Home » » Wananchi wameaswa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi

Wananchi wameaswa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi

 
Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi- MAELEZO Dodoma.

Wananchi wameaswa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera hivi karibuni.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George Simbachawene alipokuwa akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu Maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera siku ya jumamosi tarehe 10/09/2016.
Waziri Simbachawene amesema kuwa hadi leo tarehe 13/9/2016 idadi ya vifo vilivyosababishwa na tetemeko hilo katika Mkoa wa Kagera ni 17, ambapo majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali zilizoko Mkoani humo ni 169, majeruhi waliotibiwa na kuruhusiwa ni 83, nyumba za makazi zilizoanguka ni 840, nyumba za makazi zenye nyufa ni 1,264 pamoja na taasisi zilizoanguka na kupata nyufa ni 44.
Aidha, Waziri Simbachawene amesema kuwa mpaka sasa Serikali imechukua hatua za kuwaokoa watu na kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya muda baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zimeathirika.
Pia Serikali inaendelea kutibu majeruhi bure na wenye Bima za Afya kutumia bima zao na kuongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka mkoa ya Mwanza ili kuweza kutoa huduma ya haraka kwa wahanga hao.
Vilevile Waziri Simbachawene amesema kuwa Serikali imeelekeza wanajiolojia kuwatoa hofu wananchi kwa kutoa maelekezo ya kisayansi kuhusu hali hiyo na kuendelea kufanya tahimini ya athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Hata hivyo Waziri Simbachawene amesema kuwa serikali imezifunga shule za sekondari Ihungo na Nyakato zilizopo mkoani humo kutokana na athari za tetemeko iliyopelekea kuharibika kwa miundombinu ikiwemo madarasa, vyoo, mabweni na maabara, wakati serikali ikiendelea na taratibu za kushughulikia tatizo hilo.
Waziri Simbachawene ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa hatua za dharura zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha ili kuwasaidia wahanga.
Mbali na hayo Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi ametoa hoja juu ya wabunge kuchangia posho yao ya siku moja ili iweze kuwasaidia wahanga wa tetemeko hilo lililokadiriwa kuwa na ukubwa wa kiwango cha 5.7 katika vipimo vya Richter ambapo wabunge waliunga mkono hoja hiyo na kuridhia kuchangia kusaidia maafa hayo.
Aidha, Mbunge wa Muleba, Prof. Anna Tibaijuka ameishukuru Serikali kuwepo kwenye eneo la tukio mkoani Bukoba hatua ambayo imewapa faraja wanakagera na kutoa wito kwa wabunge na watu wenye mapenzi mema kuzidi kuwafariji wahanga hao.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charles Tizeba amesema kuwa Serikali itafanya tathmini ya kina na ya kitaalamu ili kuepuka wale ambao wanatumia maafa hayo katika kujinufaisha.
Akishukuru kwa niaba ya Serikali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewashukuru wadau wote kwa kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto na kuwahakikishia wabunge kuwa mchango wao utawafika walengwa na kuongeza kuwa jambo hilo limepelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha safari yake nchini Zambia ili kuweza kusimamia suala hilo.
Aidha, Waziri Lukuvi amesema kuwa Serikali inauchungu mkubwa juu ya maafa hayo, hivyo amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidiana na Serikali ili kuweza kuwasaidia wahanga hao  na kuwapa pole waathirika wa tetemeko hilo na kuwaombea marehemu wapumnzike kwa amani.  
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa