Na Beatrice Lyimo
MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amewataka Viongozi wa Serikali
mkoani Kagera kuhakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya vifaa vya
misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea hivi karibuni
mkoani humo.
Waziri Jenista aliyasema hayo leo wakati alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kukagua
taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo shule za msingi ileega na
nyamilima ambazo zimeathirika kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi.
Katika
ziara hiyo, Waziri Jenista alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyerwa
kuhakikisha ukarabati wa taasisi za umma unakamilika kwa wakati ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii.
Aidha Waziri Mhagama amewataka wananchi kwa umoja wao kushirikiana katika kurejesha hali ya makazi kutokana na idadi kubwa ya wanaohitaji msaada huo.
“Nitoe
rai kwa wananchi wote kwa umoja wenu kushirikiana kwa hali na mali
katika kuhakikisha mnarejesha hali yenu ya makazi kutokana na idadi
kubwa ya wanaohitaji msaada huo”, alisema.
Mbali
na hayo Waziri Jenista aliwataka wanafunzi walioathirika na maafa hayo
kutokatisha masomo bali waendelee kama ratiba ya vipindi inavyoonyesha.
Kwa
upande wake mwalimu kutoka shule ya Msingi Ileega Anna Mollel
ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusaidia familia zilizopatwa
na athari ya tetemeko hilo na kuzipa kipaumbele shule, nyumba za walimu
pamoja na taasisi nyingine za Serikali.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment