na Mbeki Mbeki, Ngara
MABWENI mawili katika Shule ya Sekondari Mt. Alfred, wilayani Ngara, Kagera, yameteketea kwa moto pamoa na mali za wanafunzi zilizokuwamo. Tukio hilo limetokea Alhamisi iliyopita, majira ya saa 3 usiku.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Jimbo la Rulenge, Sprian Vumilia, mabweni hayo yaliungua wakati wanafunzi wakiwa darasani wakijisomea.
Alizitaja baadhi ya mali zilizoteketea kwa moto kuwa ni magodoro, vitanda na nyingine ambazo thamani yake bado haijajulikana.
Alisema mabweni yaliyoteketea ni ya wavulana; Nkrumah “A” na “B”, yaliyokuwa yakichukua wanafunzi 234 wa kidato cha kwanza hadi nne.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Nidhamu wa shule hiyo, Joshua Samson, alisema chanzo cha moto huo kinasadikiwa kuwa ni hujuma ya wanafunzi tisa waliokuwa wamefukuzwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu tangu Julai 26, mwaka huu.
Alisema wanafunzi hao wa kidato cha tatu na cha nne, walifukuzwa kutokana na kujihusisha na vitendo vya uvutaji bangi, kumiliki simu na ugomvi wa mara kwa mara.
Jeshi la Polisi wilayani Ngara limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema bado linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo chake.
Wakati huo huo, mkazi wa Kijiji cha Rulenge, Maritha Runaku (75) amefariki dunia kutokana na kunywa pombe kupita kiasi.
Tukio hilo limetokea Ijumaa iliyopita, majira ya saa 2 asubuhi. Alikutwa amefariki dunia kandokando ya barabara.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, January Sakindu, alisema kuwa Maritha inasadikiwa amefariki dunia kutokana na kunywa gongo kupita kiasi na kukosa chakula, jambo lililochangia kifo chake.
Alisema Maritha alikuwa akiishi katika Kijiji cha Rulenge bila kujulikana alikozaliwa na alikuwa akifanya kazi za vibarua.
Kwa upande wake, mtendaji wa Kata ya Rulenge, Peter Kapalala, alisema uongozi wa kijiji umechukua jukumu la kumzika baada ya kuruhusiwa na Jeshi la Polisi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment