Na Benedict Liwenga-WHUSM, Bukoba.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January
Makamba amewatoa wasiwasi waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea
Wilayani Bukoba Mkoani wa Kagera.
Mhe.
Makamba ameyasema hayo leo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya
kutembelea maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na tetemeko hilo kwa lengo la
kuwapa pole waathirika na kuwap ujumbe wa Serikali kuhusu namna
inavyojitahidi kuwasaidia waathirika hao.
Amesema
kwamba, wananchi wasiwe na wasi wasi kuhusu suala la kupatiwa misaada
ya dharura kwani Serikali imejipanga na bado inaendelea na zoezi la
kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea ingawa zoezi la kuwapatia baadhi
ya huduma za msingi linaendele.
“Tumekuja
kutoa msaada kwa mji kwa ujumla wakati tunapanga namna ya kusaidia
katika masuala ya mazingira na tambueni kuwa Serikali inawajali ndiyo
maana kuna viongozi wakubwa wako hapa na wengine wanazidi kuja”, alisema
Mhe. Makamba.
Aliongeza
kuwa, suala la kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo limepewa uzito
mkubwa na Serikali na suala la kuchelewa kwa kutolewa kwa misaada
kunatokana na umakini unaoendelea kufanywa sasa hivi na Serikali ili
kuwatendea haki waathirika pekee.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali Denice Filangali Mwila amesema
kuwa katika Wilaya yake sehemu iliyoathirika zaidi ni Kata ya Minziro
ambapo jumla ya nyumba 512 haziwezi watu kuishi,pia nyumba 1,524 zenye
nyufa mbalimbali zinazohitaji ukarabati, Taasisi za serikali 91 na
taaisis 71 za watu binafsi ikiwemo makanisa na misikiti imeathirika na
tetemeko hilo.
Ameongeza
kuwa tayari amepata msaada wa Serikali katika tukio hilo kupitia Kamati
ya Maafa ambapo jumla ya maturubai 520 amepewa kwa ajili ya maeneo
mbalimbali, chakula, blanketi 240 ambazo pia zimegaiwa kwa waathirika
hao.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Bugandika Bw. Amudi Migeyo amewataka
wananchi wake kutobeza juhudi za Serikali zinazofanywa sasa na amewataka
kuridhika na chochote wakipatacho katika kipindi hiki kigumu.
Hivi
karibuni siku ya tarehe 10 Septemba, 2016 mkoa wa Kagera ulikumbwa na
ukubwa wa nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko la 5.7 kwa kutumia skeli
ya ‘Ritcher’ ambapo jumla ya watu 17 walipoteza maisha na majeruhi
kadhaa ambapo wengi wao wameshapatiwa matibabu na wanaendelea vizuri.
0 comments:
Post a Comment