Home » » WAATHIRIKA WA MAFURIKO WADAI KUTELEKEZWA

WAATHIRIKA WA MAFURIKO WADAI KUTELEKEZWA

BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Bulembo ambao walikumbwa na maafa ya nyumba zao kuanguka na nyingine kuezuliwa na mazao yao kuharibiwa na mvua, wamedai kutelekezwa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema walipatwa na maafa hayo Machi 20, mwaka huu, lakini hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kimekaa kimya wakati hawana chakula wala mahala salama pa kuishi na kwamba baadhi yao wanalala katika magofu.
Pia wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho kwa kugawa misaada kwa upendeleo.
Walisema misaada inayotolewa wanagawiwa hata ambao hawakuathiriwa na mvua hizo huku walioathiriwa wakiachwa.
Mmoja wa wananchi hao, Elipidius Christopher, mkazi wa kitongoji cha Bulembo, alisema nyumba yake ilianguka, mazao yake yote ikiwamo migomba, mibuni, magimbi na mihogo yameharibika, lakini amekuwa akibaguliwa wakati wenzake wanapopatiwa misaada.
“Sikupewa hema, nalala kwenye gofu nikiwa na watoto wangu, viongozi wangu wana taarifa kuwa nami ni mmoja wa watu walioathirika, lakini sifahamu kwa nini nabaguliwa,” alisema Christopher.
Pia walilalamikia uongozi wa kijiji hicho kupokea misaada ya vyakula na kuifungia stoo wakati wao hana chakula.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulembo, Longinus Clement, alikiri baadhi ya wananchi wake kutopatiwa misaada inayopelekwa kijijini hapo kutokana na kutoorodheshwa katika orodha ya awali ambayo inatumika kugawa misaada hiyo.
“Wakati wanapita kuorodhesha wananchi walioathirika katika kitongoji changu, mimi nilipewa kazi ya kuhesabu miti iliyoangushwa na upepo, niliporejea nilikuta viongozi wenzangu wamekwishaorodhesha waathirika, nikagundua kuwa kuna ambao walibaki bila kuorodheshwa,” alisema.
Clement alisema baada ya kugundua hilo aliwasiliana na viongozi wenzake lakini cha kushangaza walikataa kuwapatia misaada wakidai wanagawa kwa kutumia orodha ya awali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulembo, Trazias Kyabona, alisema wanaolalamika kuwa misaada inayotolewa imefungiwa stoo ni majungu, kwani kinachofanyika wanakusanya misaada midogomidogo na kuiweka pamoja  na baadaye kuigawa kwa wananchi.
Kyabona pia alikana misaada hiyo kuwagawia watu ambao hawajaathirika na kuwa misaada hiyo wanapewa kulingana na walivyoorodheshwa na kamati ya maafa ya kijiji kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya.
 Chanzo;Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa