na watu mashuhuri ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kushuhudia tukio hilo.
Kardinali Rugambwa alizaliwa mwaka 1912 katika Kijiji cha Rutabwa na kupata upadri mwaka 1948. Alipata ukardinali mwaka 1960 na kufariki dunia Desemba 8 mwaka 1997 na kuzikwa Kashozi Desemba 17 mwaka 1997.
Kabla ya kifo chake, Kardinali Rugambwa aliagiza mwili wake uzikwe katika Kanisa Kuu la mjini Bukoba, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likijengwa upya kwa ajili ya kuuzika mwili wake.
Chanzo: Tanzania Daima

MWILI WA KARDINALI LAUREAN RUGAMBWA KUZIKWA UPYA OKTOBA 6, BUKOBA


Marehemu Kardinal Laurean Rugambwa enzi ya uhai wake.
Kanisa kuu katoliki jimbo la Bukoba ambalo masalia ya marehemu kardinali Rugambwa yatazikwa ndani yake.

========  ======= =======
MWILI WA KARDINALI LAUREAN RUGAMBWA  KUZIKWA UPYA OKTOBA 6, BUKOBA 

Kanisa katoliki nchini dayosisi ya Bukoba mkoani Kagera, wanajiandaa kuzika upya masalia ya mwili wa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo Kardinali Laurean Rugambwa, aliyefariki mnamo mwaka 1997 katika kanisa kuu la Bukoba. Maziko ya Kadinali Rugambwa yamepangwa kufanyika siku ya oktoba 6 mwaka huu.

Mwili wa askofu huyo wa kwanza nchini na Kardinali wa kwanza mweusi barani Afrika umezikwa katika kanisa la kwanza mkoani Kagera lililopo Kashozi kutokana na kwamba kanisa kuu la Bukoba ambalo marehemu aliagiza kuzikiwa ndani yake lilikuwa katika matengenezo makubwa.

Akizungumza katika kipindi cha Baragumu Channel ten na baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba Askofu  Methodius Kilaini , amesema wanataka kumzika kardinali Rugambwa kwa heshima tena katika kanisa alilopenda kuzikiwa kutokana na kukamilika kwake, lakini kabla ya kuzikwa humo kutatanguliwa na ibada mbalimbali ikiwa sehemu alikozaliwa, alikobatizwa, sherehe zitakazoambatana na kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa kardinali Rugambwa tarehe 7 mwezi Octoba.

"tuna alika watu wengi kuhudhuria kwenye tukio hili..., na pia tunakaribisha michango itakayowezesha kuwa na kitu cha kumkumbuka marehemu kwa mchango wake.... alisema askofu Kilaini.

Naye mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo , James Rugemalira, alimwelezea Kardinali Rugambwa kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kwenye jamii ya watanzania, kuanzia kwenye nyanja za elimu, afya na kiroho.

Marehemu Kardinali Rugambwa ana mambo mengi ya kukumbukwa na jamii ya watanzania hususani watu wa mkoa wa Kagera hasa kwa juhudi zake za kupeleka elimu mkoani humo kwa kuagiza ujengwaji wa shule za msingi na sekondari ikiwemo shule ya kwanza ya wasichana ya Rugambwa ambayo ujenzi wake ulikuwa ni mafanikio ya marehemu huyo kuomba msaada wa ujenzi wa shule hiyo alipohutubia bunge la Ujerumani akiwa mwafrika wa kwanza.

Licha ya mambo hayo yote kanisa hilo pia liko mbioni kuanzisha mfuko rasmi wa kumuenzi kardinali huyo mfuko utakaojulikana kwa jina la Kardinali Rugambwa ambao utakuwa maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Padre Laurean Rugambwa aliwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 10 Februari,1952. Alizaliwa julai 22 1912 na kufariki miaka 15 iliyopita.

ASKOFU MOKIWA: ACHENI KUHUBIRI KWA MAZOEA

Mwandishi wetu, Biharamulo-Kagera Yetu
Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuacha tabia ya kuhubiri kwa mazoea bali wahubili kwa maono ili kuiletea Jamii maadili yanayo kwenda sambamba na matakwa ya Mungu.
Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Angelikana Tanzania Dr Valentino Mokiwa wakati akihubili katika ibada ya ufunguzi wa nyumba ya askofu wa Dayosisi tarajiwa ya Biharamulo (leo jumanne)
Askofu Mokiwa amesema wapo baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakihubili neno la Mungu kwa mazoea ya kuyarudiarudia kila siku na hivyo kutokea mmomonyoko wa maadili katika jamii na kuwafanya waumini kutopenda kuyasikia.
Aidha amesema katika kuhakikisha jamii inamurudia Mungu viongozi wa dini wakiwemo wachungaji, wainjirist, Mashemasi Mapadri na masikofu kuacha tabi hiyo kwa kuwa wao ni kioo cha jamii inayo wazunguka.
Blogzamikoa

ASILIMIA 40 KYERWA WAHAMIAJI HARAMU

na Mbeki Mbeki, Kyerwa
MKUU wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Luteni Kanali (mstaafu) Benedict Kitenga amesema asilimia 40 ya wakazi wake wapatao laki saba ni wahamiaji haramu kutoka nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.
Alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya wilaya kwa Waziri wa Shirikisho la Afrika Mashariki, Samwel John Sitta aliyekuwa katika ziara yake ya kiserikali wilayani humo.
Kitenga alisema kuwa katika kata za Kibingo, Murongo na Kaisho asilimia 70 ya wakazi wake ni wahamiaji haramu kutoka nchi hizo.
Mbali na tatizo hilo, wilaya hiyo pia inakabiliwa na uharibifu wa mazingira na kuharibika kwa migomba inayoshambuliwa na ugonjwa wa mnyauko na uvuvi haramu uliokithiri.
Mkuu huyo aliongeza kuwa tatizo jingine ni kuongezeka kwa usafirishaji magendo ya kahawa kwenda nje ya nchi kunakofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa Kitanzania.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya wakazi, kumekuwa na ongezeko kubwa la utekaji wa magari ya abiria na migogoro ya ardhi na kuonya kuwa vitendo hivyo visipodhibitiwa vinaweza kuharibu uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.
Kitenga alisema kuwa uhamiaji huo haramu unaweza pia kuathiri mradi wa NIDA wa utolewaji wa vitambulisho kwa Watanzania kutokana na mwingiliano wa watu kuwa mkubwa hasa kwa wilaya zilizo mpakani.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alisema kutokana na takwimu za sensa mwaka 2002, wilaya hiyo ina wakazi zaidi ya laki nne na kuwa inasadikiwa kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kwa ongezeko la watu kwa asilimia 2.9 idadi yao itakuwa ni zaidi ya laki sita.
Kwa upande wake, Waziri Sitta amewataka wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana na serikali kudhibiti vitendo vya uhamiaji haramu, ambapo alisema kuwa Mkoa wa Kagera unasadikiwa kuwa na wahamiaji haramu 18,000.

Chanzo: Tanzania Daima

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa