Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Bilele ya Mjini Bukoba, mkoani Kagera,
Siasa Phocus amevuliwa madaraka kwa madai ya kuendelea na msimamo wa
kutaka wazazi wenye watoto shuleni hapo, waendelee kutoa michango
kinyume na agizo la serikali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera,
Nassoro Mnambila aliliambia gazeti hili jana mjini hapa kwamba mwalimu
huyo alishapewa utaratibu wa kuzingatia sera ya utoaji elimu msingi
bure, lakini alikaidi.
“Kwa mamlaka niliyonayo, nachukua hatua
hii kwa kumvua mamlaka mkuu wa shule Bilele kutokana na kushindwa
kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali…,” alisema Mnambila.
Alisema
mwalimu huyo aliendelea na msimamo wa kuwaambia baadhi ya wazazi
waliofika kuuliza utaratibu wa michango, kwamba hana taarifa na miongozo
ya serikali, akiwasisitiza kila mzazi kutimiza mahitaji yaliyopo kwenye
fomu ya mwanafunzi.
“Mwalimu huyo aliendelea
kutoa fomu kwa kila mwanafunzi iliyoainisha kila mahitaji kama
ilivyokuwa hapo awali (miaka ya nyuma) huku akitaka michango ya
madawati, karatasi za kuchapia mitihani na mlolongo wa gharama nyingine
nyingi,”alisema Katibu Tawala.
Michango mingine ambayo wanafunzi
wa sekondari wamekuwa wakitozwa kila mwaka ni ya fyekeo, ndoo, jembe,
uji, chakula cha mchana na uzio.
Katibu tawala alionya walimu
wakuu na wakuu wa shule, kuzingatia na kutekeleza sera ya utoaji wa
elimu msingi bure, kama ilivyo kwenye taratibu za miongozo iliyotolewa
kwao katika idara ya elimu.
Fedha zafika mikoani
Wakati
huo huo, mikoa mbalimbali imethibitisha kupokea fedha zilizotolewa na
Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure. Jumla ya Sh
bilioni 18.77 zimetolewa na serikali kwa ajili ya shule zote za umma
nchini.
Miongoni mwa mikoa iliyothibitisha kwa waandishi wa
habari kupokea fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza
elimu msingi bila malipo ni pamoja na Kagera, Morogo, Rukwa na Mwanza.
Ofisa
Elimu wa Mkoa wa Kagera, Aloyce Kamamba alisema wamepatiwa jumla ya Sh
810,157,000 ambazo zimeshaelekezwa kwenye akaunti za shule zilizoko
mkoani humo, ambapo za msingi ni 888 na sekondari 190. Kati ya hizo, 17
ni sekondari za bweni. Kiasi hicho kimetolewa na serikali kwa ajili ya
kugharimia huduma mbalimbali ikiwemo chakula.
Mkoani Rukwa, Mkuu
wa Mkoa, Magalula Said Magalula alisema wamepokea Sh milioni 336 ambapo
Sh 143,859,000 zimepelekwa kwenye shule za msingi 360 na kiasi
kilichobaki, kimepelekwa shule 105 za sekondari. Kwa mujibu wa Magalula,
fedha hizo ni kwa ajili ya mwezi huu kwani kila mwezi serikali itakuwa
ikitoa fedha kwa ajili ya mpango huo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari
Kalangasa Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri shule yake
kupokea Sh milioni 1.4 kwa ajili ya Januari mwaka huu. Katika Mkoa wa
Morogoro, Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo anayeshughulikia elimu,
Wariambora Nkya, alithibitisha kupokea Sh milioni 724.7 kwa ajili ya
shule 846 za msingi na 179 za sekondari za bweni na kutwa.
Mkoa
mwingine uliothibitisha kupokea fedha hizo ni Mwanza wenye shule za
sekondari 197, ambazo zimepewa Sh 642,648,000 kwa ajili ya fidia ya ada
za kutwa na bweni na chakula kwa shule za bweni. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Magesa Mulongo alisema upande wa Shule za Msingi, zipo 850 ambazo
zimepokea Sh milioni 356,728,000.
Alisema hadi Desemba 30 mwaka jana, shule zote zilishawekewa fedha kwenye akaunti zake.
Wahadharishwa matumizi
Walimu
wakuu, wakuu wa shule, bodi wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya
fedha hizo na wakati huo huo kuzingatia maelekezo ya serikali ya
kuhakikisha elimu msingi inatolewa bure.
Licha ya wakuu wa mikoa
na idara ya elimu kuhadharisha juu ya hilo, pia Wizara ya Fedha na
Mipango hivi karibuni, ilionya wakuu wa shule za msingi na Sekondari
watakaotumia ovyo fedha hizo zilizotolewa na serikali kutoa elimu bure,
ikisema atakayebainika kuzitumia isivyo, atashughulikiwa.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango iliwataka walimu katika
kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, waweke wazi fedha
walizopokea kutoka serikalini wananchi wafahamu alichopewa na matumizi
yake.
Bodi za shule zimepewa kazi ya kuhakikisha zinasimamia
matumizi na kutoa taarifa. Pia wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi
wamepewa wajibu wa kusimamia fedha hizo Sh bilioni 14.7, ambazo kati
yake, Sh bilioni tatu zimepelekwa katika vyombo vya usimamizi wa
mitihani.
HABARI LEO