13 KORTINI KWA KUZUIA SENSA



na Mbeki Mbeki, Bukoba
WATU 13 wamefikishwa mahakamani mkoani Kagera kutokana na kuingilia shughuli za Sensa ya Watu na Makazi na kuzuia isifanyike.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, alipokuwa akitoa taarifa ya Mkoa kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, katika ziara yake ya kiserikali mkoani Kagera.
Alisema watu hao wamefikishwa mahakamani kwa nyakati tofauti kutokana na vitendo vyao vya kukataa kuhesabiwa na baadhi yao kuhamasisha watu wengine kutoshiriki sensa katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Alisema watu hao walitoka katika Wilaya ya Misenyi (5), Manispaa ya Bukoba (5), Kyerwa (1) na Muleba (1).
Aidha, alimhakikishia Waziri Sitta kuwa taarifa zote zitakazokusanywa katika shughuli hiyo zitakuwa siri kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya mwaka 2012 na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu pekee.
Chanzo: Tanzania Daima

BREAKING NEWS: MSAFARA WA WAZIRI WA AFRIKA MASHARIKI SAMWELI SITTA UMEPATA AJALI MKOANI KAGERA


Msafara wa Waziri wa Afrika Mashariki Samweli Sitta umpata ajali Mkoani Kagera, taarifa zaidi tutakuletea.

KAGERA WASOTEA USAFIRI


na Ashura Jumapili, Bukoba
WANANCHI wa Mkoa wa Kagera jana walisotea huduma ya usafiri kutokana na mgomo wa madereva waliokuwa wakiishinikiza Manispaa ya Bukoba kupunguza tozo ya ushuru wa stendi kuu ya mabasi.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema walishindwa kufanya shughuli zao mbalimbali  kutokana na kukosa usafiri wa kuwapeleka maeneo tofauti.
Salehe Mashaka mkazi wa Kata ya Kamachumu Wilaya ya Muleba, alisema mgomo huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa sambamba na kukwaza shughuli za kiuchumi na hivyo kuwaweka katika wakati mgumu.
Alisema kuwa kufuatia mgomo huo, nauli zilipandishwa mara tatu ya nauli za awali kutoka sh 2,000 hadi sh 10,000 kwa safari za Kamachumu-Bukoba mjini.
Naye Mariam Mlama mkazi wa Wilaya ya Karagwe, alisema mgomo huo ulimfanya ashindwe kusafiri kuelekea kwenye kituo chake cha kazi.
Alibainisha kuwa alipofika stendi kuu ya mabasi mjini Bukoba akiwa amefuatana na wenzake watatu, waliambiwa kuwa nauli ya kwenda Karagwe ni sh 15,000 badala ya sh 5,000 ambayo ni nauli halali.
Aliongeza kuwa pamoja na nauli hiyo kupanda, bado hakukuwa na mabasi ya kubeba abiria kituoni hapo hali iliyowalazimu kusubiria mabasi makubwa yanayotoka Mwanza kuelekea Karagwe yanaoyoingia mjini Bukoba saa tisa alasiri.
Mmoja wa madereva wa mabasi madogo yaendayo kwenye wilaya mbalimbali yakitokea mjini Bukoba, Abdallah Msakanjia, alisema wameamua kugoma ili kuishinikiza serikali ya mkoa huo kushughulikia malalamiko yao ya ushuru wa stendi.
Alisema basi dogo (Hiace), kila linapotoka stendi hulipia ushuru wa sh 2,000 bila kujali limebeba idadi gani ya watu wakati kituo hicho hakifanyiwi matengenezo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Khamis  Kaputa, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kutokana na kubanwa na majukumu ya serikali za mitaa kwenye miji iliyoko pembezoni mwa ziwa Victoria.
Kaputa alisema atakutana na wasafirishaji Septemba Mosi mwaka huu, kuzungumzia mgomo huo.
Chanzo: Tanzania Diama

KAGERA YAHITAJI MAMILIONI KULINDA MIPAKA YA NCHI

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe

Mkoa wa Kagera unahitaji Sh. milioni 400 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukabili maeneo ya mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani zilizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkuu wa mkoa huo, Kanali mstaafu Fabian Massawe, alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mkoa huo kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Kanali Massawe alisema maeneo ya mipaka ya Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi na Kenya (upande wa Ziwa Viktoria) inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na ukosefu wa rasilimali hasa fedha, ili kukabiliana navyo.

Alisema eneo hilo ambalo kwa sehemu kubwa ni msitu, linahitaji ushiriki wa taasisi zinazounda kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, kufanikisha jitihada za kukabiliana na changamoto hizo.

Hata hivyo, Kanali Massawe alisema sehemu ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini, wanakaribishwa na wenyeji ili kushirikishwa shughili za uzalishaji kama kilimo, uvuvi na kuchunga mifugo.

Kwa mujibu wa Kanali Massawe, takwimu rasmi inayohusisha watu walioorodheshwa inaonyesha kuwepo wahamiaji haramu 35,000 mkoani Kagera.

Alisema ongezeko la wahamiaji haramu linaweza kuibua machafuko kama inavyotokea hivi sasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Alisema wahamiaji haramu kutoka nchi tofauti waliingia mashairiki ya DRC na kufanikiwa kuweka makazi ya kudumu, sasa wamekuwa chanzo cha migogoro nchini humo.

Hata hivyo, Sitta alielezea kushangazwa kwake na taarifa za kuhitajika kwa fedha hizo (Shilingi milioni 400) kwa vile serikali ilishaidhinisha zitolewe.

Akijibu baadhi ya hoja za Kanali Massawe, Sitta alisema mikoa iliyopo maeneo ya mipakani kama Kagera, inahitaji uwekezaji na uwezeshaji ili kukabiliana na changamoto ikiwemo ya kukabiliana na wahamiaji haramu.

Pia Sitta alisema ipo ya haja kwa Wakuu wa Wilaya za mpakani kuwasiliana na nchi jirani ili kuunda kamati za ujirani mwema hadi ngazi za vijiji, ili kurahisisha mwingiliano hasa unaohusu utafutaji wa mahitaji ya kibinadamu.

Alitoa mfano wa baadhi ya maeneo mkoani Kilimanjaro na Arusha yanayopakana na Kenya, serikali za vijiji zinatoa vibali vya aina hiyo, vikilenga kufika eneo lisolozidi kilomita 30 kutoka mpakani.

Akiwa katika mpaka wa Mutukula unaozitenganisha Tanzania na Uganda, Sitta alipiga marufuku vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wafanyabiashara wadogo aliowaita kuwa wajasiriamali.

Amri hiyo ilifuatilia swali aliloulizwa na mmoja wa wafanyabiashara hao, Sauda Athumani, akielezea kunyanyaswa kwao na halmashauri ya wilaya ya Missenyi kupitia kwa mzabuni wa ukusanyaji ushuru waliomtaja kwa jina moja la Kimela.
Chanzo: Nipashe

BREAKING NEWS: WASANII WA BONGO FLAVA LINEZ, SUMA LEE NA BABA LEVO WAPATA AJALI

Linex,Baba Levo na Suma Lee wamepata ajali eneo la Nyakanazi kuelekea Kigoma.
Taarifa zaidi zinakuja...

MABWENI YATEKETEA SEKONDARI MT. ALFRED


na Mbeki Mbeki, Ngara
MABWENI mawili katika Shule ya Sekondari Mt. Alfred, wilayani Ngara, Kagera, yameteketea kwa moto pamoa na mali za wanafunzi zilizokuwamo. Tukio hilo limetokea Alhamisi iliyopita, majira ya saa 3 usiku.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Jimbo la Rulenge, Sprian Vumilia, mabweni hayo yaliungua wakati wanafunzi wakiwa darasani wakijisomea.
Alizitaja baadhi ya mali zilizoteketea kwa moto kuwa ni magodoro, vitanda na nyingine ambazo thamani yake bado haijajulikana.
Alisema mabweni yaliyoteketea ni ya wavulana; Nkrumah “A” na “B”, yaliyokuwa yakichukua wanafunzi 234 wa kidato cha kwanza hadi nne.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Nidhamu wa shule hiyo, Joshua Samson, alisema chanzo cha moto huo kinasadikiwa kuwa ni hujuma ya wanafunzi tisa waliokuwa wamefukuzwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu tangu Julai 26, mwaka huu.
Alisema wanafunzi hao wa kidato cha tatu na cha nne, walifukuzwa kutokana na kujihusisha na vitendo vya uvutaji bangi, kumiliki simu na ugomvi wa mara kwa mara.
Jeshi la Polisi wilayani Ngara limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema bado linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo chake.
Wakati huo huo, mkazi wa Kijiji cha Rulenge, Maritha Runaku (75) amefariki dunia kutokana na kunywa pombe kupita kiasi.
Tukio hilo limetokea Ijumaa iliyopita, majira ya saa 2 asubuhi. Alikutwa amefariki dunia kandokando ya barabara.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, January Sakindu, alisema kuwa Maritha inasadikiwa amefariki dunia kutokana na kunywa gongo kupita kiasi na kukosa chakula, jambo lililochangia kifo chake.
Alisema Maritha alikuwa akiishi katika Kijiji cha Rulenge bila kujulikana alikozaliwa na alikuwa akifanya kazi za vibarua.
Kwa upande wake, mtendaji wa Kata ya Rulenge, Peter Kapalala, alisema uongozi wa kijiji umechukua jukumu la kumzika baada ya kuruhusiwa na Jeshi la Polisi.
Chanzo: Tanzania Daima

BUKOBA MWENYEJI MKUTANO WA LAVLAC

 
Na Audax Mutiganz, Bukoba
HALMASHURI ya Manispaa ya Bukoba itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 15 wa Ushirikiano wa Nchi za Afrika Mashariki (LAVLAC).

Kwa mujibu wa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani, mkutano huo utajumuisha halmashauri za wilaya na manispaa 130 zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Katika taaarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Amani alisema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya Jimkana vilivyoko Manispaa ya Bukoba kuanzia keshokutwa Agosti 30 mwaka huu.

Mstahiki meya huyo alisema Tanzania itawakilishwa na halmashauri za wilaya na manispaa zipatazo 28 kutoka katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

Alisema mkutano huo utaenda sambamba na maonyesho mbalimbali yanayozihusisha taasisi mbalimbali za kiserikali, mashirika ya umma na watu binafsi.

Amani alisema kauli mbiu ya mkutano huo itakuwa Serikali za Mitaa na Utatuzi wa Mabadiliko ya Tabia Nchi. Kwa mujibu wa Amani, maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika.

Alisema Manispaa ya Bukoba imeomba Rais Jakaya Kikwete awe mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kwamba manispaa yake inasubiri jibu kutoka Ikulu.

Amani aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na mkutano huo, kwa kufanya biashara ili waweze kujiongezea kipato kutokana na kuwepo kwa ugeni huo.
Chanzo: Mtanzania

BINTI WA KIHAYA ABELA ATAMBA MAREKANI, ANGALIA VIDEO YA WIMBO WAKE MPYA, BALL & CHAIN


Video mpya ya Abela inaitwa Ball & Chain. Binti huyu ambaye jina lake kamili ni Abela Kibira ana kipaji cha utunzi na uimbaji, Abela ni mzaliwa wa Bukoba, 
Tanzania lakini kwa sasa anaishi Minneapolis, Marekani.
 
Binti huyu anasauti nzuri, tena ya kipekee na ya kuvutia na kutokana na wimbo wake huu kupendwa na wengi kuna kila dalili za kuteka soko la muziki duniani.Heko Bukoba, Heko Tanzania




KAMATI YA SENSA LAWAMANI


na Mbeki Mbeki, Ngara
MAKARANI wa sensa 125 katika Kata ya Omurusagamba, wilayani Ngara, Kagera, wameilalamikia Kamati ya Sensa wilayani hapa kushindwa kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo litakalofanyika Agosti 26.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya makarani hao walisema, baada ya kumaliza mafunzo hayo yaliyochukua siku 11, wamekaa vituoni muda mrefu bila kukabidhiwa vifaa vya kufanyia kazi.
“Hii hali inatukatisha tamaa, fedha tuliyolipwa hakuna gharama ya kulala, hapa tunapoendelea kukaa tunaongezewa gharama zisizo za lazima,” alisema mmoja wa makarani hao.
Mmoja wa makarani hao, Mwalimu Privatusi Andrew, alisema uongozi wa wilaya haujatoa taarifa kwao kujua hatma ya vifaa hivyo na kutoa tahadhari kwa uongozi wa wilaya kuhakikisha vinatolewa kwa muda mwafaka.
Andrew alizitaja sehemu nyingine ambazo zimecheleweshewa vifaa vya sensa, ni Rulenge, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ilemera, Ngara Sekondari na Omurushagamba.
Pamoja na hayo, alisema makarani hao hawakupata fomu za mikataba wala kiapo cha kufanya kazi na kuongeza kuwa, mkataba uliopo una mapungufu kwani hautaji muda wa kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu, alisema makarani hao wamepewa ushirikiano wa kutosha na taratibu zote zinaendelea kama kawaida.
“Jukumu la kugawa vifaa ni letu, logistics zote zimepangwa vizuri, ninapozungumza na wewe magari yanazunguka kugawa vifaa,” alisema Kanyasu na kuwataka makarani hao kuwa wavumilivu muda wa kugawa vifaa bado upo.
Chanzo: Tanzania Daima

MNYAUKO WA MIGOMBA WAANZA KUZUA BALAA KAGERA


Na Audax Mutiganzi, Bukoba
UGONJWA wa mnyauko unaoshambulia migomba umeanza kuathiri upatikanaji wa ndizi katika maeneo mbalimbali mkoani Kagera.

Ugonjwa huo ambao hadi sasa haujajulikana unasababishwa na nini, unasambaa kwa kasi, hasa katika maeneo ya wilaya za Muleba na Karagwe, Misenyi na Bukoba ambazo zimekuwa zikizalisha ndizi kwa wingi mkoani Kagera.

Ugonjwa huo umesababisha kupungua kwa uzalishaji wa ndizi mkoani hapa, jambo ambalo limechangia kupanda kwa bei ya ndizi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba katika soko kuu la Bukoba ndizi kubwa zinauzwa kwa wastani wa kati ya Sh 15, 000 hadi 20, 000 ambapo miaka iliyopita ndizi hizo ziliuzwa kwa kati ya Sh 6,000 hadi 8,000.

Kupanda kwa bei ya ndizi iliyochangiwa na ugonjwa wa mnyauko wa migomba kumewalazimisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kagera ambao hutegemea ndizi kama chakula chao kikuu kubadilika na sasa wanalazimika kula ugali na wali.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera wamelazimika kubadili fikira zao za kudhani kuwa ndizi ndicho chakula kikuu baada ya kushindwa kumudu gharama za kununua ndizi katika masoko kutokana na bei yake kuwa kubwa.

Baadhi ya wakulima bora wa migomba mkoani hapa ambao mashamba yao yameathirika kutokana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba ni pamoja na Kamishina Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Alfred Tibaigana.

Kamishina Tibaigana shamba lake lililoko katika kijiji cha Buganguzi wilayani Muleba limeathirika sana. Mkulima huyu kabla ya ugonjwa huu alikuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 40 za ndizi kwa wiki, ambapo sasa anazalisha wastani wa tani zisizozidi 10 kwa wiki.

Baadhi ya wakulima mkoani Kagera wameitahadharisha serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi, ili zao la ndizi lisibaki katika vitabu vya historia.

Kwa upande wake Sai Bulili, mtafiti wa Kituo cha Mazao cha Maruku kilichoko katika Wilaya ya Bukoba vijijini, alisema ugonjwa wa mnyauko hadi sasa bado haujapata tiba.

Bulili alisema wakulima ili waweze kuepukana na ugonjwa huo ni lazima wafuate tararibu zote za kupambana na ugonjwa huo wanazoelekezwa na wataalamu wa kilimo, ambazo ni pamoja na kuing'oa na kuichoma moto miche yote ya migomba inayoonyesha dalili za ugonjwa huo.
Chanzo: Mtanzania
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa