WALIMU WANAOHUDHURIA MIKUTANO YA SIASA YA WAPINZANIA WAWAJIBISHWA

Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Bukoba Mkoa Kagera  kimesema kama mwalimu atawajibishwa kushiriki kuhudhuria mikutano ya vyama vya upinzani awajibishwe pia kuhudhuria mikutano ya Chama Cha Mapinduzi.wakati wa uchaguzi mkuu wa Serikali za Mtaa.

Hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) Mkoa Kagera Bw.Dauda Bilikesi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika (leo ijumaa) kwenye ukumbi wa Red Cros ulioko Manispaa ya Bukoba.

Bw.Bilikesi amesema CWT itahakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote kwani vyama hivyo vya siasa ni vizawa na hivyo mwalimu ana haki ya kusikiliza hali mradi asishiriki kuvaa sare,kupiga kampeini au kuchochea wapigakura waunge mkono chama kimoja.

Mwenyekiti Bilikesi amesema wapo baadhi ya viongozi wa siasa wameanza kutishia baadhi ya walimu  wawajibishwe baada ya kwenda kusikiliza mikutano ya viongozi wa vyama vya upinzani wakidai wasipowajibishwa wahamishwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu  (CWT) Manispaa ya Bukoba  Bw.Laulean Kashaija amewaasa walimu hasa wafundishao shule za sekondari wasiwe wachochezi wa kuwaongoza wanafunzi wamchague kiongozi yupi kati ya wagombea.

Bw.Kashija amesema walimu wa sekondari wanatakiwa kufundisha somo la Uraia kama mwongozo unavyoelekeza kama masomo ya kawaida.

Mkutano mkuu huo ulihudhuliwa na viongozi ambao ni walimu wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za kazi.

MKUTANO MKUU WA TATU WA PSPF WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM

Rais mstaafu wa awamu ya pili,Alhaj Ali Hassan Mwinyi, akizindua huduma mpya ya PSPF Pamoja nawe na PSPF call centre, itolewayo na mfuko wa Pensheni wa PSPF, baada ya kufungua Mkutano mkuu wa tatu wa wadau wa mfuko huo Feb 26.2014.
 Mgeni rasmi Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Hassan Mwinyi, kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, kulia kwake ni Ndugu Peter Ilomo aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya PSPF George Yembesi, Mkurugenzi Mkuu PSPF, Adam Mayingu na Katibu Mkuu MPAIC, John Haule
Wakurugenzi wa idara mbalimbali za mfuko wa Pensheni wa PSPF, mstariu wa mbele, wakiwa miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria mkutano mkuu wa tatu wa wadau wa mfuko huo kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa julius Nyerere jijini Dar es Salaam Februari 26, 2014.

  Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSPF, Neema Muro akijadili jambo na mmoja wa wadau wa PSPF

Usikivu 
 Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima akimkaribisha Mgeni Rasmi Rais Mstaafu wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alipowasili kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimtaifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, kuhudhuria mkutano mkuu wa tatu wa Mfuko wa PSPF wa wadau Februari 26.2014.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Adam Mayingu (kushoto), akimkaribisha Mgeni Rasmi Rais wa Mstaafu Ally Hassan Mwinyi kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimtaifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, kuhudhuria mkutano mkuu wa tatu wa Mfuko wa PSPF wa wadau Februari 26.2014.


 Kutoka kushoto ni Meneja wa Kitengo Mawasiliano ya simu, Fatma Elhadgy, Meneja wa Mawasiliano, Masoko na Uenezi wa PSPF, Costantina Martin na Ephraim Kibonde 

 Mgeni rasmi Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Hassan Mwinyi 
Mgeni rasmi Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi akionyesha zawadi aliyopewa na PSPF, kushoto kwake ni Ndugu Peter Ilomo aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya PSPF George

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TANGAZO LA MKUTANO MKUU WA WADAU WA PSPF

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MFUKO WA PENSHENI WA
PSPF

TANGAZO LA MKUTANO MKUU WA WADAU
Mfuko wa Pensheni wa  PSPF unatangaza kwamba kutakuwa na Mkutano Mkuu wa tatu wa wadau utakaofanyika tarehe 26 na 27  Februari 2014 kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa kumi jioni katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo barabara ya Shaban Robert  jijini Dar es salaam.
Madhumuni ya Mkutano huu ni kutoa taarifa ya hesabu ya mwaka na utendaji wa Mfuko na kutathmini mafanikio na changamoto zinazokabili Mfuko na sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa ujumla.
“PSPF - TULIZO LA WASTAAFU”
Mkurugenzi Mkuu
Mfuko wa Pensheni wa PSPF,
Makao Makuu,Golden Jubilee Towers,  S.L.P 4843. Dar-es-Salaam.
Simu: +255222120912/52 au +255222127375 /6
 Nukushi: +255222120930

 Barua pepe:pspf@pspf.tz.org

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Mbaroni akidaiwa kuuza nyama ya binadamu

Ngara. Mkazi wa Kijiji cha Kihinga, Kata ya Bugarama wilayani Ngara mkoani Kagera(jina tunalo), anashikiliwa katika kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo baada ya kutuhumiwa kuuza kilo moja ya nyama ya binadamu kwa Sh100,000.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kihinga, Hassan Mohamed alisema kuwa jana saa mbili usiku, wananchi walipeleka fedha nyumbani kwake kununua nyama hiyo na alipowaona alikimbia na wananchi hao kwa hasira walimkimbiza ili kumuua na hapo hapo kuunguza nyumba yake.
“Mgambo ndio walimnusuru asiuawe na wananchi wenye hasira kali na alikimbizwa kituo kidogo cha polisi Kata ya Bugarama ili kuokoa maisha yake “.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa mgambo wa kijiji hicho, Emanuel Kaloli alisema wananchi waliandamana baada ya kusikia taarifa za kuwapo mtu anayeuza nyama ya binadamu na kutaka kuhakikisha ukweli huo.
Alisema baada ya wananchi kufika, walianza kumshambulia na kutaka kumuua, lakini wanamgambo wa kitongoji walifika kisha kumuokoa mtuhumiwa na hatimaye kumfikisha kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wake.
“Kijana aliyefahamika kwa jina la Man Balyamwabo mkazi wa Shina la Kalenge katika kitongoji hicho, ndiye aliyeambiwa kuwa angeuziwa nyama hiyo ya binadamu na kuleta taarifa katika uongozi wa kijiji ili uweze kuchukua hatua zaidia”.Alisema Kaloli.
Alisema nyumba aliyounguziwa pamoja na mali iliyokuwamo ndani hasa maharage, mavazi na vitu vinginevyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Sh2.6milioni. Pamoja na kuwepo kwa tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema mtuhumiwa inasemekana ni raia wa nchi jirani ya Burundi na alianza kuishi katika kitongoji hicho tangu mwaka 1981 kama kibarua wa kilimo kwenye mashamba.
Taarifa zinasema kuwa katika kuishi kwake na ndugu yake aliyefahamika kwa jina la Kahungu walikuwa wakituhumiana kwa uchawi na ilifikia mahala wakatofautiana na kaka yake ambaye alirejea kwao.
Polisi wilayani Ngara imethibitisha kumpokea mtuhumiwa huyo na kwamba linafanya mahojiano ya kina kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Chanzo;Mwananchi

NYAVU ZA SH. MIL 781 ZATEKETEZWA

Zana haramu za uvuvi zipatazo 6,347 zenye thamani ya shilingi milioni 781.6 zimekamatwa na kuteketezwa kwa moto katika kipindi cha siku kumi na nne.

Afisa mfawidhi wa kikosi cha doria mkoani Kagera Aporinary Kyojo amesema kuwa zana hizo zilikamatwa katika oparesheni maalum ya kukamata zana haramu katika ziwa Victoria, iliyofanyika kuanzia Februari 3 hadi Februari 16 mwaka huu.

Kyojo ametaja zana haramu zilizokamatwa kuwa ni makokoro 59, nyavu za timba 670, makila 5,570,  nyavu za dagaa zenye macho madogo 48 na kamba za makokoro zenye urefu wa mita 51,200.

Amesema kuwa pia katika oparesheni hiyo walikamatwa samaki wachanga aina ya sangara kilogramu 4,648 wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 13.9, mizani mibovu 17, mitumbwi isiyokuwa na usajili mitano na watuhumiwa 13.

Amesema kuwa katika oparesheni hiyo ya pamoja ya kanda ya Afrika Mashariki dhidi ya uvuvi haramu, iliwahusisha maafisa kutoka makao makuu ya wizara ya uvuvi jijini Dar-es-salaam, polisi, wataalam wa uvuvi kutoka mkoani Kagera, kamati za usimamizi wa mialo (BMU) na waangalizi kutoka nchini Uganda.


Oparesheni hiyo ya siku 14 iliandaliwa na mradi wa Smart Fish unaofadhiliwa na jumuiya ya nchi za Ulaya chini ya kamisheni ya bahari ya Hindi (IOC) na kuzishirikisha nchi za Uganda na Tanzania.

‘Wanawake, watoto tambueni haki zenu’

WANAWAKE na watoto wametakiwa kuzitambua haki zao za kimsingi katika jamii ili kuepukana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyokithiri wilayani Karagwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Women’s and Men’s Development Association (WOMEDA) iliyopo mjini Kayanga, wilayani hapa, Juma Masasi, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema wanawake wilayani humo wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili na ukatili wa kisaikolojia.
Masasi alisema shirika lake limeweza kupokea kesi mbalimbali za aina hiyo zikiwemo za ndoa, talaka, mikataba ya ajira, za madai na mirathi.
Alisema shirika lake kwa kuungana na mashirika mengine kama Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), madawati ya kijinsia watahakikisha wanapambana na vitendo vya kikatili bila woga.
Chanzo;Tanzania Daima

Maeneo ya Ikulu yageuzwa uwanja wa ngono, ukabaji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga.
 
Wananchi wa mtaa wa Pwani katika Manispaa ya Bukoba, wamelalamikia vitendo vya ngono vinavyofanyika katika maeneo ya Ikulu ndogo na kutaka vidhibitiwe kwani  vinaidhalilisha serikali ya mkoa Kagera.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliotishwa na Mwenyekiti wa mtaa huo kuzungumzia hali ya ulinzi na usalama katika mtaa wao, wananchi hao walidai kuna watu wamekuwa wakiegesha magari yao karibu na makazi ya mkuu wa mkoa huo na kufanya vitendo vya ngono ndani ya magari.

Walisema kila siku ikifika saa 12 jioni hadi saa mbili usiku watu wasiofahamika huegesha magari yao na kufanya ngono katika eneo la Gymkhana  na kuliomba Jeshi la Polisi kuwakamata watu hao.

Mbali ya kulalamikia vitendo hivyo vya ufuska katika eneo hilo, pia wamelalamikia wizi wa mara kwa mara unaotokea katika makazi yao ikiwamo vitendo vya kukaba watu, wizi wa mifugo na ukwapuaji kutokana na mtaa huo kuwa karibu na ziwa.

Walisema wezi wamekuwa wakiwapora akina mama fedha wanapokuwa wakienda kununua samaki mwaloni wakati wa alfajiri.

Mwenyekiti  wa mtaa huo, Evord Barnaba alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya wizi na ngono katika eneo hilo, walilitaarifu Jeshi la Polisi ili kuwakamata wahusika na kuchukua hatua ya kuweka vibao vya kuzuia watu kuegesha magari katika eneo hilo wakati wa usiku lakini vitendo hivyo vinaendelea.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu katika mtaa huo wenye wakazi 1,457 asilimia kubwa wakiwa ni watumishi wa serikali, wananchi hao waliazimia kuchanga Sh.

3,000 kila mmoja kwa kila mwezi kwa ajili ya kuajiri kikundi cha vijana cha kulinda maeneo hayo wakati wa usiku kama njia mojawapo ya kukabiliana na vitendo hivyo. 

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga aliwaagiza mkuu wa polisi wa wilaya na mkuu wa polisi wa tarafa Rwamishenye kuhakikisha zinafanyika doria katika maeno ya Ikulu ndogo ili kudhibiti wizi na vitendo vya ngono katika eneo hilo.

“Sitaki tena kusikia vitendo vya uhalifu vimetokea katika maeneo hayo na ikifika usiku watu wasipite katika maeneo hayo, ni uzembe mkubwa kuruhusu zifanyike ngono na katika maeneo hayo”  alisema kamanda Mayunga.
 
CHANZO: NIPASHE

Wauzaji wa samaki watuhumu kiwanda kwa kuwahujumu

Baadhi ya wafanyabiashara wa samaki mjini hapa wamedai mitaji yao inahujumiwa na Kiwanda cha Kuchakata Minofu ya Samaki cha Vicfish, kwa kuwalipa bei ndogo kwa madai kwamba wanapeleka samaki wengi wasio na ubora.
Walalamikaji hao majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za biashara, walidai kiwanda hicho kinatumia kisingizio hicho ili kipate sababu ya kununua samaki wao kwa bei ya chini.
Walidai kuwa mbinu hiyo imesababisha wafanyabiashara wengi wa samaki kufilisika.
Waliendelea kuwa samaki wasio na kiwango maarufu reject (wasiofaa) hulazimika kuwauza kwenye kiwanda hicho kwa bei ya Sh250 kwa kilo, badala ya bei ya kawaida ya Sh800 na kwamba, licha ya kupeleka samaki wa viwango sawa, malipo hutolewa kwa viwango tofauti.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, alidai aliwahi kupeleka tani moja ya samaki aina ya sangara na kuambiwa kilo 700 hazikuwa na kiwango cha ubora unaotakiwa na kiwanda hicho, hatua iliyiosababisha kuziuza kwa bei ya Sh250 kwa kilo.
Pia, walidai wanalazimika kuuza kwa bei inayopangwa na mnunuzi kwa sababu baada ya kuwafikisha samaki hao kiwandani, hawawezi kupata soko jingine na mmoja wao kudai mbinu hiyo imemfanya abaki na madeni mengi ya wavuvi.
Hata hivyo, Meneja wa kiwanda hicho, Nurdin Salim alikanusha madai hayo na kwamba, anazo nyaraka zinazoonyesha saini za walalamikaji kwa samaki wasio na ubora wanalipwa Sh800 badala ya 250 kama walivyodai.
Salim alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaouza samaki kiwandani hapo hutoa madai yasiyo na ukweli, huku wengine wakidaiwa fedha nyingi na kiwanda na kwamba kama hawaridhiki na bei siyo lazima wauze samaki katika kiwanda hicho.
Chanzo;Mwananchi

Mgeja atamba CCM ipo imara hakuna wa kuiyumbisha

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Byantanzi, wilayani Muleba, wamemuomba Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka,  kushughulikia  mgogoro wa ardhi inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji.
Wakizungumza na gazeti hili juzi katika kijiji hicho, wananchi hao walisema uongozi wa  wilaya, umewapa muda wa miezi sita kuhama katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na mwekezaji.
Walisema hata hivyo amri hiyo imetolewa  bila wao kupewa maeneo mbadala ya kuendesha maisha yao.
Walielezea kushangazwa kwao juu ya taarifa za kuuzwa kwa eneo hilo kwa mwekezaji, wakati  uongozi wa kijiji ukiwa hauna taarifa.
Mmoja wa wananchi hao, Faston Benson, alisema wananchi katika kijiji hicho, wamekumbwa na hofu baada ya kuelezwa kuwa wanatakiwa kuhama ili kumpisha mwekezaji.
Diwani wao, Khalid Hussein (Chadema) alielezea kushangazwa kwake juu ya  amri iliyotolewa na uongozi wa wilaya hiyo ikiwataka wananchi, kuhama katika eneo hilo.
Alisema inashangaza kuwa viongozi waliotoa amri hiyo, hawakuwahi kwenda katika kijiji hicho  na kuwasikiliza wananachi.
Mwenyekiti wa Kitongozi cha Ntungamo, katika kijiji hicho, Desdery Hurubano alisema zaidi ya kaya 300 katika eneo hilo zinaishi kwa hofu kutokana na vitisho vya kuhamishwa.
Aliwasihi uongozi wa wilaya kwenda  katika kijiji hicho ili kusikiliza malalamiko ya wananchi badala ya kuwapa vitisho vya kutaka wampishe mwekezaji.
Hurubano alisema jambo hilo halikubaliki na kwamba ni vizuri viongozi waka wazi  kwa wananchi wa kijiji hicho.
Kiongozi huyo wa kitongoji alisema inashangaza na kusikitisha kuona wananchi walioishi katika eneo kwa muda mrefu, waamriwa kuhama bila kushirikishwa.
Chanzo;Mwananchi

Wakazi wakiri kula kinyesi bila kujua wilayani Karagwe

Karagwe. Baadhi ya wananchi wa  Kijiji cha Kafunjo, Kata ya Kiruruma, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, wamesema wamekuwa wanakula kinyesi bila kujua kutokana na kutokuwa na vyoo bora.
 Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo  mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kutembelewa na Ofisa wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Wilaya ya Karagwe, kuwaelimisha jinsi ya ujenzi wa vyoo bora na matumizi yake.
Mmoja wa wakazi hao,  Renatus Kanyabuhura alisema kutokana na kutokuwa na vyoo bora, walikuwa wakila kinyesi kwa sababu walikuwa wakitoka chooni bila kunawa mikono na kuvuta sigara huku  wengine kula matunda.
“Kutokana na kutokuwa na vyoo bora, unakuta nzi wanaotoka chooni wanatua kwenye chakula na huku mlaji anaendelea, jambo linalojionyesha tunakula kinyesi,” alisema Kanyabuhura.
Naye Ofisa wa Afya, Moses Aligawesa alisema magonjwa mengi yanatokana na matumizi mabaya ya vyoo na kula kinyesi kwa njia tofauti.
Aligawesa alitaja magonjwa yanayotokana na kula kinyesi kuwa ni, kipindupindu, kuhara, kichocho, safura (minyoo) na kwamba,  magonjwa hayo yanaathiri kila mmoja kuanzia familia, kijiji, kata hadi taifa. Alisema choo bora ni shimo lenye urefu wa futi 12 na kuendelea, kinachosafishika, kuezekwa   bila kusahau kunawa mikono kwa kutumia maji na sabuni.
Chanzo;Mwananchi

RC awapa kibarua watendaji

MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, amewataka watendaji wa vijiji na kata kuwafikisha mahakamani wazazi wanaowaozesha  watoto wao chini ya umri na wale wanaowapa ujauzito na kuwasababishia kutoendelea  na masomo.
Kanali mstaafu Massawe alitoa wito huo juzi wakati wa maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika kimkoa wilayani Kyerwa.
Alisema watendaji wa vijiji na kata hawana budi kuwachukulia hatua watu wanaohusika kuwapa ujauzito wanafunzi na kuwaharibia  ndoto zao za kupata elimu na kuwasababishia  umaskini  na uduni wa maisha.
“Sitakaa kimya kwa hawa mafataki, nitabanana nao katika kipindi chote cha madaraka yangu, hata nikitoka madarakani sitawachoka, nitaendelea  kuwalaani kwani ni watu waharibifu kwa watoto wetu,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Alisema kuna baadhi ya wazazi ambao nao wanachangia kutowapeleka watoto wao shule kwa visingizio vya ugumu wa maisha, na wengine kuwaozesha kabla ya umri nao watafikishwa mahakamani watakapobainika kuhujumu haki za watoto wao.
Alisema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali za msingi na sekondari kwa ajili ya watoto kupata elimu bora na kwamba watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kuanza mwaka huu wataingia darasani bila matatizo, kwa kuwa  miundombinu ya kila shule, vyumba vya madarasa, madawati na walimu vinakidhi kiwango.
Chanzo;tanzania Daima

MTU MMOJA AKUTWA AMEJINYONGA UFUKWE WA SPICE HOTEL

TUNAOMBA RADHI KWA PICHA


Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Bahati maarufu kwa uuzaji wa mifuko ya plastiki maeneo ya stand kuu ya mabasi Bukoba amekutwa kajinyonga juu ya mti  maeneo ya ufukwe wa Spice Motel majira ya saa nane mchana ..
Chanzo: Dj Sek Blog
 
Taarifa za awali  kutoka kwa watu waliokuwa katika tukio hilo zinasema  kuwa , kabla ya kifo cha, marehemu alionekana akiwa na mafurushi ya vitu na alikuwa akifua katika eneo hilo la ufukwe...

Mtu mmoja ambae hakuwa tayari kutaja jina lake  ameueleza  mtandao  huu  kuwa  leo majira ya saa 12.00asubuhi alisalimiana na marehemu maeneo ya stand ya mabasi akiendelea na shughuli yake ya kutembeza mifuko ya plastiki kwenye mabasi yaendayo  mikoani na maeneo mengine akiwa mzima wa afya.

Mwili wa marehemu umepelekwa Hospital ya Mkoa  wa Kagera kuifadhiwa kwa ajili ya utambuzi ( ndugu zake )

 Askari akiwa amepanda mti ili aweze kukata kamba aliyotumia kujinyonga
 Amekutwa katika hali hii
 Haijafahamika ni kwa nini kachukua maamuzi haya
 Mwili wa marehemu ukishushwa
 Kamanda wa polisi wilaya ya Bukoba akishuhudia tukio
 Wananchi waliokusanyika katika tukio
 Mkuu wa kituo cha polisi Bukoba(mwenye koti) akiwa anaangalia baadhi uya vitu vya marehemu alivyokuja navyo kabla ya kujinyonga
 Hivi ni vitu vya marehemu alivyokuja navyo babla ya kujinyonga
 Maeneo ya spice beach
 Mmoja wa watu wa kwanza kutoa taarifa kituo cha polisi Mama Faima
 Mwili wa marehemu ukipakiwa kwenye gari la polisi
Mwili wa marehemu ukipelekwa kuifadhiwa hospital ya mkoa wa kagera

Kesi 82 zafutwa kwa kukosa ushahidi

KESI 82 zilizokaa muda mrefu zimefutwa mkoani Kagera kwa kukosa ushahidi wa kutosha katika kipindi cha mwaka 2012/2013.
 Akizungumza wakati wa sherehe za Siku ya Sheria nchini, jana Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali Kanda ya Bukoba, Sakina Sinda, alisema kesi zilizofutwa zilihusisha washitakiwa wa zamani.
 Sinda alisema tatizo la kesi hizo kukaa muda mrefu linatokana na sababu mbalimbali ikiwamo mashahidi kushindwa kufika mahakamani hasa kesi za jinai. 
Alisema ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua wanajitahidi kutembelea magereza yote mkoani Kagera na kupitia majalada, lengo ni kubaini kesi zilizodumu muda mrefu bila kusikilizwa ili zitolewe maamuzi.
 “Tunajitahidi kukutana na mahabusu, kuwasikiliza na kubaini matatizo yao, baadaye tunatoa maelekezo ili kesi zao ziharakishwe,” alisema Sinda.
 Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Gad Mjemmas, alisema suala la haki kutolewa kwa wakati linakabiliwa na changamoto ikiwemo sheria za uendeshaji wa mashauri huku akitolea mfano kifungu namba 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
 Akizungumzia kifungu hicho, Jjaji Mjemmas alisema kinawataka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi  ndani ya siku 60 tangu mshtakiwa kufikishwa mahakamani lakini hakishughuliki na makosa ya kughushi na mauaji ya makusudi au ya bila kukusudia.
 Alisema hayo husababisha mshitakiwa kukaa mahabusu hata miaka 10 kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika, ambapo Mahakama hufungwa mikono kwa kutotoa unafuu kwa mshitakiwa kwa kuwa sheria haijaweka wazi ukomo wa muda wa upelelezi kwa baadhi ya makosa. 
Chanzo;Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa